12/16/2018

Kagame Apangua Tuhuma za Rwanda Kutaka Kuipindua Serikali ya Burundi


Rais Paul Kagame amesema nchi yake haitajiingiza katika kile alichoelezea kuwa ni uchokozi unaofanywa na Burundi na akaongeza kwamba kufanya hivyo ni "kuwapa kile wanachotaka."

"Tumekuwa na aina zote za uchokozi kutoka Burundi na hatujaangukia ndani. Kadhalika hatujahangaishwa na aina hizo za uchokozi kwa sababu hiyo itakuwa kuwapa kile wanachotaka, kuthibitisha hoja yao kwamba hawana tatizo jingine lolote isipokuwa Rwanda," amenukuliwa Kagame akiwaambia waandishi wa habari kando ya mkutano wa Majadiliano ya Kitaifa ya 2018.

Katika taarifa iliyochapishwa kwenye Twitter rasmi ya Rais wa Rwanda, Kagame aliwaambia waandishi wa habari kwamba Rwanda ilijiunga katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa hiari.

"Kwa Rwanda kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki ilikuwa hiari yetu lakini pia ilikuwa haki yetu. Haikuwa juu ya mtu yeyote kutufanyia upendeleo. Tulipojiunga na EAC hatukupiga magoti, kuwainamia watu watupatie upendeleo. Jitihada zozote za mtangamano zinahitaji kanuni ya toa na chukua. Kila nchi ina mamlaka huru lakini unapochagua ushirikiano, unaelewa kwamba baadhi ya mambo yatasitishwa. Watu wanakuja pamoja na kuunda kitu ambacho ni kikubwa zaidi kuliko mamlaka huru ya kila taasisi," alisema.

Kauli ya Kagame imekuja saa kadhaa baada ya kuchapishwa taarifa kwamba Rais Yoweri Museveni wa Uganda na mwenzake wa Burundi Pierre Nkurunziza, katika kipindi cha wiki moja, walitumiana barua zenye maneno makali zikionyesha wazi mgawanyiko unaotokota kati ya nchi za wanachama wa EAC.

Katika barua ya Desemba 4, 2018 kwa Museveni kama mwenyekiti wa sasa wa EAC, Rais Nkrunziza aliomba uitishwe mkutano wa dharura wa viongozi wa kikanda kutatua kile alichokiita "uvamizi" wa Rwanda dhidi ya nchi yake.

"Mbali na ukweli kwamba Rwanda iliandaa na kusimamia mapinduzi ya serikali ya mwaka 2015, wahusika wa uhalifu na wahalifu wengine wameweka makazi huko Rwanda ambako wanapata msaada wa kushambulia Burundi, kuvuka mpaka wa Rwanda-Burundi au kupitia mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, pamoja na kupata msaada na hati za kusafiria ili kuwawezesha kuzunguka katika ukanda huu na hata Ulaya," aliandika Nkurunziza.

Hata hivyo, Kagame alibainisha kuwa Rwanda ndiyo imekuwa ikikabiliwa na uvamizi kutoka nchi za jirani.
HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Weka Comment Yako Hapa Chini:
Share:
Loading...

0 [disqus]:

Post a comment

Copyright © UDAKU SPECIAL BLOG | Powered by Blogger