Mke wa zamani wa Nelson Mandela, Winnie Madikizela-Mandela ameambulia patupu katika wosia wa kinara huyo wa vita dhidi ya ubaguzi wa rangi, imebainika.
Rais huyo wa zamani wa Afrika Kusini amegawanya mali zake zenye thamani ya Pauni za Uingereza milioni 2.5 kati ya wanafamilia yake, wafanyakazi na chama tawala cha African National Congress.
Hatahivyo, ameamua kutompatia chochote Winnie - mke wake wa pili, ambaye alizaa naye watoto wawili, Zenani na Zindziswa.
Wakati huohuo, mke wake wa tatu, Graca Machel, ametajwa kama mrithi mkuu wa wosia huo sababu ndoa yao ilikuwa 'kwenye mali ya jamii', kwa mujibu wa msimamizi wa mirathi, Naibu Jaji Mkuu Dikgang Moseneke.
Hivyo amethibitishwa kupata asilimia 50 ya mali zake, ambayo imethaminishwa kufikia Randi milioni 46 (sawa na Pauni za Uingereza 2.5), bila kuhusisha mirabaha.
Wosia huo wa Mandela wenye kurasa 40 - ulioandikwa mwaka 2004, na kufanyiwa maboresho mwaka 2005 na 2008 - ulisomwa mjini Johannesburg jana asubuhi.
Mgawanyo huo wa mali zake ulitarajiwa kuibua mgogoro mkubwa miongozi mwa watoto zake 30, wajukuu na vitukuu.
Lakini inaaminika kuwa umekubalika na familia yake bila pingamizi lolote mpaka sasa.
Kama mrithi mkuu, Mama Graca lazima adai nusu yake ya utajiri huo ndani ya siku 90, alisema Moseneke, ambaye aliungana na wasimamizi wa mirathi George Bizos, mwanasheria wa haki za binadamu ambaye alikuwa rafiki wa siku nyingi wa Mandela, na Themba Sangoni, jaji mkuu kutoka jimbo la Eastern Cape.
Aliongeza kwamba ingawa Winnie hakuwa ametajwa katika wosia huo, wajukuu zake kila mmoja atapata Dola za Marekani 9,000 (sawa na Pauni za Uingereza 5,500).
Moneseke alisema usomwaji wa wosia huo kwa ndugu wa Mandela 'ulienda vizuri' - lakini aliongeza 'kulihitajika ufafanuzi mara kwa mara'.
Utajiri wa shujaa huyo wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi umegawanywa kati ya taasisi tatu alizoanzisha, ikiwamo moja iliyoundwa kwa ajili ya kuhudumia ndugu wa familia yake, alisema.
Mandela, mfungwa wakati wa utawala dhalimu wa weupe wachache ambaye alikuja kuwa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, alifariki Desemba 5 akiwa na umri wa miaka 95 - na kufuatiwa na kipindi cha siku 10 za maombolezo nchi nzima na kufurika salamu za rambirambi kutoka kote duniani.
Ameacha mali ambazo zinahusisha jumba la thamani kubwa mjini Johannesburg na nyumba ya wastani ya makazi kwenye kijiji chake alikozaliwa katika jimbo la Eastern Cape. 
Pia unahusisha mrabaha kutoka mauzo ya vitabu, vikiwamo 'Mandela's autobiography' na 'Long Walk to Freedom'.
MUHTASARI WA WARITHI WALIOTAJWA KATIKA WOSIA WA MANDELA:
Takribani watu 50 au taasisi zimetajwa kama warithi kwenye wosia wa Nelson Mandela, kwa mujibu wa muhtasari maalumu.
Warithi wakuu ni:
-        Mke Graca Machel, ambaye amekabidhiwa asilimia 50 ya utajiri wake, wenye thamani ya takribani Dola za Marekani milioni 4.1. Anatarajiwa kupata haki hiyo kwa kupokea vitegauchumi vinne nchini Msumbiji, magari, michoro, vito na mali nyinginezo.
-        Watoto wa Mandela kila mmoja atapata takribani Dola za Marekani 300,000, au kama waliwahi kukopa kiasi hicho kutoka kwake wakati wa uhai wake, deni lao litafutwa.
-        Watoto wa Graca, Josina Machel na Malengane Machel, kila mmoja atapata takribani Dola za Marekani 270,000.
-        Wajukuu wanne wa Mandela kwa marehemu mtoto wake wa kiume Makgatho kila mmoja atapata 300,000 na wameruhusiwa kutumia nyumba yake iliyoko Houghton, Johannesburg.
-        Chama cha ANC, kitapata kati ya asilimia 10 na 30 ya mrabaha kutoka kwenye miradi yake mbalimbali. 
-        Makazi ya Mandela katika kijiji alichokulia cha Qunu yatatumiwa na familia ya Mandela, na pia mjane Graca na watoto zake wawili.
-        Wajukuu kutoka katika ndoa yake ya kwanza Evelyn Mase na ndoa ya pili kwa Winnie kila mmoja atapata Dola za Marekani 9,000. Haikuwekwa wazi mara moja kama kuna chochote kimerithishwa kwa Winnie.
-        Wafanyakazi, akiwamo msaidizi wake binafsi wa muda mrefu Zelda la Grange, watapata Dola za Marekani 4,500 kila mmoja.
-    Mashule na vyuo vikuu alivyosoma na kuweka sawa maisha yake ya kisiasa kila kimoja kilitunukiwa Dola za Marekani 9,000.

 
Top