Maaskofu Wamjibu Rais Kikwete.....Watoa Tamko Zito Kuhusu Mahakama ya Kadhi......Wasisitiza Kuwa Wakristo Wote Wapige Kura ya HAPANA Katiba Inayopendekezwa

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA

Siku tano baada ya Rais Jakaya Kikwete kusema kuwa tamko la Jukwaa la Wakristo (TCF) kuwataka waumini wao kupigia kura ya ‘hapana’ Katiba Inayopendekezwa lilikuwa la hasira, viongozi hao wamejitokeza tena na kusisitiza kwamba msimamo wao huo utabaki kama ulivyo.

Katika tamko pamoja walilolitoa jana baada ya kukutana juzi mjini Dodoma, viongozi hao wamemtahadharisha Rais Kikwete kuwa kuendelea kupigia debe Katiba Inayopendekezwa na kuruhusu Mahakama ya Kadhi, kunaweza kulitumbukiza Taifa katika machafuko na hali ikiwa hivyo Serikali ndiyo itakayolaumiwa.

Tamko hilo limesainiwa na viongozi walewale waliosaini lile la awali la Machi 12, mwaka huu ambao ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Askofu Dk Alex Malasusa, Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa na Mwenyekiti wa Kanisa la Pentekoste Tanzania (CPCT), Askofu Daniel Awet.

Tamko  lao  hili  hapa:

Sisi, Maaskofu kutoka TEC, CCT na CPCT tumekutana leo tarehe Machi 30, 2015 hapa Dodoma ili kuomba kwa pamoja juu ya mgawanyiko unaodhihirika wa dini za Kikristo na Kiislamu kutokana na muswada wa Mahakama ya Kadhi.

Maaskofu tuliokutana hapa hatuna hasira na wala hatuongozwi na hasira wala mihemko katika kufikia maamuzi tunayofanya kama ambavyo wengine wanavyotutafsiri.

Tunafikia maamuzi yetu baada ya maombi na sala na tunasukumwa na upendo kwa wananchi ili kujenga taifa lenye umoja, amani, utulivu na maelewano.

Pia tumekuja kufuatilia kwa kina Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali ya 2014 unaopendekeza, pamoja na mambo mengine, marekebisho ya Sheria ya Tamko la Sheria za Kiislamu la mwaka 1964.

Muswada huu unapendekeza kuanzishwa Mahakama ya Kadhi  ambao utawasilishwa Bungeni April 01, 2015 kwa hati ya dharura na hivyo kuufanya umma wa Watanzania kutokujua maudhui yaliyomo katika muswada huo wakati bado hoja zetu za msingi tulizopeleka kwenye Kamati ya Katiba na Sheria ya Bunge na kwa Waziri Mkuu hazijajibiwa.

Tangu tulipokutana Machi 10, 2015 ambako tulitoa tamko letu kuhusiana na Mahakama ya Kadhi na Katiba Inayopendekezwa, tumekuwa tukiendelea kutafakari juu ya yale tuliyokuwa tumesema katika matamko yetu mbalimbali na jinsi amani na utulivu wa nchi yetu vinavyoendelea kumomonyoka siku zinavyokwenda.

Kwanza tumeshangazwa na tabia ya viongozi wa serikali ya kuitisha na kuendesha mikutano wanayodai ni ya viongozi wa dini lakini isiyo rasmi. Machi 03, 2015 Waziri Mkuu aliitisha mkutano kupitia Mchungaji mmoja ambapo hakuna hata kiongozi mmoja wa taasisi au Kanisa aliyeshiriki.

Jambo la kushangaza ni kile kilichotokea Machi 28, 2015 ambapo Mhe. Rais alishiriki kikao cha kikundi ambacho sio rasmi yaani Kamati ya Amani ya Mkoa wa Dar es Salaam.

Tunasema kamati hiyo siyo rasmi kwa sababu haina baraka za viongozi wa ngazi za juu wa kidini wa Mkoa huo na haina mwongozo wa kazi zake.

Mikutano ya jinsi hii kati ya serikali na wale ambao imewaona kuwa ndio viongozi wa dini sio sahihi kwani viongozi wa dini wana taratibu zao za kualikwa au kuwakilishwa katika mikutano na viongozi wa serikali au wa dini au madhehebu mengine.

Tunawashauri wanaohutubia na wanaoshiriki mikutano hii wajue kwamba washiriki hawana uwezo wa kuamua au kukubaliana na jambo lolote kwa niaba ya viongozi wao wa juu na pia viongozi husika wa serikali wasifurahi kwamba ujumbe wao umewafikia viongozi wa dini kwani hao washiriki sio wawakilishi rasmi na hawana uwezo wa kutoa maamuzi au kukubaliana juu ya jambo fulani la kitaifa.

Pili, tumekuwa tukifuatilia kwa karibu juu ya muswada wa Mahakama ya Kadhi na tumebainisha dhahiri kwamba kile tulichokuwa tunasema kitatokea kimeaanza kutokea bayana.

Yale yaliyotokea kwenye semina kuhusu Mahakama ya Kadhi kwa Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Machi 29, 2015 ambao ni wasomi, ni ishara ndogo sana ya kile kitakachotokea maeneo yote ya nchi yetu. SERIKALI KWA NIA MOJA NA KWA SABABU TUSIZOZIJUA INAANZISHA VITA VYA KIDINI KATI YA WATANZANIA WAKRISTO NA WAISLAMU.

Tunashangazwa kuona jinsi serikali inavyonuia jambo hili ovu litakaloleta balaa kwa nchi yetu wakati huu wa kuelekea kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa na baadaye Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Kutokana na mambo hayo makuu mawili hapo juu, sisi Maaskofu wa Jukwaa la Wakristo Tanzania tunatamka kama ifuatavyo :

1.Matamshi ya Mhe. Rais akihutubia aliyowaita viongozi wa dini tarehe Machi 28, 2015 kuwa Mahakama ya Kadhi ni ya Waislamu wenyewe na serikali haitajihusisha wala kugharamia yanakinzana na kile kinachoendelea bungeni na nchini.

Hapa tunajiuliza, endapo maneno ya Rais ni kweli, mbona Bunge linaendelea kujadili kitu ambacho serikali haitajihusisha wala kukigharimia ? Kwa mantiki hiyo, tunamtaka Mhe. Rais aagize muswada huu uondolewe Bungeni na usijadiliwe tena kwa kuwa Utafiti wa Tume ya kurekebisha sheria ulishaonyesha madhara ya uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi.

 Vinginevyo, kuendelea kujadiliwa kwa muswada huu maana yake ni kwamba serikali inajihusisha na itagharimia mahakama hiyo.

2.Serikali ijue kuwa endapo Wabunge wa dini za Kikristo na Kiislamu watapigana na kisha baadaye wananchi nao wakafanya hivyo katika maeneo yao, SERIKALI ITAKUWA NDIYO CHANZO CHA MAPIGANO HAYO.

Kama tulivyotamka hapo juu, kuhusiana na jambo hili tunamtaka Mhe. Rais aiepushe nchi yetu na kuingizwa kwenye mapigano ya kidini ambayo kuyadhibiti itakuwa vigumu sana (tafadhali rejea kinachoendelea huko Nigeria).

Pia tunamwomba Mhe. Rais akumbuke na kutafakari kile kilichotokea na kinachotokea nchi ya Afrika ya Kati kati ya kundi la Seleka (Waislam) na kundi la Anti Balaka (Wakristo).

3.Tunaamini kuwa viongozi wa serikali wanafahamu viongozi rasmi wa dini na madhehebu ya dini. Kwa mantiki hiyo tunawashauri viongozi wa serikali waache kabisa kutumia vikundi visivyo rasmi kualika mikutano wanayodhani kuwa itakubalika na waumini wa dini hizo. Mikutano yote ya jinsi hiyo itakayoitishwa ni batili na maamuzi yake hatuyatambui na hatutayatambua.

4.Bado Maaskofu tunasimamia Tamko letu la Machi 10, 2015 na tunawahimiza Wakristo wajitokeze kwa wingi katika kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la wapiga Kura na zaidi wajitokeze kwenda kupiga kura ya HAPANA wakati wa kura ya maoni kwani Katiba inayopendekezwa ilifikia hapo kwa njia ya ubabe, ilikosa uadilifu na mbaya zaidi ni RUSHWA YA AHADI YA MAHAKAMA YA KADHI ya iliyotolewa na Waziri Mkuu kwa Waislamu wakati wa kupitisha Katiba Inayopendekezwa.

Tunafanya hivyo kwa dhamiri safi kwa sababu ya imani yetu na kwamba sisi ni raia wa nchi hii na tuna haki ya kueleza mawazo yetu bila woga kama Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 inavyotupa haki.

5.Mwisho tunawaomba Wakristo wote waendelee kufunga na kuomba kwa ajili ya utulivu na amani ya nchi yetu.
-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Post a Comment

8 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Tutaendelea kuomba ili nchi iwe na AMANI. Na tutapiga kura za hapana,, Na tunamuomba Kikwete awe na msimamo sahihi na sio ANAROPOKA HOVYO KAMA VILE SIO KIONGOZI.

    ReplyDelete
  2. Huyo jamaa ni kiherehere sana

    ReplyDelete
  3. Tunapigaje kura ya hapana jamani..na mimi nimo ila sijui jinsi yakupiga...Tanzania hatugawanyiki sisi sote ni ndugu hakuna bora ya mwingine wote sawa

    ReplyDelete
  4. Hili taifa letu litapoteza amani tusipo jiangalia mwanzo tumeishi vizuri ila sasa wanasiasa wanaivuruga nchi bila kuangalia mazara yatakayo tokea

    ReplyDelete
  5. Hamkujifunza kwa nchi jirani zilizokwisha onja vita vya wenyewe kwa wenyewe?Mtoto akililia wembe mpe walisema waswahili

    ReplyDelete
  6. HII SERIKALI INAJARIBU KUWARIDHISHA WAISLAMU WALIOWADANGANYA MIAKA YA NYUMA ILI WAPATE KURA ZAO 2015 NA BAADAE WAWABWAGE CHINI... SIASA ZA TANZANIA SIO MZURI MIAKA YA HIVI KARIBUNI

    ReplyDelete
  7. Ee Mungu simama mwenyewe ujitetee, wakristo siku zote ni wapenda amani ndo maana wanatoa tahadhari, waislamu walituchomea makanisa, wakaua wachungaji na mapandre lakini bado wakristo walikaa kimya wakimsihi Mungu atupiganie, vita vyetu sio vya damu na nyama, wakristo tudumu katika maombi.

    ReplyDelete
  8. Msishabikie shari ipigeni vita kwa nguvu zote tumo kwenye jahazi moja vipi tunagombea mbao.

    ReplyDelete

Top Post Ad