Maaskofu Wamjibu Dr. Slaa Baada ya Kuwatuhumu Kuhongwa na Lowassa......Gwajima Naye Ampa Makavu, Asema Slaa Ametumwa na CCM

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA

Gwajima
Baadhi ya viongozi wa dini na wananchi wamesema shutuma za aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa kuwa baadhi yao walihongwa na Mgombea Urais wa Ukawa kupitia Chadema, Edward Lowassa, ni upuuzi mtupu.

Wamemtaka atoe ushahidi wa madai hayo kwa kutaja majina ya viongozi na kiasi walichohongwa, wakisisitiza kuwa hizo ni siasa za majitaka na kwamba anaifanyia kazi CCM ili apate njia ya kurudi katika chama hicho.

Rais wa TEC azungumza
Akizungumzia shutuma hizo, Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Severin Niwemugizi, amemtaka Dk. Slaa kutoa ushahidi wa madai yake kuwa maaskofu wa kanisa hilo wamehongwa na Edward Lowassa.

“Hizo taarifa ndiyo nazisikia kwako, lakini kama kweli amesema hivyo kwa nini hakuweka ushahidi kuanzia majina ya maaskofu hao waliopewa fedha, kiasi na zilikopokelewa. Lakini kwa upande wangu binafsi sijapokea kiasi chochote kutoka kwa mtu yeyote."  Amsema  askofu  huyo

Askofu Niwemugizi alimtaka Dk. Slaa kutoa uthibitisho wa maaskofu wa kanisa hilo kupokea fedha kutoka kwa Lowassa waweze kutoa uamuzi.

“Lowassa nimewahi kukutana naye nilimwalika kwenye shule yangu ya seminari kule Biharamulo… shule yenyewe inaitwa Katoke na nilimuweka wazi sababu za kumwalika na sikupokea kiasi chochote cha fedha kutoka kwake,”alisema askofu huyo na kuongeza:

“Athibitishe hilo aonyeshe kiasi cha fedha na majina ya maaskofu, mimi sijapata kiasi chochote labda kama nimetupiwa kwenye akaunti yangu bila mimi kujua lakini nasisitiza atoe ushahidi.”

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu kwa Jamii ya Madhehebu ya Dini nchini, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kipentekosti, William Mwamalanga alisema kauli za Dk. Slaa zina dalili ya kuleta kisasi fulani.

“Angekuja mapema kabla ya taratibu hizi kuanza tungemwelewa lakini kwa sasa yupo nyuma ya wakati. Kwanza ameonekana amesukumwa afanye aliyofanya na hilo haliwezi kuwabadilisha Watanzania walioamua kutaka mabadiliko,”alisema na kuongeza:

“Hotuba yake haina mashiko na taifa halihitaji watu wabinafsi,”alisema Mchungaji Mwamalanga.

Askofu Gwajima azungumza
Naye Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amekana kuwa mshenga wa Edward Lowassa kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendelea (Chadema) .

Pia amekana kuhusika kuwarubuni kwa fedha maaskofu 30 wa Kanisa Katoliki ambao wanadaiwa kumuunga mkono Lowassa katika mbio zake za urais baada ya kuhongwa fedha.

 Askofu Gwajima amesema Dk. Slaa ndiyo risasi ya mwisho iliyokuwa imebakia ndani kati ya bunduki ya CCM ili kuwaokoa.

Amesema yote yaliyosemwa na Dk. Slaa ni tuhuma za uongo hivyo wananchi wazipuuze kwa kuwa mwanasiasa huyo anatafuta uungwaji mkono kwa wananchi aelekee CCM.

“Yaani ni uongo kabisa tena uongo mweupe, imedhihirisha wazi kuwa huyu mtu asingefaa kuwa rais. Ni dhahiri ameona akiwasema wanasiasa wenzake watamjibu kwenye majukwaa yao ya siasa, lakini sasa amewasema maaskofu kwa kuwa wao hawana majukwaa.

“Kwa hiyo namshauri hayo mambo ya kuwahusisha maaskofu na uchaguzi aache uongo wa namna hiyo. Nafikiri awaseme wanasiasa wenzake kuzungumzia mambo ya siasa ila kuwahusisha maaskofu si mambo ya busara,” alisema.

Akizungumzia suala la kuwa mshenga wa Lowassa na Chadema, Askofu huyo amesema anafikiri Dk. Slaa ametumwa na waliomtuma, hivyo anawafanyia kazi watu.

“Kwa kawaida inashangaza kwamba kama watu wawili wanagombana, inatakiwa awepo mtu wa kuwaunganisha, ila anaposema maaskofu 34 haileti maana, haiingii akilini… ameingiza Gwajima, Rostam (Aziz) na maaskofu, haeleweki anachozungumza. Lakini ninachosema kuna waliomtuma ni watu ambao anawafanyia kazi.

“Kikubwa ni kwamba baada ya Lowasaa kuchaguliwa kugombea urais kwa Chadema alichukia, alifikiri Lowassa hataendelea kuwa na umaarufu, sasa anaona Lowassa anakwenda, hiyo imemtia hasira anataka kumchafulia Lowassa, ndiyo maana anaongelea Lowassa Lowassa tu.

“Kwa mfano alisema Lowasa angekuja na wabunge wenyeviti wa CCM, ina maana angemkubali Lowassa aje nao, sasa angekuja nao asingekuwa fisadi? Ni swali zuri ila amekwepa kulijibu.

“Nafikiri Dk. Slaa ndiyo risasi ya mwisho iliyobakia ndani ya bunduki ya CCM. Natoa wito kwa waumini wangu wafahamu kuwa hizi tuhuma ni za uongo na namsihi huyo daktari asihusishe maaskofu na uongo wake abaki nao mwenyewe,” alisema Askofu Gwajima.
-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Top Post Ad