SEREKALI YAZIDI KUYAANDAMA MAGAZETI LINGINE LAPIGWA MKWAEA MZITO

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA

KWA mara nyingine serikali imeendelea kuandama vyombo vya habari viwili ilivyovifungia wiki iliyopita, magazeti ya Mwananchi na Mtanzania.

Jana ilitishia kuchukua hatua kali dhidi ya gazeti la Rai (dada wa Mtanzania) ikisema iko tayari kulifunga iwapo litaendelea kuchapishwa katika siku tofauti na Alhamisi.

Kupitia kwa Mkurugenzi wa Habari (MAELEZO), Assah Mwambene, serikali jana ilisema haitaki kuliona gazeti la Mwananchi mtandaoni kama ambavyo hailitaki mitaani.

Mwambene alipiga marufuku magazeti hayo kuonekana popote, kwa njia yoyote, kabla hayajamaliza kifungo.

Mwambene alisema kuwa gazeti la Mwananchi baada ya kufungiwa limeendelea kutoa habari zake kupitia tovuti ya gazeti lao kinyume cha amri iliyotolewa na kwamba serikali imewaandikia kuwataka kuacha mara moja la sivyo watalazimika kuchukua hatua kali zaidi.

“Kampuni ya New Habari 2006 baada ya kufungiwa moja ya magazeti yake, imeanza  kuchapisha gazeti la ‘Rai’ kila siku tangu  Septemba 29, mwaka huu bila ya kibali cha Msajili wa Magazeti,” alisema.

Hata hivyo, amri ya serikali ya kuzuia Rai kutoka kila siku hasa baada ya Mtanzania kufungiwa siku nne zilizopita, imekumbana na upinzani mkali kutoka kwa uongozi wa New Habari.

Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano kwa njia ya simu, Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Hussein Bashe, alisema kuwa kauli ya mkurugenzi wa MAELEZO inaonyesha bayana jinsi serikali ilivyokusudia kuiangamiza kampuni yake.

Bashe alimshambulia Mwambene akidai kuwa huenda mkurugenzi huyo hajui sheria za kuendesha makampuni au ana nia mbaya na tasnia ya habari nchini kwa sababu Rai imesajiliwa na ina kibali cha kutolewa kila siku.

“Rai ni gazeti lililosajiliwa kutoka kila siku kwa kibali cha serikali kilichotolewa na msajili wa magazeti Desemba 22, 1994 kwa barua yenye kumb: IH/TN/283/12. Barua hiyo inasema: ‘Yah kuchapicha gazeti la Rai kila siku’ na kutiwa saini na Dominica C. Haule, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo).

Hata hivyo, Mwambene pamoja na kukiri barua hiyo, amedai kuwa ilitolewa kwa kampuni ya Habari Corporation, na sio New Habari (2006) Ltd, iliyonunua hisa za Habari Corporation.

Mwambene alisema kwa msingi huo, Rai haiwezi kuchapishwa kila siku kama anavyojaribu kusema Bashe katika utetezi wake.

Hata hivyo, Bashe alionekana kushangazwa na kauli ya mkurugenzi huyo na kuhoji uelewa wake kuhusiana na sheria za biashara za kununua na kuuza kampuni.

Alihoji ikiwa kampuni ilinunua hisa zote, itashindwaje au kuzuiwa vipi kuendelea na uendeshaji wa shughuli ikiwa imenunua mali zote na hivyo kuwa halali kuendeleza shughuli zinazotakiwa.

“Sisi tulichofanya ni kuitaarifu tu idara ya habari kwamba sasa tutaendelea na kuchapa kila siku na tulifanya hivyo Jumamosi. Sasa tunashangaa anaendelea tena kutusakama. Kuna nini hapa?” alihoji Bashe kwa mshangao.

Mwambene alisema kuwa serikali  imeyafungia  magazeti ya hayo kwa kuzingatia  Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976 na kanuni zake za mwaka 1977.

Alisema kuwa umma unapaswa kufahamu kuwa serikali  haikukurupuka  kufungia magazeti hayo, baada ya kufuata taratibu zote za msingi ikiwemo kuwasikiliza wahusika.

“Mwananchi limefungiwa kwa muda wiki mbili kuanzia  Septemba 27, mwaka huu, na Mtanzania limefungiwa kwa muda wa miezi mitatu au siku 90 kuanzia  Septemba 27, mwaka huu,” alisema.

Aidha, serikali imelaumiwa kwa tamko lake la kulitaka gazeti la Mwananchi kutowekwa mtandaoni mambo ambayo wachunguzi wanasema yalipaswa kufanywa na mamlaka ya mawasiliano (TCRA), ambayo ndiyo yenye mamlaka na mambo ya mitandao nchini kama kulikuwa na ukiukwaji uliofanyika.

Wadau  wanasema tofauti za kimajukumu kati ya Idara ya Habari na Mamlaka ya Mawasiliano nchini ziko bayana ndio maana hata Rais Jakaya Kikwete alitofautisha Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, huku nyingine inayohusisha mambo ya mitandao ikiwa chini ya Mawasiliano Sayansi na Teknolojia.

Hatua hiyo ya serikali imezidisha mpasuko mkubwa kati ya utawala na vyombo vya habari, mashirika ya kiraia ndani na nje ya nchi.

Taasisi na mashirika hayo yamelaani hatua hiyo, huku yakiitaka serikali kuacha kuzuia haki ya wananchi ya kujieleza na kupokea habari na mengine yakienda mbali zaidi na kutuhumu kuwepo kwa hujuma ya kuwanyima wananchi habari zinazoendelea kujiri katika mchakato wa Katiba au kuwapa yale ambayo serikali inawachagulia wananchi ili wasome.

Padre wa Kanisa Katoliki aliyekuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Dk. Joseph Matumaini amesema, “Idara ya Habari Maelezo imepitwa na wakati, hivyo ifutwe au kama haitafutwa vyombo vya habari viunde chombo kiingine kitakachotenda haki ili kuiacha idara hii kwa maslahi ya serikali ambayo yameonekana kuwa sio maslahi ya umma.”

-Tanzania Daima
-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad