9/18/2019

Mwandishi Kabendera afanyiwa vipimo


MWANDISHI wa habari za uchunguzi nchini Tanzania, Erick Kabendera, anayetuhumiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi, ameieleza mahakama nchini humo kuwa ameanza kupelekwa hospitali.

Kabendera alionekana akiuvuta mguu wake na kuonekana kuwa kwenye maumivu wakati alipopandishwa kizimbani Septemba 12, mwaka huu na mawakili wake kuiambia mahakama kuwa mteja wao ana matatizo ya kupooza mguu wa kulia na pia kupumua kwa shida.

Leo, kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi, Kabendera amethibitisha kuwa jana Jumanne Septemba 17, 2019,  alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Amana na amefanyiwa kipimo cha X Ray kwenye mgongo pamoja na kipimo cha damu.

“Nashukuru jana nilifanikiwa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Amana na nilifanyiwa kipimo cha X Ray kwenye mgongo wangu na majibu yametoka,” amedai Kabendera.

Amesema pia alikuchukuliwa kipimo cha damu na majibu yake bado hajapewa na yanasubiriwa ili aanze matibabu.

Ameieleza mahakama kuwa bado ana maumivu makali katika mguu wake. Upande wa mashtaka umedai kuwa bado haujakamilisha upelelezi na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Kisutu, Augustine Rwizile, ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 1, 2019.

Kabendera alipandishwa kizimbani Agosti 5 mwaka huu na kusomewa mashtaka matatu ya ubadhirifu wa kiuchumi. Katika mashtaka hayo Kabendera anatuhumiwa  kujihusisha na genge la uhalifu na uhujumu wa uchumi nchini Tanzania, ambapo shtaka la pili ni la kukwepa kulipa kodi ya zaidi ya milioni mia moja sabini za Kitanzania.

Kosa la tatu ni la utakatishaji fedha zenye thamani ya zaidi ya millioni mia moja na sabini. Kwa mujibu wa mashtaka yaliyowasilishwa, Kabendera anadaiwa kuyatekeleza hayo baina ya Januari 2015 na Julai mwaka huu jijini Dar es Salaam na kwa baadhi ya makosa anadaiwa kuyafanya kwa ushirikiano wa watu ambao hawakuwepo mahakamani.

Makosa yote hayana dhamana na Kabendera anaendelea kusota rumande. Kumekuwa na ukosoaji ndani na nje ya Tanzania juu ya kesi hiyo, huku wanaharakati wakiitaka serikali ya Tanzania kufuta mashtaka dhidi ya mwanahabari huyo.

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Weka Comment Yako Hapa Chini:
Share:
Loading...

0 [disqus]:

Post a comment

Click Below to Subscribe

Loading...

Copyright © UDAKU SPECIAL BLOG | Powered by Blogger