NDANI YA BOKSI: Miaka minane baada ya kifo cha Kanumba, Bongo movie inahaha

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA


Wiki iliyopita nilikuwa natazama movie ya Kanumba. Ndani yake yupo Rose Ndauka, Patcho Mwamba, Ben na Seth Bosco. Wapo wengine ila siwakumbuki majina yao. Boooonge moja la movie. ‘Ofu kozi’ kuna mapungufu mengi sana lakini mapungufu yake yanavutia kuliko ubora wa movie za sasa. Ukitaka kujua kwa nini Kanumba alikuwa staa sana. Tazama movie zake akiwa hai, leo ikiwa imepita takriban miaka minane utaelewa kuwa yule mwamba alikuwa maili nyingi mbele ya wenzake wengi si kwamba alikuwa mwigizaji mkali kuliko wenzake wote, ila mfanyaji kazi bora kuliko wenzake wote. Jiulize wale aliowaacha wako wapi?

Vicent Kigosi wa kujiita ‘Ray’ najua yupo mitaa ya Sinza Mori, nisichojua ni maendeleo ya kampuni yake na Blandina wanayemuita ‘Johari’.

Kampuni ya RJ sijui kama kuna rekodi ya kulipa kodi huko TRA. Kabla ya kifo cha Kanumba, ningeweza kukutajia mpaka idadi ya filamu za RJ, tena bila kuhitaji maelezo ya Blandina, Chuchu wala kwa mdosi Dileshi pale Kariakoo. Wakati wa uhai wa Kanumba kazi zao zilikuwa wazi kama vazi la kahaba. Leo giza kama vazi la mtawa.

Ray kakosa nguvu ya kupambana? Kakosa hasimu mbadala baada ya Kanumba? Au alikuwa anabebwa na uwepo wa Kanumba? Kwa maana ile ile kuwa Simba bila Yanga haina maana? Hapana! Au filamu kwa ujumla wake zimepoteza soko? Lakini mbona wasanii bado wanavutia kwenye macho ya mashabiki kwa matukio mengine?

Tazama kurasa zao mitandaoni zilivyojaa ‘folowazi’. Wanavutiwa na sura zao kuliko kazi zao zilizowapa umaarufu? Au wanavutiwa na ‘drama’ zao nje ya sanaa? Yawezekana Ray alipata kila kitu kwenye sanaa kwa nguvu ya ‘uhasimu hewa’ na Kanumba. Kwamba hata Mlela angeweza kuwa hasimu wa Kanumba na kung’ara.

Mwigizaji JB pia alikuwa juu kiasi, majina aliyokuwa akitumia kwenye filamu zake kama Eric Ford, yalitikisa ngome ya jina lake kongwe la JB. Ubora na ukongwe wake kwenye tasnia hii uliwapa amani ya moyo mashabiki kwamba pengo la Kanumba limetoweka. JB alikuwa juu kama nguzo za treni ya SGR. Lakini leo JB kikazi amerudi miaka 20 nyuma.

Tunamuona kwenye tamthiliya tena nyakati za usiku mnene. Kitu ambacho alikifanya miaka ya 90 na kina Bishanga. Sioni jitihada za makusudi kwa miamba hii kurejesha uhai wa soko la filamu. JB na wenzake ni wepesi, mafundi na wenye vipaji mbadala vya kuhudhuria shughuli za minuso zaidi. Ni kama wameacha soko la filamu lijiendeshe kama mtoto yatima. Hakuna jipya, hakuna wapya, hakuna mpya. Wasanii wengi wa filamu wamekuwa mashabiki wa mastaa wa muziki. Utawaona kwenye shughuli za wanamuziki wakiselfika kisha kuposti insta na kuchambana na mashabiki kwenye kommenti.

Elizabeth Michael ‘Lulu’, mmoja wa wasanii ambao ni dili. Ilikuwa ukienda Kariakoo na movie ambayo kuna jina lake, wadosi walikuwa hawana muda wa kujiuliza yeyote wa kike. Leo hii yuko wapi? Ukiachana na matatizo yake ya kesi mpaka kifungo hana la kushangaza kwenye filamu tena. Licha ya ubora wake wa sura na uigizaji pia anabaki kuwa staa wa filamu nchini anayesubiria ndoa zaidi kuliko kazi zake. Suala siyo kucheza filamu, bali kupambania soko la filamu.

Kulikuwa na hofu sana baada ya akili za mastaa hawa kuanza kuongozwa na fikra za Steve Nyerere. Ndo tukafikia hapa tulipo hii leo. Duh!

Kutoa ndinga mpya mpaka pamba kwenye miili yao. Utawaambia nini? Walipamba magazeti, mitandao na majukwaa ya bendi kila mwisho wa wiki. Najaribu kuvaa uhusika wa wasanii wenzao ambao walilazimika kuwa wapambe na mashabiki wao ili wapewe shavu kwenye filamu zao. Iliwaumiza! Hata wadosi pale Kariakoo ni kama walishikiwa akili. Lakini toka mwili jumba wa Kanumba ulazwe pale Kinondoni. Na Ray akatoweka kama sauti ya Lufufu kwenye vibanda umiza.

Lulu staa wa sanaa ya uigizaji kabla ya Sinta na Johari, kabla ya Kanumba, Ray, Uwoya, Wolper na mastaa kibao unaowajua. Amekuwa staa kipindi ambacho Mondi na Kiba hawajui lolote kuhusu muziki. Kawa staa akiwa mdogo sana nyakati za za Dk Cheni na Nora. Ana nyota kali kwa matukio yake ya maisha tu.

Kwa mwingine angetoweka kisanaa muda sana. Kawa staa akiwa dogo mpaka leo akiwa katika umri sahihi wa kumuweka kwenye foleni ya kuelewa. Lakini si yeye wala wadau ambao wametumia nyota yake kurudisha hadhi ya soko la filamu. Yeye pekee ni movie tosha ya kupindua matokeo ya soko la filamu. Hawamtumii.

Watamtumiaje wakati yeye na soko lenyewe hawana muunganiko? Kila mtu anasema asemavyo juu ya kushuka kwa mizuka ya filamu zetu. Hata vipindi vya kina Zamachache kuleta siasa kwenye maisha yao. Kwa kuongea uongo juu ya biashara yao na kuiaminisha Serikali na TRA kuwa biashara ya filamu ni kubwa kama madini na gesi kama si mafuta. Kwenye vikao na Serikali waliingia na magari ya kifahari wakitanua mikono kama wana majipu ya kwapa. Unategemea nini? Mbwembwe na hesabu zao za kihayawani walizotoa kwa Serikali tofauti na hali halisi ya biashara yao. Matokeo yake ni kupangiwa makato ya kimiujiza, kodi na kila kitu tofauti na uhalisia. Mdosi akatiwa ubaya kana kwamba anachoingiza kingi na anachotoa kwenye kodi na wasanii ni kidogo. Kuna wakati kila mtu alitamani kuwa msanii. Hivi sasa kila msanii anatamani kuwa paparazi wa runinga za mtandaoni. Wenyewe wanaita ‘yutyubu chaneli’ au ‘onlaini tivii’. Usanii umeyumba kama vibendera vya waamuzi wa Ligi Kuu Bara.

Kutaka sifa na ukaribu kwa wanasiasa wa awamu hii kukawapa upofu wasanii wasijue hata unafuu wa kipato chao kwa uwepo wa wasambazaji wadosi. Waswahili kazi yao ilikuwa kuwatia ndimu wasanii kuwa wanaibiwa lakini huoni mbadala wa mdosi kabla na baada ya kuacha kusambaza. Unoko umewanokea wao. Wezi wa kazi za wasanii wapo. Tatizo kutojua yupi ni yupi na kwa vipi. Mdosi akaona isiwe tabu, kuepusha shari na malumbano akaamua kujikita kwenye dili zake nyingine. Watazame wasanii wa leo wasioibiwa na mdosi na wa wakati ule walipoibiwa. Afadhali iko wapi? Waache tu washinde ‘lokesheni’ za tamthiliya. Wasanii wetu wa sanaa zote hawajawahi kumtambua adui yao. Kujielewa.

Tunaambiwa na ndo ukweli kwamba wasanii walikuwa wanauza mpaka hakimiliki. Yaani mpaka ile ‘masta sidii’ kama siyo ‘tepu’ ni mali na urithi kwa familia ya mdosi. Yaani wanauza wazo, utendaji wao mpaka urithi wa watoto wao. Yaani mtoto wa Ray hana haki ya kurithi chochote katika kazi alizouza kwa mdosi, sasa hapo msanii anaibiwaje? Kama kuna watu wanadurufu. Anayeibiwa hapo ni mdosi au msanii? Maana msanii kishalipwa chake chote tatizo ni uelewa wao.

Sanaa imekuwa chaka la watu waliofeli kielimu na kimaisha. Kitu ambacho si jambo la afya kwa sanaa na wasanii.

Wasanii walihitaji elimu zaidi kuliko kuweka mazingira magumu kwa mdosi mpaka akaacha kazi ya usambazaji. Wasanii walihitaji elimu ya kibiashara na haki zao badala ya kuleta mazingaombwe ya kutaka kuzuia filamu za kutoka nje. Wasanii walipaswa kupewa sapoti ya mazingira rafiki kwa kazi zao. Kuliko kugawa mashabiki wao kwa siasa. Wasanii walitakiwa kupewa elimu mtambuka, wajue sanaa bila elimu ni kama kinywa bila meno.Ujuaji, sifa za kibwege kwenye mambo yanayotaka elimu. Mwisho ndo kama tunavyoona leo. Wakati zamani wasanii ungewakuta pale Leaders Club, leo utokee msiba labda ndo utawaona. Inaumiza.

Kinachofurahisha wenyewe wakihojiwa wako ‘vere komfotabo’ kana kwamba kila kitu kiko kwenye mstari. Hata hawataki kujali kuwa sanaa ni kazi na biashara ya wazi. Ikiwa vizuri kila mtu atajua. Lakini wao wanaishi kana kwamba sanaa yao wanafanyia na kuuzia Korea Kaskazini na hapa wanaishi tu. Kwa maana kuwa Wabongo hatujui linalo endelea. Ni ‘prinsipo’ kwamba ukitaka kutatua tatizo ni lazima ukubali kwanza kuwa hili ni tatizo. Lakini ukiwatazama wasanii midomo yao haitaki kukiri kuwa ni tatizo. Ila miili, macho, ngozi, mavazi mpaka makazi yao yanaonyesha hilo wazi wazi. Kuwakumbusha pia ni msaada kwao.

Mwananchi

-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad