Vijana 100 Arusha Wanaomuunga Mkono Dr. Slaa Wahama UKAWA na Kujiunga ACT-Wazalendo

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA

WANACHAMA zaidi ya 100 wa Chadema, NCCR-Mageuzi na CUF wameandamana mjini Arusha na kuchoma moto bendera na kadi za vyama hivyo, wakimuunga mkono aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa.

Watu hao waliandamana jana na maandamano hayo yamefanyika siku mbili baada ya Dk Slaa kutangaza hadharani, Dar es Salaam kuwa ameachana na siasa.

Wakiwa katika maandamano yaliyoambatana na kubeba mabango yenye ujumbe mbalimbali, wanachama hao wengi wao wakiwa vijana, walijiunga na Chama cha ACTWazalendo, wakidai kuwa hawawezi kuviunga mkono vyama vyao vya zamani kwa kuwa vimenunuliwa na mafisadi.

Huku wakiimba nyimbo za kuvishutumu vyama vyao vya zamani (Chadema, NCCR-Mageuzi na CUF), vijana hao walidai kuwa hawako tayari kuendelea kuviunga mkono vyama hivyo kwa sababu vimeonesha wazi kuwa havina ajenda ya kuwasaidia Watanzania masikini, bali vinawakumbatia matajiri na hivyo kupoteza mwelekeo wa kisiasa.

Mmoja wa viongozi wa maandamano hayo, Hassan Juma aliyedai kuwa mwanachama wa Chadema tangu mwaka 2005, alisema chama hicho kimenunuliwa na mafisadi na kuwa hakiwezi tena kuwasemea wanyonge ambao ndio wamekuwa tegemeo lao na hivyo hawana sababu tena ya kukiunga mkno katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

“Mimi nilikuwa naamini katika sera za Chadema za kupambana na ufisadi tangu nilipojiunga nacho mwaka 2005, lakini sasa imedhihirika walikuwa wanatutumia vijana kwa ajili ya malengo yao binafsi na kwa hiari yangu nimeamua kuachana nacho na nataka kuwa mwanachama wa ACT-Wazalendo ambao ni tegemeo la wanyonge hivi sasa nchini,” alisema Juma akiungwa mkono na wenzake wakiwa katika ofisi za ACTWazalendo Arusha.

Mwanachama wa NCCR-Mageuzi aliyejitambulisha kwa jina la Eliphas, alisema viongozi wakuu wa vyama hivyo wamekuwa na tabia ya kuwaburuza kwa kufanya maamuzi ya kuwanufaisha wao wenyewe na hilo limewachefua na wameamua kuachana na chama hicho ili kujiunga na chama chenye mwelekeo unaofanana na watu wa chini.

“Kwa hali ilivyo hivi sasa ndani ya Ukawa ni afadhali hata kule CCM ambako tulikimbia zamani kwa kuwa hakuna demokrasia kabisa, viongozi wananunuliwa ovyo, hatuna ajenda ya kuisimamia sasa ni bora tuachane na walanguzi hao wa kisiasa na tuungane na vyama ambavyo tunaona wazi kwamba vitatetea maslahi yetu.
 
“Hatuwezi tukalaani ufisadi ukiwa ndani ya CCM halafu ukija kwetu tunaukumbatia na kuuhalalisha. Tuliondoka CCM kwa sababu ya ufisadi na mizengwe na sasa tunaona kwamba viongozi wetu wameyakaribisha na kuyakumbatia bila aibu yoyote mambo hayo na kamwe hatukubaliani na hilo na ndio maana tunaondoka na wenzetu wengine wengi wapo njiani kutufuata,” alisisitiza Eliphas huku akichoma moto kadi yake ya NCCR-Mageuzi.

Miongozi mwa maneno yaliyoandikwa katika mabango waliyobeba wanachama hao ni pamoja na ‘Mbowe ameuza chama chetu kwa fisadi Papa,’ ‘Lowassa angekuwa mwanao amelawitiwa ungemwachia Babu Seya?’ na Bye bye Chadema, bakini kwa mafisadi wenu.’

Hata hivyo, Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa alisema vijana hao ni mamluki waliopangwa na CCM na kwamba wana taarifa za mikakati ya kuwanunua vijana ili waandamane wakionesha kuwa wanaipinga Chadema wakati ni mamluki tu wa kisiasa ambao hawana chochote zaidi ya kuganga njaa.

-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad