20 Mar 2017

Rais Wangu Magufuli: Makonda Ulimtengeneza Alengwe - Wape Ushindi Wao...


Na. M. M. Mwanakijiji 

Ninalirudia hili mara nyingi siku hizi za hivi karibuni - tunatumia muda mwingi kujadili mambo ambayo yalitakiwa yawe ya kujadilika siku moja yakaisha. Inasikitisha, inaudhi, inakera na inakatisha tamaa kuona karibu taifa zima tunazungumzia suala ambalo kama kungekuwa na hekima, busara na weledi lingeisha mapema sana na wala lisingezaa mambo mengine. 

Suala la cheti cha Makonda au kubadili jina lake wala halikuwa jambo ambalo halitatuliki kwa haraka. Naamini lingeweza kuzungumzwa, kutolewa uamuzi na watu wangesonga mbele; hata kama ni kuendelea na Makonda watu wangeendelea kama ingetolewa kauli ya kwanini watu wanaendelea. Ambao wangetaka kuendeleza ligi wangeendeleza tu. 

Bahati mbaya sasa limefika mahali kwamba linahoji siyo tu hekima, bali uthubutu, busara, umakini, heshima na tunu nyingine mbalimbali za Rais na viongozi wenzake wa juu. 

Niseme tu kuwa, Makonda angeweza kuendelea kuwa mkuu wa Wilaya au hata na utumishi ndani ya chama akiendelea kujengwa na hata kushughulikia mambo mengine. Niliandika wakati anateuliwa ukuu wa wilaya kuwa ilikuwa ni jambo la ajabu kidogo. Na sikutaka kuendelea kuandika muda wote baada ya hapo. Sababu kubwa ni kwamba, ni kiongozi kijana ambaye anahitaji muda wa kujifunza na kufunzwa. Sijui kama ameshajifunza lakini nina uhakika matukio ya hivi karibuni yatakuwa yamemfunza mambo mengi tu. 

Hata hivyo, Makonda amejikuta kwenye hali ngumu ya mengi si kwa sababu ya yeye mwenyewe tu bali kwa sababu ya Rais wangu Magufuli mwenyewe. Alimteua kuwa Mkuu wa Mkoa na kumbakisha Dar-es-Salaam kama namna ya kuwakata ngebe watu waliokuwa wanamsemasema sana akiwa Mkuu wa wilaya. Alimpa Dar kama alama ya "wakome" waliokuwa wanamsema. Ni yeye alimfanya Makonda awe mlengwa wa kisiasa (political target). Katika siasa kama vile ilivyo katika mapenzi na vita - yote yanaruhusiwa (all is fair in politics just as they are fair in love and war). Kama alitaka kumtumia Makonda kama mjeledi wake wa kisiasa katika Jiji la Dar basi alipaswa kujua kuwa na wenzake wanaweza kumtumia huyo huyo Makonda kumfanya awe mjeledi wao. 

Lakini pia pamoja na hayo kitabia, na weledi wa kiuongozi Makonda mwenyewe pia amejitengeneza kuwa mlengwa. Tangu sakata lake lianze na mashambulizi yaanze dhidi yake ni wachache wameonesha kujali kumuonea huruma. Hii imenishangaza kidogo lakini nimeelewa. Kama hawawezi kumgusa mfalme, kwanini wasimguse mtoto wa Mfalme? Tuliliona hili kwa Kikwete sana; pale ambapo watu waliona ni ngumu kumgusa Kikwete wakaamua kumgusa Ridhiwani - kwa ukweli au la. Bahati mbaya Makonda amechukuliwa na wengi na jinsi alivyojengwa kama vile ni mtoto wa Magufuli mwenyewe na hivyo kama watu hawawezi kumgusa Magufuli basi watamgusa "mwanaye mpendwa aliyependezwa naye". 

Lakini, ukiondoa tuhuma za vyeti - ambazo kama nilivyoelezwa jana kwenye ZamaMpya - kwa kiasi kubwa zile zilikuwa ni siasa zaidi. Kulikuwepo na hoja lakini haikuwa hoja kubwa kivile bahati mbaya ni hoja inayomhusu mpendwa wake na hivyo imekuwa hoja kubwa. Kama ingewezakana kumuangusha Makonda kwa suala la cheti wangeweza lakini naamini lile lilikuwa linapita na nilitarajia lipite kwa maelezo machache tu. Ikulu ingeweza kulizima lile hata kwa hadaa za kisiasa (serikali inafuatilia tuhuma mbalimbali dhidi ya Makonda lakini hadi hivi sasa Rais ana imani naye - kauli ingesema). Watu wangekasirika na kulalamika lakini lingepita. 

