Shaidi Ashindwa Kujua Kilichosababisha Kifo cha Kaka Yake

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA

Mdogo wa Kanumba Hajui Kilichosababisha Kifo cha Kaka Yake
Wakati kesi ya mauaji ya mcheza filamu maarufu nchini, Steven Kanumba ikianza kuunguruma, shahidi wa upande wa mashtaka ameileza mahakama kuwa hajui aliyesababisha kifo cha msanii huyo.

Katika kesi hiyo iliyoanza jana Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam, Elizabeth Michael Kimemeta, ambaye pia ni msanii wa filamu akijulikana zaidi kama Lulu , ameshtakiwa kwa kosa la kumuua Kanumba bila ya kukusudia.

Lulu, ambaye yuko nje kwa dhamana, anadaiwa kufanya kosa hilo eneo la Sinza Vatican wakiwa nyumbani kwa Kanumba Aprili 7, 2012.

Aliposomewa maelezo ya awali mwaka 2014, Lulu alikana kuhusika na mauaji hayo, jambo ambalo liliilazimu upande wa mashtaka kuita mashahidi kuthibitisha shtaka hilo dhidi ya mshtakiwa.

Kwa mara nyingine, jana msaanii huyo aliposomewa shtaka hilo alikana kuhusika, ndipo upande wa mashtaka ukamuita shahidi wake wa kwanza kwa upande wake, Seth Bosco (30) ambaye ni mdogo wa marehemu Kanumba.

Shahidi huyo aliieleza mahakama kuwa alikuwa akiishi pamoja na Kanumba Sinza Vatican na kwamba siku ya tukio kaka yake na mshtakiwa ambaye alikuwa ni mpenzi wake, walifika nyumbani saa 6:00 usiku.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Faraja George, shahidi huyo alidai kuwa akiwa chumbani kwake alisikia kelele za ugomvi baina ya Kanumba na Lulu na kwamba baada ya muda Lulu alitoka na kumueleza kuwa Kanumba ameanguka.

Aliongeza kuwa alikwenda chumbani akamkuta Kanumba akiwa katika hali ya kukosa hewa, ndipo akamfuata daktari wao, kisha wakampeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili. Baada ya kuchunguzwa ikabainika kuwa alikuwa ameshafariki dunia.

Hata hivyo, alipoulizwa na moja wa wazee wa Baraza, Rajabu Mlawa baada ya kutoa ushahidi wake, kama anajua aliyesabisha kifo cha msanii huyo, shahidi huyo alisema hajui.

Mzee wa Baraza: Katika kumchunguza kwako marehemu baada ya tukio hilo, ulibaini kwamba marehemu alipata madhara gani?

Shahidi: Madhara niliyoyabaini ni kukosa pumzi

Mzee wa Baraza: Hayo madhara ya kukosa pumzi yalisababishwa na ugomvi ule?

Shahidi: Kwa hilo mimi siwezi kujua nini kilisabisha kukosa pumzi.

Mzee wa Baraza: Umesema kuwa ulipokwenda chumbani kwa marehemu ulimkuta ameanguka akiwa ameegemea ukutani, unajua ni nani alisababisha tukio la kuanguka?

Shahidi: Siwezi kujua ni nani aliyesababisha kwa sababu mimi sikuwemo mle ndani

Wakati akihojiwa na wakili wa mshtakiwa, Peter Kibatala, kama alikuwepo wakati sampuli za mwili wa marehemu zikichukuliwa kwa ajili ya vipimo vya maabara, kama ilivyoandikwa kwenye maelezo yake, alisema hakuwepo.

“Mimi sikuwepo wakati wa kuchukua sampuli za mwili wa marehemu. Alikuwapo ndugu yangu mwingine, mimi nilikuwepo kwenye mostmortem (taarifa ya kitabibu ya chanzo cha kifo) ya kawaida.”

Wakili Kibatala: Kwa hiyo aliyeandika hapa alikuwa akibuni?

Shahidi: Siwezi kusema kuwa alikuwa akibuni, labda kama ungemuuliza mwenyewe.

Wakili: Katika maelezo yako Polisi ambayo uliyaandika muda mfupi tu wakati wa tukio, kuna mahali ulipoeleza polisi kwamba ulipokwenda kumfuata Dk Paplas ulimwambia mshtakiwa abaki na marehemu?

Shahidi: Hakuna mahali ambapo kuna kipengele nilipomweleza polisi kuwa nilimuacha Elizabeth Michael na marehemu (Baada ya kusoma maelezo yake)

Hata hivyo, alipoulizwa tena na Wakili wa Serikali, George kuhusu kuwepo kwa tofauti ndogondogo katika maelezo yake aliyoyaandika polisi na yale aliyoyatoa kwenye ushahidi wake mahakamani, shahidi huyo alieleza kuwa yeye alikuwa akihojiwa tu na aliyekuwa akiandika ni askari.

Kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Sam Rumanyika iliahirishwa na itaendelea tena leo kwa mashahidi wengine wa upande wa mashtaka kutoa ushahidi wao.

Awali Wakili George aliieleza mahakama kuwa alitegemea kuwa na mashahidi wawili jana, akiwemo Dk Kageiya, lakini wakati wakifanya mazungumzo na shahidi huyo, aliwaeleza kuwa hajisikii vizuri na kuomba atoe ushahidi wake kesho.

Pia Wakili George aliileza mahakama kuwa wataomba kuongeza shahidi mwingine ili wafikie watano.
-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad