KWA Utajiri Huu wa Ridhiwani Kikwete,,Bill Gates Haoni Ndani..!!!!

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA


Ukipanda daladala huwa hakuna mfumo unaoeleweka, siku nyingine utakutana na kelele kama sokoni, wale wanaongea yao, hawa wanabishana hivi, hapa napo kuna ubishi wa soka.

Siku nyingine ndani ya daladala kama mnasindikiza msiba, kimya kinatawala. Wakati mwingine kuanzia mwanzo wa kitu mpaka mwisho ni ugomvi tu kati ya kondakta na abiria. Kimsingi daladala huwa haina utaratibu maalum.

Nikipanda daladala huwa napenda kukaa siti ya mbele au karibu na dereva ili nijifunze jinsi ya kuendesha. Si unajua tena, wanasema ukiwa karibu na mahakama lazima utajua vifungu vya sheria. Matunda ya ujirani hayo.

Nikiwa namtolea macho dereva jinsi anavyobadili gia kwa mbwembwe, abiria aliyekuwa amekaa pembeni yangu akanifinya, nilipogeuka akanipa ishara nitazame mlangoni. Kulikuwa na mrembo anaingia.

Yule abiria jirani yangu alimfuatilia yule mrembo mpaka alipokwenda kuketi, kisha akanigeukia na kuniambia: “Kaka umeona mambo ya Ridhiwani Kikwete?”

Nikawa sijamuelewa, nikamuuliza: “Ridhiwani Kikwete amefanya nini hapo?”

Akasema: “Kaka si unaona mwenyewe mwanamke alivyo mzuri, ameumbika. Yule siyo wa kawaida.”

Nikamuuliza tena: “Sasa kuumbika kwa huyo mwanamke kunahusiana nini na Ridhiwani?”

Akanijibu: “Kumbe wewe ndugu yangu umechelewa mjini, nilivyokuona nilidhani mchangamfu mwenzangu wa jiji. Kwa taarifa yako misemo yetu sisi watoto wa mjini ni kwamba vitu vizuri tunaita mambo ya Ridhiwani.

“Magari yote mazuri mjini ni Ridhiwani, vituo vya mafuta vikubwa vyote Ridhiwani, maghorofa makubwa ni Ridhiwani, ndiyo maana na wanawake wazuri wote mjini tunasema ni mambo ya Ridhiwani.”

Aliposema hivyo, alinikumbusha kitu. Ikabidi niingie kazini kufanya mahojiano, maana habari za Ridhiwani na utajiri wake ni nzito na zimekuwa zikizungumzwa kwa kitambo kirefu sasa.
Nikamuuliza yule abiria: “Lakini ndugu yangu wewe si una mke? Ni mzuri au mbaya?”

Akajibu: “Wewe unaniona mimi wa kuja? Siwezi kuoa mwanamke mbaya. Mke wangu chuma, kisu kikali, mrembo hasa, tena niliwahi kugombana na Hashim Lundenga alipotaka kumchukua kumuingiza kwenye mashindano ya Miss Tanzania.”

Hapahapo ndipo nilikuwa napataka, nikamuuliza: “Wewe mkeo akiitwa wa Ridhiwani utafurahi?”
Haraka sana alijibu: “Thubutu, patachimbika siku hiyo.”

Uzuri alikuwa anajileta mwenyewe, nikampiga swali lingine: “Sasa mbona wewe unaona sawa kusema wake wa wenzako kuwa ni mali ya Ridhiwani?”

Safari hii kwa utulivu akasema: “Umeniuliza swali lenye maana kubwa, unajua mjini watu wanakuza sana maneno. Kuna kipindi nilikuwa nikisikia jina la Ridhiwani nilikuwa naogopa, siku nilipomuona nikashangaa, kumbe mtu mwenyewe ana umbo dogo tu, tena wa kawaida.”

Aliposema hivyo, siti ya nyuma yetu alikuwepo mtu ambaye alikuwa anafuatilia mazungumzo yetu, akauliza: “Samahani kaka, kama sijakosea nimekusikia ukisema Ridhiwani ana umbo la kawaida, tena dogodogo, hivi ni kweli?”

Abiria pembeni yangu akajibu: “Wa kawaida ndiyo, kwani ulifikiriaje?”

Abiria wa siti ya nyuma akasema: “Jamani hii dunia kumbe unaweza kumuogopa mtu mdogo ambaye unaweza hata kumzaa. Mwenzenu kwa jinsi stori za Ridhiwani zilivyo na jinsi anavyozungumzwa, mimi nilifikiri ni jitu kubwa la miraba minne mara 10.

