Vikwazo Vitano Vyatajwa Kwenye Agizo la Rais Magufuli Kufuta Safari za Nje

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA

Agizo la Rais John Magufuli la kusitisha safari za nje linakabiliwa na ugumu katika utekelezaji wake kutokana na nchi kuwa na balozi 36 tu ambazo zitatakiwa kufanya kazi maeneo mbalimbali duniani.
Muda mfupi baada ya kuapishwa na kuanza utekelezaji wa majukumu yake ya mkuu wa nchi, Rais alifuta safari zote za nje kwa watumishi wa Serikali na viongozi ili kuokoa fedha zinazotumika kwa ajili hiyo na kuagiza shughuli hizo zifanywe na mabalozi.

Rais alisema safari hizo zitadhibitiwa na Ikulu ambayo itatoa kibali kwa safari maalumu, ikiwa ni pamoja na kuweka masharti ambayo mtumishi anayetakiwa kusafiri atatakiwa kuyatimiza kabla ya kupewa kibali.

Lakini utekelezaji wa agizo hilo unakabiliwa na vikwazo vingi, hasa vikubwa vitano ambavyo ni uchache wa balozi za Tanzania nje ya nchi, ukomo wa madaraka ya mabalozi, wigo wa ufahamu wa mambo ya kitaalamu na ukosekana kwa mazungumzo endelevu iwapo suala moja litawakilishwa na watu wawili tofauti kwenye mikutano miwili tofauti.

Takwimu za Umoja wa Mataifa (UN), zinaonyesha kuwa hadi sasa chombo hicho kina wanachama 193 ambao nchi zinazaweza kuwa na uhusiano nazo wa kidiplomasia, kwa mujibu wa makubaliano ya wanachama wa umoja huo. Kwa mujibu wa wakosoaji, uchache huo utasababisha mabalozi hao kusafiri sehemu mbalimbali duniani kushiriki kwenye shughuli ambazo viongozi wa umma walitakiwa kwenda, hali ambayo itasababisha safari kuwapo kama kawaida isipokuwa wanaosafiri ndiyo watakaobadilika.

“Ni kweli kwamba idadi ya watu wanaosafiri itapungua, lakini ile dhana ya safari itabakia vilevile,” alisema mmoja wa wakosoaji ambaye hakutaka jina lake litajwe.
“Kwa mfano, mkutano wa Jumuiya ya Madola unaofanyika Malta, Balozi wa Tanzania nchini Uingereza ndiye atatakiwa kwenda. Kwa hiyo ni safari pia.”
Bara zima la Amerika Kusini lina ofisi moja tu ya ubalozi iliyoko Brasilia, Brazil, wakati bara la Amerika Kaskazini lina balozi tatu, mbili zikiwa Marekani--Umoja wa Mataifa jijini New York na Washington--, huku Ulaya yenye nchi 50 ikiwa na balozi nane, wakati Asia, Arabuni pamoja na Australia kuna ofisi nane za ubalozi.

Bara la Afrika lenye nchi 52, ndiko kuna balozi nyingi zaidi, kukiwa na ofisi 14.
Ugumu katika utekelezaji unaosababishwa na idadi ndogo ya mabalozi pia ulidokezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula mapema mwezi huu.
Akizungumzia suala hilo, Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue ambaye alikuwa akijibu maswali kuhusu vikwazo vitano vya utekelezaji wa agizo hilo la Rais, alisema suala hilo linaweza kujibiwa vizuri zaidi na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Lakini msemaji wa wizara hiyo, Mindi Kasiga alisema atumiwe ujumbe wa barua pepe ili ajibu suala hilo.

Ukomo wa madaraka ya mabalozi
Suala jingine linalozungumziwa ni ukomo wa mabalozi katika mamlaka yao, hasa pale wanapotakiwa kumuwakilishi Rais wakati hawabebi madaraka hayo ya mkuu wa nchi. Mara nyingi wakuu wa nchi huona umuhimu zaidi wa kuwa na mazungumzo baina yao kuliko na mabalozi inapotokea wamekutana kwenye mikutano ya mikubwa kama ya Jumuiya ya Madola, Umoja wa Mataifa, Sadc na mingine inayoweka maazimio muhimu kuhusu masuala kama ya mazingira, afya, na ya kibiashara.
Lakini Balozi Sefue alisema Rais atakuwa akihudhuria mikutano michache na hivyo uamuzi huo hautaathiri nchi. “Ni mikutano michache sana ambayo wanahudhuria wakuu wa nchi,” alisema Balozi Sefue. “Pale ambapo tutajiridhisha kuwa ubalozi hauwezi kutuwakilisha vizuri, basi tutaruhusu mtu atoke hapa nyumbani. Hiyo itakuwa ni baada ya kujua ni nani atakayekwenda na atakwenda kufanya nini,” alisema Balozi Sefue.

Kwa uzoefu wake, alisema hata viongozi watakaopewa ruhusa hawatakuwa na misafara mirefu kama ilivyokuwa awali kwa kuwa wapo baadhi yao ambao wanakuwa hawafanyi chochote huko waendako.
“Nilipokuwa Washington niliwahi kushuhudia. Kuna msafara ulikuja, mkubwa sana na kwa kipindi chote walichokaa pale, wapo baadhi hawakupata nafasi ya kufanya chochote. Hili nalo ni miongoni mwa mambo yatakayozingatiwa katika vibali vitakavyokuwa vinatolewa kwa wale watakaokidhi masharti,” alisisitiza.

Kuhusu ukubwa wa ujumbe ambao kiongozi anaruhusiwa kuambatana nao aendapo nje ya nchi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Mindi Kasiga amewahi kufafanua kuwa, kwa mujibu wa itifaki, kila mmoja ana maelekezo yake.
“Msafara wa Rais hauwezi kulingana na wa makamu wake, Waziri Mkuu au waziri wa kawaida ambao pia hutofautiana na makatibu wakuu au wakuu wengine wa idara na vitengo vya Serikali,” alisema Kasiga wakati akitoa ufafanuzi juu ya gharama za safari za nje wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne.


Uwakilishi wa mamlaka ya Rais
Mbali na vikwazo hivyo, suala jingine ni mabalozi kubeba majukumu ya Rais kwenye mikutano ya nje jambo ambalo wakosoaji wanasema litawawia vigumu hasa watakapotakiwa kufanya uamuzi kwa madaraka ya mkuu wa nchi.
Lakini Balozi Sefue alisema mabalozi watakaotumwa kwenye mikutano hiyo watabeba kofia hiyo ya mkuu wa nchi na taarifa itakayotumwa nchini itakuwa na uzito unaostahili hivyo suala hilo halitaathiri ushiriki wa nchi.

Mabalozi kutokuwa na utaalamu
Uwezo wa mabalozi kushiriki kikamilifu kwenye masuala ya kitaalamu pia ni moja ya mambo yanayoonekana kuwa kikwazo kwa agizo la Rais Magufuli kuzuia safari za nje.
Lakini Balozi Sefue alisema matukio yanayohusu masuala ya kitaalamu kama kilimo, mazingira, afya, madini na mawasiliano ambayo yanahitaji watendaji waliobobea kwenye fani hizo, yatawekewa utaratibu licha ya kuwa changamoto kwa mabalozi.
“Kila ubalozi una wataalamu wa masuala mbalimbali ambao wanaweza kutoa mchango unaostahili kwa lolote linaloweza kuhitajika,” alisema.
“Si rahisi kukosa mtu mwenye uwezo wa kumsaidia balozi kutekeleza majukumu yake kiasi cha kuhitaji mtu mwingine kutoka nyumbani. Lakini likijitokeza hilo, tutatuma mwakilishi.”
Akizungumzia suala hilo, Balozi Mulamula alisema mapema mwezi huu kuwa utekelezaji huo utachukua muda kidogo kutokana na balozi nyingi kukosa fedha na watalaamu.
Suala la fedha kwenye balozi za Tanzania limekuwa kilio kikubwa kila wakati wa Bunge la Bajeti na mwaka huu suala hilo liliibuka kwenye hotuba ya kambi ya upinzani iliyosema kiasi cha Sh30 bilioni ziloizotengwa kwa wizara hiyo hazikutosha kuwawezesha mabalozi kufanya kazi yao kwa ufanisi.
Suala la weledi pia lilizungumzwa kwenye hotuba ya kambi ya upinzani ya mwaka 2014/15 ikisema uteuzi holela wa mabalozi usiozingatia sifa, unalikosesha Taifa fursa nyingi za kiuchumi kwa kuwa wengi hawana ufahamu wa fursa zilizoko kwenye nchi wanazokwenda.
Lakini mapema mwezi huu, Balozi Mulamula alisema suala hilo sasa litaangaliwa kwa jicho la karibu zaidi, hasa uteuzi wa mabalozi.

Alisema watatoa mwongozo ambao utawataka wawakilishi hao wasibweteke katika utendaji wao kwa kuwa kuna mpango wa kuanzisha utaratibu wa kupima matokeo ya utendaji wao kwa kila baada ya kipindi kitakachoelekezwa.
“Kwa sasa tutakuwa tunawapima mabalozi wetu kwa malengo tuliyokubaliana nao ambayo yanaweza kuwa ya mwaka au zaidi.
Tutakuwa tunamuuliza balozi umeweza kuleta watalii au kuwahamasisha wawekezaji wangapi nchini?” alisema.

“Hii ni kwa sababu zamani tulikuwa tunakwenda kienyeji lakini kwa sasa hapa kazi tu.”
Kikwazo kingine kinachoonekana kwenye utekelezaji wa agizo hilo ni kukosekana kwa mazungumzo endelevu iwapo suala moja litawakilishwa na watu wawili tofauti kwenye mikutano miwili tofauti.
“Mfano iwapo kutakuwa na mkutano wa suala fulani la Jumuiya ya Afrika Mashariki nchini Kenya, kwa agizo hilo la Rais, atakayewakilisha ni balozi wa Tanzania nchini Kenya,” alisema mkosoaji huyo na kuongeza:
“Iwapo suala hilo litaendelezwa kwenye mkutano mwingine wa jumuiya nchini Uganda, ni dhahiri atawakilisha balozi wa Tanzania nchini humo ambaye hakuwapo kwenye mkutano wa Kenya. Kwa hiyo kutakuwa na upungufu.”

Balozi Sefue hakutaka kufafanua kuhusu hoja hiyo na badala yake akaielekeza kwa Wizara ya Mambo ya Nje, ambayo alisema ina nafasi nzuri zaidi ya kulizungumzia.
-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Post a Comment

10 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Changamoto haziwezi kukosekana katika kila jambo, natumai kila kitu kitakaa sawa tu. Mungu bariki viongozi wetu, Mungu bariki Tanzania

    ReplyDelete
  2. vyovyote vile lakini Mh kafanya la maana sana kufutilia mbali safari holela za hawa viongozi walizokuwa wakizifanya bila tija, safi sana Magufuli, pamoja hukupata kura yangu, umefanya la maana sana Mh.

    ReplyDelete
  3. Tatizo hawa wanahabari nao wapotoshaji. Gharama kusafiri nje ya nchi ni cheap kuliko huku kwetu.

    Go Jembe go. Ngos

    ReplyDelete
  4. Mimi nilijua,tena mapema kuwa Wizara hii ya Mambo ya nchi za nje kupitia kwa Viongozi wake wooote ukianzia kwa Katibu mkuu Wataanza kuleta chokochoko na kumchimba Mheshimiwa Rais Magufuli kwani ufujaji wao,wizi,uhujumu uchumi sasa vimo kwenye powerful radar.wizara hii imebobea kwa ufujaji.nikupe moja.Wapo mabalozi na maafisa ubalozi zaidi ya 30 ambao tayari umri wao wa kustaafu kazi ulishafika na kupita wanaendelea kukaa huko na serikali inatumia zaidi ya million 500 kuwalipa mishahara ya zawadi, kwani walikwishastaafu! Pili nizungumzie CV za mabalozi wenyewe.balaa,balaa,balaa.sifafanui,utalia.Ombi Muheshimiwa Magufuli woote 36 TUNAKUOMBA Uwarudishe nchini na wewe mwenyewe ufanye uteuzi mpya kabisa.wengine wao hata kiswahili kinawapa shida kuongea.Tatu malalamiko ya uwakilishi finyu. huu ni upuuzi.mnafanya nini cha maana huko zaidi ya kuharibu uchumi wa nchi.kwa kuanzia kwa maoni yangu mabalozi 20 tuu wanatosha kuanza nao kazi.na badala yake Ofisi za Biashara chini ya wizara ya Biashara na viwanda zichukue nafasi yake iliyokua wanastahili kwa miongo kadhaa sasa.tunahitaji kukuza biashara,tunahitaji kuimarisha uchumi,tunahitaji kuuza nje zaidi tena zaidi kupindukia hatuhitaji longo longo ya kuiibia nchi na kujinufaisha,tumegutuka. kwa chokochoko hizi nafikiri upo mkono wa aliyekua kiongozi fulani.Sasa Mheshimiwa Magufuli,Usimcheleweshe MNAFIKI huyu mlete hadharan TUMSASAMBUE.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Usisahau kuna maofisa ubalozi wako nje zaidi ya miaka kumi na hawana dalili yakurudi wanaume enjoy na familia zao .wakati wengine wanasubiri tu bongo

      Delete
    2. Usisahau kuna maofisa ubalozi wako nje zaidi ya miaka kumi na hawana dalili yakurudi wanaume enjoy na familia zao .wakati wengine wanasubiri tu bongo

      Delete
  5. Seif anataka kuendeleza kilichojificha. Wizi wa mali za umma kupitia safari, na mikataba binafsi. Rudia mikataba yote mikuu. Kundi lililokuwa likisafiri na Kikwete kiangaliwe upya. Tafuta mwenye uwezo , wa kuongea, kunegotiate, na kuwewka Tanzania mbele. Fumua mikataba binafsi inayowahusisha viongozi wa awamu iliyopita. Wengi wamejiingiza kwenye biashara binafi ambazo ni mali ya Watanzamia. Ziba nyufa zote.

    ReplyDelete
  6. NDIYO, NAUNGA MKONO,TUIMARISHE TENA KWA KASI NA MAKUSUDI UWAKILISHI WA NCHI KIBIASHARA NA KIUCHUMI.HII NI OPERATION FUFUA UCHUMI.MIRIJA MIBAYA YA WIZI NA UHUJUMU SERIKALINI SASA INADHIBITIWA.MBONA BADO, NASA NASA IKIANZA WATANASWA WEZI WENGI.

    ReplyDelete
  7. Kuna waandishi wa habari wananufaika na hizi safari, maana kuna baadhi ya vigogo wana'wabeba na kutembea nao nchi mbalimbali, kwa hiyo sioni ajabu kutafuta 'vikwazo' vya kitoto kututangazia eti agizo la JPJM halitekelezeki!!! HATUDANGANYIKI........MTANYOOKA, HAPA KAZI TU!!!

    ReplyDelete

Top Post Ad