Star Tv Yaitunishia Kifua TCRA yaweka ngumu

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA


Siku moja baada ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuagiza matangazo ya Star TV yarejeshwe kwenye kisimbuzi cha Star Times ifikapo saa 10 jioni jana, televisheni hiyo imegomea agizo hilo na imetishia kwenda mahakamani ikiwa italazimishwa kurejea humo. Taarifa ya kugoma agizo hilo, ilitolewa jana na Meneja Mipango na Utafiti wa Sahara Media Group Ltd, Kampuni inayomiliki Star TV, Nathan Lwehabura.
Ilieleza kuwa kinachofanywa na TCRA, kuwalazimisha kurejesha matangazo Star Times ni ukiukwaji wa Sheria ya Hatimiliki na Sheria ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010.
“Serikali ya Tanzania ni mwanachama wa WTO na pia WIPO (World Intellectual Property Rights Organization) na hivyo kwa kulazimisha uvunjaji wa sheria za hati miliki ina maana inavunja haki zetu zilizopo kikatiba! Tutakwenda mahakamani kupata haki yetu hii muhimu,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Pamoja na kutoweka bayana lini watakwenda mahakamani, Lwehabura alisema sheria ya hati miliki inaweka
kinga kwa vipindi vya redio, televisheni, nyimbo na sanaa. Alisema kulazimisha Star Times kupora vipindi vya Star TV, inadhihirisha kilio cha wasanii wa Tanzania, wasivyolindwa na Serikali yake. Taarifa hiyo ilieleza Mei 23 mwaka huu, Star TV kupitia mwanasheria wake iliwataka Star Times kuiondoa kwenye kisumbuzi chao ifikapo saa sita usiku wa Mei 31, mwaka huu kutokana na kurusha na kuuza maudhui na vipindi vyake bila idhini na kukiuka sheria za haki miliki (Copyright laws).
“Katika barua hiyo, Star TV iliwakumbusha Star Times kwamba hawakuwa na mkataba wa kurusha kituo hicho kwa mujibu wa sheria ya EPOCA, pia hawana haki ya kutumia maudhui yake bila idhini chini ya Sheria ya Haki miliki ya Tanzania na kimataifa,” ilieleza taarifa hiyo.
Hata hivyo, Mei 31 Star Times/Star Media walijibu kwamba hawajakiuka sheria yoyote. Walisisitiza wataendelea kuirusha Star TV, kutekeleza matakwa ya sheria ya EPOCA na kanuni zake. Lakini, Star TV iliwaandikia tena na kuwaeleza itachukua hatua zaidi kwa kukiuka ;na kuwataka iwaondoe saa sita usiku wa Juni 8, mwaka huu.
Tarehe 6 Juni mwaka huu, Star TV iliwaandikia tena Star Times ikisisitiza nia yake ya kuchukua hatua zaidi, kutokana na wao kuendelea kukaidi ombi hilo na kuainisha mapungufu kadhaa ya kisheria kwa upande wao, yanayoifanya Star TV ijiondoe kwenye king’amuzi chao ifikapo saa sita usiku wa tarehe 8 Juni, mwaka huu na kufanya hivyo.
Jana, TCRA, kupitia Mkurugenzi Mkuu, Profesa John Nkoma, iliagiza chaneli hiyo irejeshwe mara moja jana ifikapo saa 10 jioni na kuzitaka pande hizo mbili, kukutana na mamlaka Juni 17 mwaka huu kwa majadiliano zaidi.
Hata hivyo, mpaka jana saa 11.20 jioni, Star TV haikuwa inaonekana kwenye Star Times huku TCRA ikidai Star TV inakiuka sheria ya EPOCA na ikikaidi, itachukuliwa hatua kwa kuwa si yenyewe wala Star Times walioko sawa katika maamuzi hayo.
TCRA iliwataka watoa huduma hao kufuata Sheria, inapotokea kutokuafikiana katika jambo fulani badala ya kutoa maamuzi bila kumshirikisha Mdhibiti (TCRA), kwani kufanya hivyo ni kuwakosea haki wananchi.
Hata hivyo, Star TV imesema haipo tayari kuona maudhui yake yakiuzwa nje ya nchi bila makubaliano. Star Times jana hawakuwa tayari kuzungumzia suala hilo. Lakini, awali, Msaidizi wa Meneja wa Star Times, Hellen Elisa alithibitisha kujitoa kwa Star TV. Alisema waliwaandikia barua na kudai wamejitoa kwa matakwa yao.
-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Bora mngetuwashia ANALOJIA yetu maana naona mnatupatia MAUZAUZA tusiyoyaelewa huyu anasema hiki na yule nae anasema kile na hao wadhibiti nao wanasema yao, hakuna tunaemuelewa. je TVZ , MLIMANI TV zinapatikana KISIMBUZI kipi ? michelin

    ReplyDelete

Top Post Ad