Nina uhakika lingepita kwa sababu hata waliotoa tuhuma zile za vyeti wanajua kabisa kuwa kipimo hicho kikiendelea kutumiwa kwamba hata mtu aliyesoma baada ya kubadilishwa jina lake na wazazi wake akiwa darasa la saba au kidato cha nne basi wengi watakwenda na maji. Wengi walikuwa na ukali zaidi kwa mtu aliyefoji cheti cha taaluma kuliko aliyetumia jina jingine kwenda kusoma na kupata taaluma ya ukweli. Kuna tofauti ya John Juma kusema ana shahada ya uhandishi na kuonesha cheti wakati hana elimu hiyo bali cheti kanunua mtaani na mtu ambaye anaitwa Juma John ambaye jina lake la asili ni Fredy Ramadhani. Juma John akaenda akasoma, akafaulu, akaenda chuo kikuu akapasi vizuri akiwa na jina hilo jingine na akawa na elimu ya uhandisi na kazi yake ikaonekana ana tofauti sana na John Juma mwenye cheti feki! Sidhani kama kuna mtu ambaye ama shule ya msingi au sekondari ambaye hakuwa kukutana au kusoma na kina Juma John na akawaheshimu. 

Kuwafukuza kina Juma John kazi baada ya kuwekeza kote katika elimu yao ni dalili ya kutokuwa na hekima na kukosa ubunifu wa kusahihisha na kuadhibu makosa ya wa zazi wao lakini bila kuwapoteza hawa hasa kama ni watu wenye weledi na waadilifu. Bora unipe Juma John kuliko mtu ambaye ana jina lake la asili na amesome kote lakini hajaelimika, hana weledi na ni janga katika mahali pa kazi. Kuna faida gani ya kuwa mtu mwenye jina halisi lakini hana a wala be ya utendaji? Ndio maana nasema suala la cheti halikuwa kubwa isipokuwa limekuwa kubwa kwa sababu ni la mpendwa wa Rais. 

NI kwa sababu hiyo basi naamini, tuhuma hizi mbili kubwa za wiki iliyopita ni kubwa mno kiasi kwamba wanaotaka Makonda aondolewe - hata kwa kuwa demoted - wanafanya hivyo kwa haki na ni ushindi ambao wameushinda. 

Katika mapambano kuna kushindwa baadhi ya mapigano; si lazima ukubali umeshindwa vita. Magufuli raia wangu kwenye hili la Makonda umeshindwa pigano hili, na kwa vile wewe pia ni mwanasiasa unajua ni wakati gani wa kukubali kushindwa na kuamua kujipanga upya. Na njia mojawapo ya kujipanga ni kuhakikisha watendaji wako huwafanyi wawe walengwa wa kuangushwa na mojawapo ni kuhakikisha wanasimamiwa vizuri katika utumishi. 

Kwa sababu sasa hivi ukiangalia kinachohojiwa siyo tena Makonda bali ni wewe mwenyewe. Kama ulimuondoa Kitwanga kwa kuhutubia Bunge akiwa amelewa na alikuwa ni Waziri na inadaiwa alikuwa ni rafiki yako wa karibu ni kitu gani kimefanya mtu mwenye tuhuma kama za Makonda kuendelea kuwepo hata kwa siku nyingine moja? Maana hata Mlevi anaweza kusema kweli akiwa amelewa na akawa sahihi! 

Rais wangu Magufuli wape wapinzani wako ushindi huu kwani wamekushinda katika hili; halafu twende kwenhye mambo mengine ya kitaifa na ya kulijenga taifa, siyo ya kutafuta kujibu mashambulizi, kukomoa na visasi. Acha kazi yao na utendaji wako useme wenyewe. Waache Watanzania waangalie jinsi unavyotekeleza kazi zako na unavyowasimamia watendaji wako. Usiwape mianya isiyo ya lazima. 

Lakini ukiwapa mianya hiyo, usishtuke, usikasirike wala kukwazika wao nao wakaaitumua kukugonga na wewe mumo kwa mumo. 

Ndio siasa hiyo. Kuna magoli unaweza kuyapinga lakini mengine inabidi ukubali tu umefungwa. Huitaji kamera kukuonesha goli limeingia kweli kweli.


Install Application ya Udaku Special Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi
=>BOFYA HAPA KUINSTALL/DOWNLOAD

Share:
Weka Maoni yako Hapa

0 facebook:

Post a Comment

Total Pageviews


Popular Posts

Matangazo

Copyright © UDAKU SPECIAL | Powered by Blogger