Ticker

6/recent/ticker-posts

KUTANA NA SARAKASI ZA PREZZO KWA WAREMBO!

Nafasi za Ajira Serikalini Zilizotangazwa Wiki Hii Bonyeza HAPA

Nafasi za Internship Zilizotangazwa Bonyeza HAPA

Matokeo ya Form Four 2022 Bonyeza HAPA

JACKSON Ngechu Makini ‘CMB Prezzo’ alizaliwa siku ya Jumatano ya Januari 09, mwaka 1980. Ni rapa lejendari wa Kenya ambaye alikuwa mmoja wa mastaa waliowakilisha nchi zao katika Shindano ya Big Brother Africa ‘StarGame’, 2012.
Kama ulikuwa hujui, jamaa alizaliwa katika Jiji la Nairobi miaka 33 iliyopita, alikulia maisha ya kitaani eneo la Eastleigh na atakuwa mmoja wa wanamuziki wakali watakaoshusha bonge la burudani katika Tamasha la Matumani 2013 litakolofunga mitaa ya Jiji la Dar na viunga vyake kwenye Uwanja wa Taifa, Julai 7, mwaka huu. 
Prezzo ni mwanamuziki mkubwa ambaye alianza ‘kuhaso’ katika muziki miaka mingi, alikuja kuwika kwenye miaka ya mwanzoni mwa karne ya 21.
Pamoja na kukumbana na vipingamizi vingi, nyota ilikuja kung’aa baada ya nyimbo zake kukubalika kwa maelfu ya mashabiki wake waliokuwa wakizisikiliza, kuziomba kwenye stesheni mbalimbali za redio na runinga huku wakihudhuria katika matamasha yake ya wazi na klabu.
Albam yake ya kwanza ni Naleta Action aliyoiachia mwaka 2004 ikiwa na ngoma zilizoshika kama Naleta Action, Lets Get Down, Mahangaiko, Leo ni Leo, Mimi na Wewe, Mafans na nyingine zilizobamba.
Katika albam hiyo, jamaa alimshirikisha mama yake ambaye aliimba mistari kadhaa katika moja ya nyimbo zake.
Albam hiyo iliuza nakala nyingi na kumfanya Prezzo kuamini kuwa alishakubali Afrika Mashariki kutokana na aina ya ngoma zake zenye hisia.
Prezzo anajulikana kutokana na aina ya maisha ya gharama anayopendelea kama kuvaa mikufu ya bei ghali, nguo, magari ya vitu vingine vya kitajiri.
Baadaye mtu mzima Prezzo alishirikishwa kwenye ngoma ya Tazama Mbele ya aliyewahi kuwa mpenzi wake wa kipindi hicho iliyotengenezwa na Ennovator wa Samawati Productions huku video yake ikisimamiwa na Ted Josiah. Ngoma hiyo ilifanya vizuri kwa kushika namba moja kwa wiki nane katika stesheni mbalimbali za redio na runinga Afrika Mashariki.
Mwaka 2006, Prezzo aliachia singo mpya ya P.R.E.Z.Z.O ambapo video yake ilisimamiwa na Ted Josiah wa Blu Zebra. Video ilikuwa kali lakini ilikutana na maneno mengi ikidaiwa ilitengenezwa kwa gharama kubwa sana ya Sh. 500,000 za Kenya. Hakukuwa na video iliyokuwa imetumia kiasi hicho cha fedha kwa wakati huo.
Ulipita ukimya kidogo, akiendelea kugonga shoo za ndani na nje ya Afrika Mashariki, Nigeria na Ulaya. Baadaye aliendelea na mtindo wa kuachia singo mojamoja kama Liqher, My City My Town, Unataka Nini, 4sho 4shizzy aliyomshirikisha Ulopa, Nipe Nikupe aliofanya na AY na Celebration of Life aliyoachia hivi karibuni akimshirikisha Chess

BIG BROTHER AFRICA ‘STARGAME’ 2012
Prezzo aliingia kwenye kinyang’anyiro cha BBA ‘StarGame’ 2012 baada ya kuona ni kitu kitakachompa changamoto nyingi kwenye maisha.
Mbali na kutamani mkwanja, alitaka kuonekana kwenye runinga kubwa za Afrika kwa saa 24, na siku saba kwa kuwa ni mtu anayependa kuonekana kuwa yupo ‘attention.
Anasema anapenda kuangalia runinga na sinema kama Scarface na watu anaowazimia katika tasnia hiyo ni Al Pacino na Mos Def wa mtoni. Anakula chochote isipokuwa kitimoto. Kitabu anachokipenda ni 48 Laws of Power.

ANATAKA KUWA KAMA OBAMA
Sehemu anayoipenda Kenya ni Nairobi na haijalishi ni Kaskazini au Kusini ilimradi tu nyumbani ni nyumbani. Anatamani awe kama Rais Barack Obama wa Marekani kwa sababu anajiamini mwenyewe na anaweza kufanya kilichoshindikana kikawezekana kutokana na ushawishi alionao.

MAISHA YA MAPENZI
Katika masuala ya kimapenzi CMB Prezzo amekuwa gumzo kwa kipindi chote cha ustaa wake na mengi yamekuwa yakisemwa.

PREZZO NA SHEILA
Tukiacha huko nyuma akiwa mtoto wa vitoto, Prezzo aliwahi kugeuka gumzo baada ya kutoka na msichana mrembo wa Kenya, Sheila Mwanyigha ‘Nikki’.
Ni kweli wawili hao walidumu kwa muda mrefu huku wakitoka ‘out’ na kwenye shughuli mbalimbali wakitumia msafara wa magari ya gharama kama Limousine, yaani kama rais. Kuna wakati ilielezwa kuwa ndiye msanii wa kwanza kutumia helikopta Afrika Mashariki huku baadhi wakisema kuwa ilikuwa ya mama yake.
Pamoja na kudumu na Nikki kwa muda mrefu, ghafla ulipita ukimya huku kukiibuka madai kuwa alioa kimyakimya.
Hata hivyo, alipotangazwa kwenda BBA, kuliibuka habari kuwa ana mwanamke mwingine aliyetajwa kwa jina la Huddah Monroe ‘The Lady Boss’ ambaye aliiwakilisha Kenya BBA mwaka huu kabla ya kutolewa wiki ya kwanza

PREZZO NA GOLDIE
Akiwa mjengoni BBA, Prezzo alidaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Mshiriki wa Nigeria, Mwanamuziki Goldie aliyekutwa na umauti siku chache baada ya kumalizika kwa shindano hilo huku kukiwa na taarifa kuwa wawili hao walipanga kufunga ndoa ‘soo’.

PREZZO, DIVA NA THE LADY BOSI
Siku chache baada ya Goldie kufariki dunia, Prezzo alitimba Bongo kwa sababu ni rafiki mkubwa wa akina Ambwene Yessayah ‘AY’ ndipo kukaibuka madai kuwa alinasa kwenye penzi la Loveness Malinzi ‘Diva’ wa Clouds FM.
Kukawa na maneno mengi, Diva akapata ‘kick’ kwenye vyombo vya habari Afrika Mashariki na kwingineko.
Wakati hayo yakiendelea, hivi karibuni kuliibuka ‘drama’ nyingine. Safari hii The Lady Boss aliibuka na kudai kuwa Diva amemnyang’anya tonge mdomoni hivyo kuthibitisha kuwa pamoja na ukongwe, Prezzo naye ni sukari ya warembo!

Post a Comment

0 Comments