Dar es Salaam. Mkali wa wimbo ‘Uno’ Harmonize ameingia tena katika mijadala katika mitandao nchini Kenya baada ya kudaiwa kuiba shairi la wimbo ‘Inauma’ wa Stivo Simple Boy wa nchini humo.
Kupitia video iliyopostiwa katika ukurasa wa Instagram wa Stivo akiwa na Byzzo The Baddest ambaye alimshirikisha katika wimbo huo walieleza kwa kirefu kuwa wimbo wao umeibiwa.
Katika wimbo wa Harmonize ‘Hainistui’ aliouachia katika mtandao wa YouTube Januari 3, 2020, mwishoni anasikika akiimba shairi lisemalo...Inauma lakini itabidi wazoee, shairi linalodaiwa kuwa limechukuliwa katika wimbo wao ambao waliuachia katika mtandao wa YouTube Novemba 12, 2019.
Katika shairi la wimbo wa ‘Inauma’ wa Stivo kiitiko chake kinasikika...Inauma lakini itabidi uzoee...
Hii ni mara ya pili kwa Harmonize kushutumiwa kwa mkasa wa aina hiyo. Novemba 20 , 2019 wimbo anaotamba nao hivi sasa ‘Uno’ ulilazimika kuondolewa katika mtandao wa Youtube baada mtayarishaji wa muziki nchini Kenya, Magix Enga, kudai ni mdundo wa wimbo wake wa Dundaing.
Kutokana na hilo, Novemba 17, 2019 Enga alimuomba Harmonize kuufuta wimbo huo katika mtandao huo kwa kumpa wiki moja na kuahidi kuwa asipofanya hivyo, angechukua jukumu hilo mwenyewe na hata ulipopotea alikiri kuhusika na hilo.
Hata hivyo, Novemba 25, 2019 wimbo huo umeonekana kurejea huku Enga akiwa mmoja wa watu anayeupigia debe watu wauangalie na kuusikiliza.
Jitihada za kumtafuta meneja wa Harmonize kuzungumzia sakata hilo zinaendelea.
0 Comments