SURA HALISI YA UCHAFU DAR ES SALAAM YAREJEA SIKU MOJA BAADA YA OBAMA KUONDOKA TANZANIA

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Rais wa Marekani, Barack Obama kuondoka nchini, maisha kwa wakazi wa Dar es Salaam yamerejea katika hali ya kawaida, huku baadhi ya wafanyabiashara na ombaomba wakirejea kwa kasi maeneo yaliyosafishwa wakati wa ujio huo.

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ilianzisha operesheni maalumu ya usafi kabla na wakati wa ujio wa Obama, hatua iliyopokewa kwa mtazamo tofauti na wakazi hao.

Timu ya Mwananchi iliyovinjari kona mbalimbali za Dar es Salaam jana, ilishuhudia wafanyabiashara wakirudi huku wengine wakijenga upya vibanda vilivyobomolewa.

Kwa nyakati tofauti, baadhi ya wafanyabiashara hao, walisema changamoto za maisha zinazowakabili ndizo zimewasukuma kurejea, kwa sababu hawana kazi wala sehemu nyingine ya kufanyia biashara zao.

Kituo cha Mabasi Mwenge, kulikuwa na wafanyabiashara wachache walioanza kurudi taratibu kwa kuvizia.

Mwananchi ilikutana na ombaomba kadhaa Barabara ya Sam Nujoma na ile inayoelekea Kiwanda cha CocaCola Kwanza Mikocheni, huku polisi waliokuwa makutano hayo wakiwaangalia bila kufanya chochote.

Wafanyabiashara hao walisema wameamua kuendelea kufanya biashara zao kutokana na hali ngumu ya maisha inayowakabili.

Katika maeneo ya Ubungo, wafanyabiashara ndogondogo walionekana kuendelea na biashara hususan pembezoni mwa barabara, Ubungo Darajani na ndani ya Kituo cha Daladala cha Ubungo.

Hata hivyo, licha ya kuendelea na biashara hizo, baadhi yao wameonyesha wasiwasi kufungua kwenye maeneo hayo waliyofukuzwa awali, kwani hakuna tamko lililowaruhusu kuendelea.

Mmoja wa wafanyabiashara hao, Jabir Hamis, alisema: “Nashukuru kumalizika kwa ziara ya Rais Obama nchini, kwani tuna siku mbili hatujafanya biashara.”

Wafanyabiashara wengine waliorudi maeneo ya Ubungo, ni wale wanaofanya biashara za nguo katika makutano ya Barabara za Mandela, Sam Nujoma na Morogoro na bodaboda wanaoegesha Kituo cha Tanesco.

Tabata Relini karibu na Ofisi za Mwananchi Communications Limited (Ltd), wafanyabiashara ndongondogo waliovunjiwa vibanda, walianza kujenga mabanda yao na kurudi kwa kasi.“Sisi bwana, tumerudi kwa sababu hapa tunajipatia kula. Ni kweli tupo kinyume cha sheria, lakini hatuna jinsi hapa ndipo tunapopata riziki zetu, nasomesha watoto kwa kazi hii ya mamalishe,” alisema mmoja wa mamalishe ambaye hakutaka kutajwa.
Maeneo ya Buguruni, wafanyabiashara wanaopanga bidhaa zao pembezoni mwa barabara, walirejea na kuendelea na shughuli zao kawaida.

Wauza nguo za mitumba wamerejea eneo la Bakhresa, walisema wao wanaamini waliondolewa kupisha msafara wa Obama, baada ya hapo wanaendelea.

Hali ya uchafu nayo ilionekana kurejea eneo hilo, mifuko ya plastiki na makaratasi yalionekana kuzagaa barabarani ambayo Jumanne ilikuwa iking’aa kwa usafi.

Maeneo ya Kariakoo kwenye makutano ya Barabara ya Uhuru na Msimbazi, lilionekana katika hali ya usafi na kuvutia kama ilivyokuwa wakati wa ujio wa Obama, ingawa wafanyabiashara walianza kurudi kwa kuvizia mgambo.

Takriban wiki moja kuelekea ujio wa Obama, maeneo mbalimbali ya katikati ya Dar es Salaam na pembezoni, yalikuwa katika hali ya usafi na wafanyabiashara waliokuwa wakipanga bidhaa pembezoni mwa maeneo yasiyo rasmi waliondolewa.

Imeandaliwa na Daria Erasto, Benjamini Mwangoka, Muka Mkufya, Minael Msuya na Amelda Ringo.
-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad