VIONGOZI CHADEMA WAZIPIGA KAVU KAVU KWENYE MKUTANO WA MBOWE ARUSHA

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA

Arusha. Mkutano wa Baraza la Uongozi la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kaskazini juzi uligeuka ukumbi wa ngumi, baada ya Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba kushushiwa kipigo.

Mwigamba alishushiwa kipigo hicho na baadhi ya viongozi wenzake wa chama kwa madai ya usaliti na tayari amesimamishwa uongozi kwa muda usiojulikana.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas jana alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo na viongozi hao wa Chadema kufikishana polisi.

 Alikutwa na zahama hiyo mbele ya viongozi wakuu wa Chadema Taifa, Mwenyekiti, Freeman Mbowe na mwasisi wa chama hicho, Edwin Mtei katika Hoteli ya Coridal Spring.

Viongozi hao wamekuwa wakifanya ziara za aina hiyo nchi nzima, kuimarisha chama na kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwakani na uchaguzi mkuu ujao wa Rais na wabunge mwaka 2015.

Habari kutoka ndani ya mkutano huo zinaeleza kuwa hatua hiyo ilifuatia tuhuma kwamba Mwigamba alituma ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Jamii Forums, unaodaiwa kukichafua chama hicho.

 Tukio hilo la aina yake lilitokea wakati viongozi wote wa juu wa chama hicho, wakiongozwa na Mbowe walipokuwa wakijadili mustakabali wa chama hicho, mkutano ambao ulihudhuriwa na wabunge karibu wote wa Chadema wa kanda hiyo.

 Hata hivyo, wakati mijadala ikiendelea baadhi ya viongozi wa chama hicho, akiwamo Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema walimtuhumu Mwigamba kutuma ujumbe kwenye mtandao huo, uliokuwa ukizungumzia ufisadi ndani ya chama hicho, wakidai alitaka Mwenyekiti Mbowe kukubali kuchunguzwa.  

Akizungumza na Mwananchi Jumapili jana, Mwigamba alisema kuwa baada ya Lema kutoa tuhuma hizo aliungwa mkono na viongozi wengine na vijana waliokuwa wameimarisha ulinzi, kumvamia na kuanza kumpiga pamoja na kumnyang’anya kwa nguvu kompyuta mpakato (Laptop), aliyokuwa nayo, kisha kumpeleka Kituo Kikuu cha Polisi, mjini Arusha.  

“Wamenipiga sana na kuniweka ndani, ila nashukuru Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Arusha (OCCID),  alikuja na kunitoa saa 5:00 asubuhi,” alisema Mwigamba.

Alisema kuwa leo katika mkutano wake na waandishi wa habari ataeleza yote yaliyotokea na hatua atakazochukua, kwa kuwa yeye ni kiongozi wa juu wa chama. 


Hata hivyo, alieleza kwamba bado anashauriana na wanasheria wake kuona kama anaweza kuwachukulia hatua waliompinga.


Kauli ya polisi

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema polisi wameona hakuna kosa la kisheria lililotokea hasa kutokana na malalamiko yaliyofikishwa kwao dhidi ya Mwigamba ya kukichafua chama kwenye mitandao.

 “Hili suala la mitandao ni kubwa na lina taratibu zake sasa kusema tu umechafuliwa na iwe kesi nadhani uchunguzi unahitajika kwao, sisi tumeona haya ni mambo yao wanaweza kuyamaliza wao ndiyo sababu tulimwachia, Mwigamba,” alisema Sabas.

Kosa analodaiwa kufanya Mwigamba

 Akizungumzia sakata hilo jana, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alisema kwamba Mwigamba alibainika kutuma ujumbe kwenye mtandao wa Jamii Forums uliokichafua chama hicho, akieleza haikuwa mara yake ya kwanza kwa kiongozi huyo kufanya hivyo na kwamba walikuwa wakimfuatilia kwa muda mrefu.