“Tena niseme ukweli, mimi nilikuwa nafikiri Ridhiwani ni mkubwa kama zimwi, yale madude ya kutisha ya kwenye hadithi za kale. Nashangaa leo unaniambia kumbe Ridhiwani wa kawaida tu. Kusema ule ukweli leo nimestaajabu.”

Abiria mwingine naye akachangia, sasa mada ilikuwa imeshakua na kupanuka ndani ya daladala. Huyu alikuwa mzee. alisema: “Nyie vijana, mimi mwenyewe nilikuwa nasikia sana habari za Ridhiwani kuwa anamiliki mali nyingi, na nikawa naamini kweli na nikawa natangaza.

“Juzi hapa nikashangaa kuna nyumba yangu ghorofa moja nilijenga wakati mambo yangu yakiwa mazuri, nimeshindwa kuimaliza kwa sababu fedha zimekata, ghafla nakuta watu wanaijadili kuwa ile nyumba yangu ni ya Ridhiwani ameisahau ndiyo maana hajaimaliza.

“Tena wale watu walikuwa wanasema Ridhiwani ana nyumba nyingi mpaka nyingine anazisahau. Niliwaambia ile nyumba ni yangu, hakuna aliyenielewa, tena waliniambia nimetumwa.”

Sauti ya kike kutoka nyuma ikasikika: “Kila kitu wanasema cha Ridhiwani, magari, majumba, makontena, migodi, bado kidogo wataanza kutangaza na wake zao ni mali ya Ridhiwani. Ikifika kipindi hicho tukumbushane.”

Mwanamke mwingine akadakia: “Bado kidogo wapi? Mwenzenu usiku leo nimepokea mkong’oto wa maana kutoka kwa mume wangu, kanipiga kweli. Hatukuwa na ugomvi wowote, kafika ananiuliza kama namfahamu Ridhiwani, nikamjibu ndiyo. Hapo ndiyo ikawa chanzo cha ugomvi.

“Akaniuliza tena namfahamu kivipi, nikamjibu kupitia kumsoma kwenye magazeti na kumuona katika televisheni. Mume wangu hakuamini, akasema hana imani na mimi kwa sababu anasikia wanawake wote wazuri ni wa Ridhiwani. Nikamwambia aache wivu wa kijinga, hapo ndipo nilianza kupokea mkong’oto. Mwili wote unauma hapa nilipo.”

Gari lilikuwa limefika Posta, nilipokuwa nashuka nikapata wazo la kuendelea na usaili wangu. Nikamuuliza mpigadebe mmoja: “Unamfahamu Ridhiwani Kikwete?”

Akanijibu: “Namfahamu sana Ridhiwani, yule ni kibosile. Kwanza ni mwili nyumba, bajeti ya serikali yote inamtegemea yeye. Hapahapa mjini ana majumba kibao.”

Mpigadebe akaanza kunionyesha nyumba za Ridhiwani, akasema: “Unaona hii hapa? Mwenyewe ni Ridhiwani. Ila unajua Ridhiwani huwa hapendi sifa za kujulikana kama ana utajiri mkubwa, ndiyo maana hii hapa imeandikwa Benjamin William Mkapa Pension Tower. Huyu Benjamin amewekwa kama geresha tu. Mwenye mali Ridhiwani.”

Akanizungusha, akasema: “Unaona hii?” Ni jengo la PPF Tower, akasema: “Huyu PPF Tower naye amewekwa tu kama geresha, hili ghorofa la Ridhiwani.”

Tukasogea mbele, tukakutana na jengo la Golden Jubilee Tower, akasema: “Kaka umeona Ridhiwani alivyo mjanja, yaani majengo yake yote ameyapa majina tofauti. Huyu Golden Jubilee Tower naye kawekwa tu hapa, mwenye mali ni Ridhiwani.”

Tukiwa tumesimama nje ya jengo la Golden Jubilee, mpigadebe akanionesha jengo la Viva Tower, akasema: “Lile pia la Ridhiwani. Viva Tower naye kama wenzake, amewekwa tu. Nimeshakwambia Ridhiwani hapendi sifa.”

Tukiwa tunatembea kwa miguu kunionesha mali za Ridhiwani ambazo mpigadebe huyo anazijua, alisema: “Ila ukitaka kujua kama Ridhiwani ni mjanja, majengo yake yote jina la mwisho ameita tower ili wasimuibie. Tower ni jina la mtoto wake.”

Tukajikuta tumesimama nje ya majengo pacha ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT), mpigadebe akaniambia: “Kaka nimekwambia kuna watu wana fedha hapa nchini, unaona haya maghorofa mawili mbele yetu yanayofanana? Yote haya ni ya Ridhiwani.”

Hapo nikaguna, nikamuuliza: “Mbona haya majengo ni ya BOT?”

Naye akaniuliza: “BOT ndiyo nini?”

Nikamjibu: “BOT maana yake ni Benki Kuu.”

Huku akitabasamu, akasema: “Unaona sasa, bila shaka utakuwa umeamini haya majengo ni ya Ridhiwani kwa sababu hata hiyo Benki Kuu unayoisema ni ya Ridhiwani.”

Mpigadebe akanipeleka kwenye majengo pacha marefu kuliko yote Afrika Mashariki na Kati, PSPF Commercial Twin Tower, tukaenda Rita Tower, Uhuru Heights, Umoja wa Vijana Complex na mengine mengi, kote huko alisema: “Mambo ya Ridhiwani kaka, huyu mtu ni kiboko.”
Kwa kutumia simu yangu, ‘niligugo’ na kupata picha ya Ridhwani, nikamuonesha yule mpigadebe kisha nikamuuliza kama anamfahamu, akanijibu ni sura ngeni, hamtambui kabisa.

Nikamwambia huyo ndiye Ridhiwani, yule mpigadebe nusura anichape makofi, akasema: “Toa ujinga wewe, huyo mtoto mdogo anawezaje kuwa Ridhiwani? Ridhiwani ni jitu lenye mwili wake, kwanza haonekani hovyohovyo.”

Alipoona nimekaa kimya, akaniambia: “Huyu alikuwa rais wetu, Jakaya Kikwete si unamjua?” Nikamjibu ndiyo, akasema: “Kwa taarifa yako Ridhiwani ndiye baba wa Kikwete, ndiye amemfanya Kikwete awe rais, ana hela Ridhiwani mpaka yeye mwenyewe zinampa homa.”

Nilipoachana na yule mpigadebe, moja kwa moja nilikwenda Kariakoo, nikakutana na mtu amejiinamia, nilipomuuliza kama anamfahamu Ridhiwani, akanijibu harakaharaka: “Umenitajia hilo jina nahisi kama nakaribia kuuaga umaskini.”

Nikamuuliza: “Kivipi?”

Jawabu lake lilikuwa hili: “Natamani kukutana naye anipe kazi, si unajua anamiliki miradi mingi? Hesabu Daraja la Kigamboni, Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi, ana mabasi na malori mpaka idadi haitambui, majumba na viwanja. Jumlisha Uwanja wa Taifa na ule wa Uhuru baada ya kuununua, sasa hivi yupo anaufanyia marekebisho ili uwe wa kisasa.”

Nilimaliza usaili wangu nikiwa nimechoka kabisa. Niliporudi nyumbani jioni, nilimuuliza mtoto wangu, Captain Nyambo: “Captain unamjua Ridhiwani?”

Captain Nyambo alijibu: “Unamzungumzia Ridhiwani mbunge wa Chalinze, mtoto wa Dk. Jakaya Kikwete?”

Sikuona sababu ya kumjibu swali lake, maana aliniuliza kwa mtindo wa majigambo kuwa anamfahamu sana, nikamuuliza lingine: “Vipi kuhusu utajiri wa Ridhiwani?”

Akanijibu kwa kuniuliza: “Ukitaka stori za Ridhiwani kama changamsha genge, unaweza ukashangaa hata mimi mtoto wako mpendwa naambiwa ni wa Ridhiwani, kwa sababu kila kitu kizuri kimekuwa cha Anko Rizi.”

Nikamwangalia Captain Nyambo, mwenyewe wala hakutetereka, akasema: “Captain Mkuu si mwenyewe huwa unaona mambo yangu ya shuleni? Wabongo hawashindwi kusema Captain Nyambo ana akili sana, atakuwa mtoto wa Ridhiwani.”

Alipoona sifurahishwi na maneno yake, Captain Nyambo aliniambia: “Wewe ndiye baba yangu, Ridhiwani hana ubavu wa kunipata, Mungu amenifanya wewe ndiye uwe baba yangu, ndiyo maana nakupenda halafu tunaelewana sana.”

“Captain Mkuu eeeh,” Captain Nyambo aliniita, nilipoitika alisema: “Tuache hizo stori za Ridhiwani, hazina tija kwetu. Ila kiukweli baba Tanzania ni ya ajabu sana, yaani kama kila kinachosemwa ni cha Ridhiwani kingekuwa kweli, basi huyu mtu angekuwa tajiri kuliko tajiri namba moja ulimwenguni, Bill Gates.”

By Luqman Maloto
+255 713 355 717
-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad