Watu Wawili Wauwawa katika Nyumba ya Kulala Wageni

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA

Watu Wawili Wauwawa katika Nyumba ya Kulala Wageni
UTATA umeibuka baada ya miili ya watu wawili waliouawa na watu wasiojulikana kukutwa katika nyumba ya kulala wageni mjini Tanga ikiwa haina nguo na imefungwa kamba za miguu na mikononi.

Katika tukio hilo ambalo limethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedicto Wakulyamba miili ya watu wawili, wote wanaume, iligunduliwa jana majira ya saa mbili asubuhi na mhudumu wa nyumba ya kulala wageni ya Bomai Inn iliyopo Kata ya Majengo jijini hapa.

Kamanda Wakulyamba aliwaambia waandishi wa habari jijini hapa jana kuwa mhudumu wa nyumba hiyo ambaye hakumtaja kwa jina, alibaini kuwapo kwa miili hiyo alipotaka kufanya usafi ndani ya chumba hicho.

"Majira ya saa mbili asubuhi wakati mhudumu alipoingia ndani ya chumba hicho namba 303 kwa ajili ya kufanya usafi, alikutana na miili ya watu hao wawili wote ni wanaume ikiwa imelala chini, imefungwa kamba miguuni na mikononi," alisema.

Kamanda huyo alisema miili hiyo ni ya watu wanaokadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 35 na 40 ambao hawakutambulika mara moja.

Alisema kuwa kwa mujibu wa kumbukumbu za kitabu cha wageni cha nyumba hiyo ya kulala wageni, mtu anayeitwa Rashid Omari alijiandikisha kutumia chumba hicho siku hiyo.

Alisema kwa mujibu wa kumbukumbu hizo, Omari ni Msafa kwa kabila, mkazi wa Dar es Salaam na ni mfanyabiashara.

Kamanda Wakulyamba alisema miili hiyo haikuwa na jeraha lolote zaidi ya michubuko ya kawaida na kwamba Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kubaini sababu za mauaji hayo na waliohusika kuyatekeleza ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Vifo vya watu hao vimezua utata kutokana na waliouawa kutofahamika kwa wakazi wa eneo hilo, mazingira ya vifo vyao kuashiria mauaji, wauaji kutojulikana pamoja na kitendo cha uongozi wa nyumba hiyo ya kulala wageni kuruhusu wanaume wawili walale chumba kimoja, kinyume cha taratibu za uendeshaji wa biashara hiyo.

"Watu wawili tena wanaume kuuawa ndani ya chumba kimoja na kusiwe na hata mtu aliyesikia kurupushani za mauaji hayo... inatia hofu kubwa na inawezekana kuna mpango maalum wa wauaji hao," alisema Asha Ramadhan, mmoja wa walioshuhudia tukio hilo la utoaji miili hiyo.

Hamza Issa, mkazi mwingine wa maeneo hayo, alisema huenda mauaji hayo yalipangwa na aliyelipia kutumia chumba hicho kabla ya kukutwa miili ya watu wawili.

Mkazi mwingine wa maeneo hayo, Anthon Aloys, alisema huenda maiti hizo ziliingizwa ndani ya chumba na mkodishaji chumba hicho baada ya watu hao kuuawa eneo jingine.

WATU WATATU
Matukio ya wanaume zaidi ya mmoja kuuawa wakiwa katika chumba kimoja cha nyumba za wageni yalififia kwa muda lakini si uhalifu ambao ni mgeni.

Machi 21, mwaka jana watu watatu walikutwa wakiwa wameuawa kwa kunyongwa katika nyumba ya kulala wageni ya Mexico, mjini Kyela mkoani Mbeya, ikiwa na majeraha ya kuunguzwa kwa moto.

Mganga mfawidhi wa Hosptali wa Wilaya ya Kyela, Dk. Francis Mhagama alikaririwa akisema maiti hizo za watu watatu zilikuwa zimenyongwa pamoja na majeraha ya moto.

Kwa mujibu wa kitabu cha wageni cha nyumba hiyo, majina ya watu hao yalikuwa Hassan Ally, Mariam Hassan na Adam.

Aidha, Agosti mosi, mwaka jana pia watu wawili walikutwa wamefariki katika nyumba ya wageni ya Kings Rest House iliyopo Mtaa wa Bumila, Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam huku miili yao ikiwa imeungua moto.

Watu hao waliofariki walikuwa wafanyabiashara wanaouza ng’ombe katika mnada wa Pugu na mara nyingi walipokuja jijini walifikia hapo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni alisema mmoja wa waliofariki alijiandikisha kama Lameck Ludovick, mfanyabiashara na mkazi wa Dar es Salaam.

-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad