Kilichomuua Mbunge Filikunjombe Sasa Hadharani

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA

Uchunguzi wa awali kuhusu ajali ya chopa iliyogharimu maisha ya aliyekuwa mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe na wenzake watatu, unaonyesha ilitokana na hitilafu ya injini, Mwananchi imebaini.

Katika ajali hiyo iliyotokea Oktoba 16 kwenye pori la Selous, mbali ya Filikunjombe, rubani wa chopa hiyo, Kapteni William Silaa na wengine wawili waliokuwamo ndani ya chombo hicho kilichokuwa na namba za usajili 5Y-DKK na namba za utengenezwaji 7027 Eucereuil, pia walifariki dunia.

Filikunjombe alikodi chopa hiyo kutoka kampuni ya ndege ya Sun Drew inayomilikiwa na aliyekuwa Makamu wa Rais wa Kenya, Kalonzo Musyoka na ilikuwa inafanyiwa ukarabati na kampuni ya Laid Loris.

Baada ya ajali hiyo Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kwa ushirikiano na Wizara ya Uchukuzi waliita timu ya wachunguzi wa ndege kutoka Ufaransa ambayo ilitua nchini Oktoba 20. Timu hiyo ya watu wanne ilijumuisha mtu mmoja kutoka kampuni ya Airbus Industries ya Marseilles ambao ni watengenezaji wa chopa hiyo; mtu mmoja kutoka kampuni ya Turbo Meca, waliotengeneza injini; na watu wawili kutoka BEA, kitengo cha uchunguzi wa ndege kutoka Serikali ya Ufaransa.

Timu hiyo ilibaini hitilafu hiyo, ikibainisha kuwa baada ya injini kufeli, chopa hiyo ilianza kushuka hadi ikaanguka na kulipuka. Sababu za kulipuka kwake zimetajwa na wachunguzi hao kuwa ni madumu matano ya mafuta ya ujazo wa lita 20 yaliyokuwa ndani ya chopa hiyo.

Mchunguzi Mkuu wa Ajali za Ndege wa Wizara ya Uchukuzi, Omar Mhina aliiambia Mwananchi kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni kufeli kwa injini.

“Katika uchunguzi wa awali, tulichukua injini na kugundua kuwa ilipata hitilafu. Hiyo ndiyo lugha ya kwanza tunayoweza kusema wakati tukisubiri uchunguzi mwingine,” alisema Mhina katika mahojiano na Mwananchi.

Mhina alisema wameshaichukua injini kutoka pori hilo la Selous na kwamba wanatarajia kuipeleka kwa watengenezaji wake kwa ajili ya kufunguliwa na kujua kiini cha kufeli kwa injini hiyo.

Alisema waliwasiliana na wamiliki wa chopa hiyo nchini Kenya, lakini hawajapata ushirikiano wa kuridhisha mpaka sasa. Lakini Mwananchi ilizungumza na opereta mkuu wa chopa hiyo wa Kenya, na rubani wa kampuni ya Sun Drew, Kapteni Charles Wachira ambaye alisema TCAA hawajawasiliana na Mamlaka ya Anga ya Kenya (KCAA) kwa ajili ya uchunguzi wa ajali hiyo.

Mimi ni kapteni wa ndege lakini siwezi kufanya lolote kama sijapata baraka kutoka TCAA na KCAA. Wao ndio walitakiwa wawasiliane kwanza kabla ya sisi Sun Drew kuchukua hatua zozote, ni suala baina ya serikali na serikali,” alisema Wachira.

Kapteni huyo amesema akipata ruhusa kutoka KCAA atakuja nchini kwa ajili ya uchunguzi wa chanzo cha ajali ya chopa hiyo.

Kauli ya Musyoka

Lakini Kalonzo alisema kampuni yake imeshampa baraka zote, Kapteni Wachira ili kushirikiana na Tanzania kubaini chanzo cha ajali hiyo na kwamba kilichochelewesha ujio huo ni kusubiri kumalizika kwa shughuli za uchaguzi zilizokuwa zikifanyika Tanzania.

Kalonzo alisema walituma mwakilishi ambaye ni mjumbe wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Peter Mathuki kupeleka salamu za rambirambi na kuhudhuria msiba wa Kapteni Silaa.

Ni lazima tushiriki katika hili kwa sababu ni pigo kubwa kwetu na kwa serikali yenu. Tayari Kapteni Wachira amekuja huko ili kushirikiana na Mamlaka ya Anga ya Tanzania,” alisema Kalonzo.

Mafuta yalilipua

Chanzo kingine cha ajali hiyo kilichoelezwa na timu hiyo ni madumu matano ya mafuta ya ndege yaliyokuwa yamepakiwa ndani.

Walikuwa wamebeba hayo madumu yenye mafuta ya akiba kwa kuwa walikuwa wametokea Ludewa ambako hakuna mafuta; unajua chopa hazikai na mafuta kwa muda mrefu ndiyo maana walibeba mafuta ya akiba,” alisema mtoaji habari wetu.

Kadhalika chanzo hicho kimesema viti vya ndege vilionekana kuanguka na kuvunjika na watu waliokuwamo walivunjika uti wa mgongo na miguu. Hata kama wasingeungua, wangepoteza maisha kutokana na madhara ya kuanguka kwake.

Ripoti ya BEA

Ripoti ya awali ya Kitengo cha uchunguzi wa ajali za ndege cha Serikali ya Ufaransa (BEA) iliyochapishwa kwenye tovuti yake imeeleza kuwa chopa hiyo ilionekana ikianguka kutoka angani, ikiwa tayari haina nguvu na ikifuka moshi. Kadhalika chopa hiyo ilionekana kwa muda mrefu ikiruka umbali wa chini na baada ya kuanguka, ililipuka.

Turbomeca

Lakini mkuu wa kitengo cha wanafizikia wa kampuni ya Turbomeca iliyotengeneza injini ya ndege hiyo, Delpgine Robelin alikataa kutoa maelezo akisema kuwa ni ya siri. “Hii ni siri kubwa. Hakuna taarifa zozote zinazoweza kutolewa,” inasema barua pepe ya Robelin akijibu barua pepe ya Mwananchi iliyoomba kupata ripoti ya awali ya uchunguzi wa ajali hiyo.

Mawasiliano angani

Uchunguzi umebaini pia Kapteni Silaa hakuwasiliana na kitengo cha usalama wa anga na mawasiliano ya ndege cha TCAA

Kuhusu tatizo la chopa. Mhina amesema Kapteni Silaa aliwasiliana na kitengo hicho wakati ndege ipo ardhini, ikipaa na ilipofika juu, lakini baada ya hapo hakukuwa na mawasiliano yoyote.

Kabla hajaruhusiwa kwenda eneo jingine la anga (area control route) ndipo alipokata mawasiliano na hakuwasiliana hata na ndege nyingine kueleza kama ana tatizo,” alisema.

“Kwa kawaida chopa zinatakiwa kuwasiliana zikiwa angani, lakini hakuna chopa yoyote iliyotoa taarifa kama waliwasiliana na Kapteni Silaa,” alisema Mhina na kuongeza: “Iwapo chopa ina matatizo ya injini, kuna namna ambayo marubaini wanaweza kudhibiti ili kusitokee madhara, lakini haijulikani kwa nini Kapteni Silaa alishindwa kudhibiti hali hiyo.”

Shahidi

Mhina alisema kwamba mmoja wa mashuhuda aliiambia timu ya wachunguzi kwamba alianza kuona chopa hiyo ikifuka moshi wakati iko hewani. “Lakini haikuwa ikiungua, hapana, ilifuka moshi hadi ilipoanguka ndipo ikawaka.”    

-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad