13 Jun 2018

Wema Sepetu na Wenzake Kuanza Kujitetea Mahakamani June 19

Kesi ya Madawa ya Kulevya Inayomkabili Wema Sepetu Kuunguruma June 19..... Yeye na Wenzake Wataanza Kujitetea
Muigizaji wa filamu Wema Sepetu na wafanyakazi wake wawili wanaokabiliwa na kesi ya kutumia dawa za kulevya katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wataanza kujitetea Juni 19, 2018.

Wema na wenzake walipaswa kuanza kujitetea leo Juni 13 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba na kwa upande wa mawakili ni Costantine Kakula wa Serikali na Wakili wa Utetezi Albert Msando.

Hata hivyo ilishindikana washtakiwa hao kuanza kujitetea kwa sababu Hakimu Simba alikuwa na kazi nyingine na kesi imeahirishwa hadi Juni 19, 2018 ambapo washtakiwa wataanza kujitetea.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Hakimu Simba kupitia ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na mashahidi watano wa upande wa mashtaka waliokuwa wakiongozwa na Wakili wa Serikali, Constantine Kakula na kutoa uamuzi uliowaona washtakiwa hao wana kesi ya kujibu na hivyo wanapaswa kujitetea.

Mbali na Wema washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ya kutumia dawa za kulevya ni Angelina Msigwa na Matrida Seleman Abbas.

Kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kukutwa na kiwango kidogo cha dawa za kulevya na kutumia dawa za kulevya.

Soma Zaidi: Wema kutumia siku mbili kuishawishi mahakama isimuadhibu

Inadaiwa kuwa Februari 4, 2017 katika makazi ya Wema huko Kunduchi, Ununio jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao walikutwa na msokoto mmoja na vipisi vya bangi vya uzito wa gramu 1.08.

Kwa upande wa Wema ambaye aliwahi kuwa mlimbwende wa Tanzania, mwaka 2006 anadaiwa kuwa Februari Mosi, 2017 katika eneo lisilojulikana jijini Dar es Salaam, alitumia dawa za kulevya aina ya bangi.
Chanzo: Mwananchi


Install Application ya Udaku Special Uweze Pata Habari Kama Hizi Kirahisi Zaidi
=>BOFYA HAPA KUINSTALL/DOWNLOAD
Weka Maoni yako Hapa

Popular Posts

Copyright © UDAKU SPECIAL BLOG | Powered by Blogger