BAADA YA SHULE KUFUNGULIWA JANA GIZA NENE KIDATO CHA TANO

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA

Matokeo mabaya ya kidato cha nne ya mwaka 2012, yameendelea kuitikisa sekta ya elimu nchini baada ya shule kufunguliwa jana bila kutangazwa kwa waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano mwaka huu.
Kwa kawaida, wanafunzi wanaochaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ualimu, hutangazwa mapema ili kutoa fursa kwa wanafunzi na shule husika kufanya maandalizi ya mahitaji.
Lakini tofauti na ilivyozoeleka, wanafunzi wa kidato cha sita walianza masomo yao jana huku wale wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ualimu wakiwa hawajatangazwa.
Mkanganyiko huo pia unazigusa shule za sekondari za binafsi kwani baadhi zilishachukua wanafunzi wa kidato cha tano na nyingine ziliahirishwa kufunguliwa jana kutokana na kutokuwa na wanafunzi hao.
Hali hiyo imewaacha njia panda baadhi ya wakuu wa shule ambao waliwaambia waandishi wetu kwa nyakati tofauti kwamba wanasubiri maelekezo ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuhusu suala hilo, huku wengine wakitishia kufunga shule hizo na kuzigeuza kuwa vyuo vya taaluma nyingine.
Akitangaza matokeo mapya ya kidato cha nne Mei mwaka huu, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa aliahidi kwamba majina ya watakaojiunga na kidato cha tano yangetangazwa mapema ili wapate muda wa kujiandaa na kuripoti kwenye shule husika mapema kadri itakavyowezekana.
Jana, Dk Kawambwa hakupatikana kuzungumzia suala hilo na msemaji wa Wizara hiyo, Bunyanzu Ntambi alisema suala la kutangaza majina hayo lipo kwenye ngazi za uamuzi.
“Sababu hasa siwezi kujua, lakini kwa kuwa matokeo yenyewe yalichelewa kutangazwa ni rahisi hata mchakato wa kutangaza waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano uchelewe,” alisema Bunyanzu.
Wakuu wa shule
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Morogoro, Thomas Chihwalo alisema: “Ninachosubiri ni maelekezo ya wizara, nini kifanyike.”
Mkuu wa Sekondari ya Azania, Dar es Salaam, Benard Ngoyaye alipoulizwa alisema: “Nenda kwa Ofisa Elimu wa Wilaya, yeye anafahamu kwa nini majina yamechelewa kufika wakati walikwishachaguliwa.” Mkuu wa Shule ya Sekondari Arusha, Christopher Malamusha alisema walitarajia wizara ingetangaza majina hayo mapema lakini hadi jana walikuwa hawajapokea taarifa zozote.
Mkuu wa Sekondari ya Tambaza aliyejitambulisha kwa jina moja, Zuberi naye alisema wanasubiri maelekezo ya Ofisa Elimu Wilaya ya Ilala.

Hata hivyo, Ofisa Elimu ya Sekondari wa Manispaa ya Ilala, Germana Mng’aho alisema asingeweza kuzungumzia suala hilo na kwamba mhusika mkuu ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Ilboru, Arusha, Julius Shula alisema hata majina ya wanafunzi wanaojiunga na shule yao hawayafahamu.
Mmoja wa walimu wa Shule ya Sekondari ya Jangwani, Dar es Salaam, alisema kwa kawaida wanafunzi wa kidato cha tano huripoti shuleni wiki mbili kabla ya wale wa kidato cha sita kitu ambacho mwaka huu kimekuwa tofauti. Msaidizi wa Mkuu wa  Shule ya Sekondari Bwiru Wavulana ya Mwanza, Malongo Charles alisema wanasubiri wanafunzi watakaopelekwa na Serikali.
Hata hivyo, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Moshi, Fanuel Angalo alisema anaamini wizara husika itatangaza wiki hii.
“Ni jambo jipya kidogo limetokea lakini tunaamini Waziri atatoa tangazo lake wiki hii halafu wanafunzi hao wa kidato cha tano waripoti shuleni wiki ijayo,” alisema Angalo.
Mkoani Tanga, walimu katika Shule za Sekondari za Tanga Ufundi, Gallanos na Usagara kwa nyakati tofauti, waliilalamikia wizara kwa kuwachelewa kuwapelekea wanafunzi wa kidato cha tano na kusema kuwa hiyo imevuruga utaratibu wa ufundishaji.
Hakuna athari
Baadhi ya wadau wa elimu walisema kilichotokea si kigeni kwani kimepata kutokea miaka ya nyuma na mihula ilirekebishwa na kwenda sawa na wenzao ambao walikuwa wameanza masomo.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Ushauri wa HakiElimu, Nyanda Shuli alisema kubadilika kwa muhula wa kuanza masomo si jambo kubwa ambalo linaweza kuathiri elimu na kwamba anaamini wizara itakuwa imetoa mwongozo.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Dk Kitila Mkumbo alisema si mara ya kwanza kwa muhula wa masomo kubadilika kwani imewahi kutokea siku za nyuma na marekebisho yakafanywa ili kufidia muda ambao wanafunzi wanakuwa wamepishana na wenzao.
“Sidhani kama ni jambo kubwa sana ambalo linaweza kuathiri chochote katika masuala ya elimu, la msingi ni kuhakikisha kuwa waliochelewa kuanza masomo wanapata muda wa kumaliza mtaala (mtalaa) wa masomo kama inavyotakiwa.”
Kwa siku tatu mfululizo, kuanzia Juni 29, mwaka huu, wakuu wa shule za sekondari za Serikali walikutana katika Chuo cha Ufundi, Arusha kupitia majina ya waliochaguliwa na kuiachia kamati ya kukamilisha kazi hiyo.
Hata hivyo, habari kutoka ndani ya kikao hicho zinasema tatizo kubwa lilikuwa ni idadi ya wanafunzi kuwa ndogo ikilinganishwa na nafasi za kidato cha tano kutokana na kufeli kwa wanafunzi wengi katika matokeo ya kidato cha nne, 2012.
-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad