Twaweza: Asilimia 67 ya Watanzania Wanataka Katiba Mpya

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA

Wananchi wawili kati ya watatu wanasema Tanzania inahitaji katiba mpya, huku nusu ya wananchi wanasema mchakato wa Katiba uanze upya na tume mpya.

Matokeo haya yametolewa na Twaweza katika utafiti uitwao Zege imelala? Maoni ya wananchi kuhusu kukwama kwa mchakato wa kuunda katiba mpya.

Imesema muhtasari unatokana na takwimu kutoka Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu za mikononi. Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze amesema, “Wananchi wanataka katiba mpya. Wengi wao wanataka mchakato uanze upya na tume mpya katika ukurasa mpya. Hata hivyo, wapo wananchi ambao wapo tayari kusonga mbele kwa kutumia rasimu iliyoandaliwa na tume iliyotangulia.”

Amesema leo Alhamisi Oktoba 19,2017 kuwa, cha msingi ni kwamba, wananchi wanaunga mkono kipengele kilichoongeza madaraka ya Bunge katika suala la kuwapitisha mawaziri walioteuliwa, na kinachowapa wananchi haki ya kuwaondoa wabunge wanaozembea kazini.

Eyakuze amesema utafiti umedhihirisha uwajibikaji wa siasa kwenye uhalali wa mchakato wa katiba.

Amesema, “Matokeo yameonyesha dhahiri kwamba wananchi wengi wanatatizwa katika kutofautisha kitendo cha Ukawa kugomea Bunge la Katiba na migomo mingineyo. Ushabiki wa kisiasa huwafanya watu wengi kutozingatia uhalali wa jambo husika.”

Eyakuze amesema, “Hivyo basi; vyovyote tutakavyofufua mchakato wa katiba, ni muhimu kwa wahusika wakuu kuheshimu na kutambua kwamba sheria mama ya nchi ni ya thamani zaidi kuliko tofauti za kisiasa. Tanzania inahitaji mchakato wa katiba utakaozingatia uhalali na ujumuishi wa Watanzania wote.”

Twaweza: Asilimia 67 ya Watanzania Wanataka Katiba Mpya
Taarifa ya Twaweza kwa vyombo vya habari imesema asilimia 67 ya Watanzania wanasema ni muhimu kwa Tanzania kupata Katiba mpya na asilimia 56 wanasema toleo la mwisho la rasimu ya Katiba lipigiwe kura na wananchi.

Hata hivyo, asilimia 48 ya wananchi wanasema kwa maoni yao, Katiba mpya haitapatikana ndani ya miaka mitatu ijayo.
Taarifa hiyo imesema wananchi wanaendelea kuunga mkono kwa nguvu kubwa uundwaji wa Katiba mpya inayotilia mkazo suala la uwajibikaji.

Imesema asilimia 79 wanataka mawaziri wanaoteuliwa wapitishwe na Bunge na asilimia 64 wanataka wawe na uwezo wa kuwaondoa wabunge katikati ya uchaguzi iwapo hawatatekeleza majukumu yao ipasavyo.
Hata hivyo, wananchi wamegawanyika kwenye baadhi ya hatua za uwajibikaji zilizopendekezwa ikiwemo kuzuia viongozi na watumishi wa umma kuwa na akaunti nje ya nchi (asilimia 52 wanaunga mkono), kuwepo kwa ukomo wa ubunge (asilimia 52 wanaunga mkono) na kuweka kanuni za uwazi na uwajibikaji kuwa sehemu ya tunu za Taifa (asilimia 48 wanaunga mkono).

Hivi vyote ni vipengele vya rasimu ya Katiba ambavyo viliondolewa na Bunge Maalumu la Katiba.

Twaweza imesema wananchi pia wanaunga mkono kuondolewa kwa kipengele kinachotaka kuchunguza na kudhibiti Ofisi ya Rais (asilimia 55) na mawaziri kuchaguliwa kutoka nje ya Bunge (asilimia 62).
Matokeo hayo Twaweza imesema yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,745 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara (Zanzibar haihusiki kwenye utafiti huu) Juni hadi Julai 2017.
Kuhusu muundo wa Serikali ni moja kati ya vipengele vilivyoibua mjadala mzito wakati wa mchakato wa kuunda Katiba Mpya na hatimaye kuwagawa wananchi. Asilimia 42 ya wananchi wa Tanzania Bara waliunga mkono muundo wa Serikali mbili.

Twaweza imesema muundo wa Serikali moja ulikubalika kwa asilimia 25 tu na muundo wa Serikali tatu uliopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ulipendwa na asilimia 16 tu.
-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad