Tabia ya Utoro Bungeni yajirudia Tena

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA

Tabia ya utoro bungeni imejirudia tena mwaka huu wakati Bunge likijadili Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika. Safari hii utoro huo unawahusisha mawaziri na siyo wabunge.

Tukio kama hilo liliwahi kutokea Julai 22, mwaka jana wakati wa mjadala wa Bajeti wa Wizara hiyo kiasi cha kufanya moja ya vikao vyake kuahirishwa kutokana na utoro wa wabunge.

Kutokana na utoro huo, jana asubuhi, Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola alilazimika kuomba mwongozo kwa Naibu Spika, Job Ndugai ili aone haja ya kusimamisha mjadala wa Wizara ya Kilimo kutokana na idadi ndogo ya mawaziri waliokuwamo ukumbini.

Lugola alisema Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika ni mtambuka kutokana na kuajiri zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania na kwamba kutokana na nchi kukabiliwa na tatizo la chakula hivi sasa, inapojadiliwa inahitaji umuhimu wa kipekee.

Mbunge huyo, ambaye amejizolea sifa ya kuihoji Serikali bila ya woga alisema katika kipindi hicho, kulikuwa na mawaziri watano na manaibu watano pekee ukumbini.
Baraza la Mawaziri linaundwa na mawaziri 56, ambao ni Waziri Mkuu, mawaziri 30 na manaibu waziri 25.

“Wizara hii ni mtambuka lakini kuna mawaziri 10 pekee humu ndani, wakiwamo mawaziri watano na manaibu watano, hivyo Mheshimiwa Naibu Spika naomba mwongozo wako kama ni sawa kuendelea na mjadala huu katika hali hii,” alisema Lugola.

Hata hivyo, mwandishi wetu aliwashuhudia mawaziri 13 ukumbini humo wakati huo ambao ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk Mary Nagu na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi), Celina Kombani na Waziri wa Chakula, Kilimo na Ushirika, Christopher Chiza.

Manaibu Waziri waliokuwamo ni Angela Kairuki (Katiba na Sheria), Stephen Masele (Nishati na Madini), Dk Binilith Mahenge (Maji), Aggrey Mwanri (Tamisemi), Saada Mkuya (Fedha) na Goodluck Ole-Medeye (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi).

Akitoa mwongozo wake, Naibu Spika, Ndugai alisema mawaziri wote wapo Dodoma hata kama hawakuwamo ukumbini wakati huo na walikuwa wanashughulika na mambo mbalimbali ya bajeti zao.

“Mawaziri wote wapo Dodoma wanaweka mambo yao sawa, ili wakija hapa wasipate shida, lakini niwaambie tu kuwa wanafuatilia kwa karibu kila kitu kinachoendelea hapa,” alisema Ndugai.

Akihitimisha kipindi cha asubuhi cha Bunge baadaye jana, Ndugai alisisitiza umuhimu wabunge kuhudhuria kipindi cha jioni kwa kuwa wizara hiyo ilikuwa inahitimisha mjadala huo.

Historia yajirudia
Julai 22 mwaka jana, Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia alisimama kuomba mwongozo wa Naibu Spika, Job Ndugai kutokana na Bunge kutokuwa na nusu ya wabunge wote kinyume cha Kanuni ya Bunge wakati wa Bajeti ya Wizara hiyo ya Kilimo, Chakula na Ushirika.

“Idadi ya wabunge wote ni 352 lakini wabunge waliomo humu ndani haizidi 110, ambapo nusu ya wabunge wote ni 176 hivyo kuendelea kupitisha bajeti hiyo ni kuvunja kanuni,” alisema Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi.
Baada ya kujiridhisha kwamba idadi hiyo ilikuwa ndogo, Naibu Spika aliahirisha kupitishwa kwa Bajeti hiyo.
-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad