4/15/2019

Zitto Ampa kazi CAG, Aagiza Ukaguzi

Zitto ampa kazi CAG, aagiza ukaguzi
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Zuberi Kabwe, amefafanua kwamba licha ya ACT- Wazalendo kumtaka CAG Prof Mussa Assad kwenye ripoti yake ya mwaka 2017/18 afanyie kazi ukaguzi wa ununuzi wa ndege sita zinazoendeshwa na Kampuni ya ndege nchini, ATCL bado imeshindikana.

Zitto ameyasema hayo wakati akichambua ripoti ya Prof Assad iliyopelekwa bungeni wiki iliyopita na kisha kutolewa kwa umma.

Akiichambua ripoti hiyo, Zitto ambaye pia ni Kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo amesema kwamba hawajafanikiwa kuona ukaguzi wa manunuzi ya Ndege ikiwemo ununuzi wa ndege za Shirika la Ndege Nchini, ATCL ambao kwa sehemu umefanyika mwaka wa fedha 2016/17 na 2017/18.

"Katika uchambuzi wetu wa ripoti ya CAG ya mwaka jana (ripoti ya mwaka wa fedha wa 2016/17) tuliwaeleza kuwa katika ripoti ile licha ya kuwa ni taarifa bora sana kwa maudhui na uchambuzi, kuna mambo muhimu kadhaa ambayo CAG aliyaacha. Na tukamtaka kwenye ripoti yake ya mwaka 2017/18 ayafanyie kazi, mojawapo ni ukaguzi wa Ununuzi wa Ndege Sita (6) zinazoendeshwa na Kampuni ya Ndege nchini, ATCL".

"Mpaka sasa Serikali imeshatumia jumla ya Shilingi Trilioni 1 kununua ndege sita, na katika makadirio ya bajeti ya mwaka 2019/20 yanayoendelea sasa bungeni. Serikali imeomba Bunge liidhinishe shilingi Bilioni 500 kwa ajili ya kulipia ndege mpya nyingine. Ufuatiliaji wetu umegundua kuwa Serikali imekuwa ikichukua Fedha za Umma kupitia fungu 62 (Wizara ya Uchukuzi) na kufanya manunuzi ya ndege" amefafanua.

Ameongeza, "ndege hizo wanakabidhiwa Wakala wa Ndege za Serikali kama wamiliki na shirika la ATCL linakodishiwa ndege hizo kwa Mkataba maalumu (ambao haujawekwa wazi popote, hata kwa Bunge). Tulitarajia kuwa ripoti hii ya CAG ya mwaka 2017/18 kwenye ukaguzi wa fungu namba 62 tungeweza kuona ukaguzi wa manunuzi ya ndege hizi. Lakini Serikali kwa lengo la kuficha taarifa imeamua kuhamishia kwenye Ofisi ya Rais (fungu 20) Wakala wa Ndege za Serikali kupitia tangazo la Serikali namba 252 la Juni 2018".

Aidha Zitto ameendelea kufafanua kwamba, "tumetafuta taarifa ya ukaguzi wa fedha hizo za umma zilizofanya manunuzi ya ndege bila mafanikio. Tunamwomba CAG, afanye ukaguzi maalumu wa fedha za umma Shilingi Trilioni 1 zilizotumika kununua ndege. CAG afanye ukaguzi wa usimamizi wa mkataba wa ukodishwaji wa ndege hizo kati ya Wakala wa ndege za Serikali na Shirika la Ndege la ATCL ili Watanzania wajue matumizi sahihi ya fedha zao za kodi".

Pamoja na hayo Zitto ametoa tahadhari kwamba kutokana na uzoefu alionao inaonyesha kwamba kila jambo lenye harufu ya wizi au matumizi yenye mashaka basi Serikali huliamishia jambo hilo ikulu kwa kuwa inajua ukaguzi wake hautawekwa wazi.
HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Share:
Loading...

0 [disqus]:

Post a Comment

Loading...

Popular Posts

Copyright © UDAKU SPECIAL BLOG | Powered by Blogger