 “Kilichotokea ni hicho, vijana wa Red Brigade ndio waliomtoa ukumbini, baada ya kumbaini kukichafua chama, kwani laptop yake baada ya kuchunguzwa na wataalamu wetu walijiridhisha ni yeye ndiye aliyetuma ujumbe huo,” alisema Lema.

Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa alitaja tuhuma zinazomkabili Mwigamba kuwa ni pamoja na kusema uongo, kupotosha taarifa za chama na kuchonganisha viongozi kupitia mtandao wa kijamii ya Jamii Forums.

Katika andiko lake kwenye mtandao, Mwigamba anadaiwa kuwatuhumu viongozi wa juu wa Chadema akiwamo Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk Wilbrod Slaa kuwa wamechakachua katiba ya chama hicho kuhusu ukomo wa nafasi za uongozi ili kujinufaisha binafsi.

Golugwa alisema kuwa baada ya kubanwa kwenye kikao, Mwigamba alikiri kuandika na kurusha taarifa hizo kwenye mitandao, lakini alipotakiwa kukabidhi kompyuta yake ili ichunguzwe na wataalamu wa mawasiliano wa chama hicho aligoma, hali iliyozua tafrani kati yake na walinzi wa chama hicho (Red Brigade), waliolazimika kutumia nguvu kumdhibiti.

Purukushani zilivyotokea

Habari zaidi zinaeleza kuwa katika harakati za kutaka kumnyang’anya Mwigamba kompyuta yake, mwenyekiti huyo wa Chadema mkoani Arusha alianza kushambuliwa na baadhi ya viongozi wa Chadema, kabla ya kufanikiwa kumdhibiti.


Zinaeleza kuwa katika tukio hilo kulitokea pia kurushiana maneno na matusi ya nguoni kati yake na viongozi wengine wa chama hicho akiwamo Lema.

Baadaye Lema aliliambia gazeti hili kwamba katika purukushani hizo Mwigamba alimrushia ngumi ambayo hata hivyo aliikwepa.

 Alisema kuwa wanakusudia kumfungulia kesi Mwigamba ya kukichafua chama chao katika mitandao ya kijamii.

 Hata hivyo, alisema kikao chao kiliendelea jana bila ya vurugu zozote na kuweka mikakati ya kushinda majimbo yote ya Kanda ya Kaskazini mwaka 2015 na kuchukua nchi katika uchaguzi huo ujao.

Adhabu kwa Mwigamba

Katika hatua nyingine Chadema, kimemsimamisha uongozi Mwigamba kwa tuhuma za kukisaliti, kukihujumu chama hicho na viongozi wake.

Akitangaza uamuzi huo mbele ya waandishi wa habari jijini Arusha jana, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Israel Natse alibainisha kuwa uamuzi wa kumsimamisha Mwigamba katika nyadhifa zote za uongozi ndani ya chama ulifikiwa na kikao cha Baraza la Uongozi wa Kanda ya Kaskazini kilichokutana juzi.

Alisema kuwa Mwigamba amesimamishwa kwa muda usiojulikana kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake na kuonya kuwa iwapo tuhuma zitathibitishwa, hatua nyingine za kinidhamu zitafuata kulingana na kanuni na katiba ya Chadema.

“Kwa sasa Mwigamba anatuhumiwa kuvunja sura ya kumi, kifungu cha 10.1 kifungu kidogo cha 8, 9 na 10 ya katiba ya Chadema inayozungumzia maadili ya uongozi,” alisema Natse.


Akifafanua zaidi alisema kuwa sura na vifungu hivyo vinakataza kiongozi wa chama hicho kutoa tuhuma dhidi ya viongozi wenzake bila kufuata vikao halali vya kikanuni na kikatiba.

Udaku Specially Blog
-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. huyo ametumwa inabidi adhibitiwe chadema juu upumbavu msiukumbatie

    ReplyDelete

Top Post Ad