"Iran ipo Tayari Kuzipa Nchi za Afrika Uzoefu wake wa Kukabiliana na Corona"Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kuyapa mataifa ya Afrika uzoefu wake katika suala la kupambana na ugonjwa wa COVID-19 (Corona).

Mohammad Javad Zarif amesema hayo katika ujumbe alioutuma kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwa mnasaba wa 'Siku ya Afrika' iliyoadhimishwa jana Jumatatu.

Katika ujumbe wake huo, Dakta Zarif amesema kuwa, "Pongezi kwa Siku ya Afrika 2020, siku hii inatukumbusha mapambano ya Waafrika dhidi ya dhulma. Iran imekuwa na daima itaendelea kuwa rafiki wa kutegemea wa mataifa ya Afrika."

Amesisitiza kuwa, Iran iko tayari kuzipatia nchi za bara hilo tajiriba na uzoefu wake katika uga wa kukabiliana na virusi vya corona ili kuokoa maisha.Siku kama ya jana miaka 57 iliyopita, hati ya Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) ilisainiwa mjini Addis Ababa, Ethiopia kwa kuhudhuriwa na viongozi wa nchi 32 za bara hilo; kwa lengo la kuleta umoja kati ya nchi za Afrika, kutatua hitilafu kati ya nchi hizo, kutetea haki ya kujitawala ya nchi wanachama na ukombozi wa nchi nyingine za Kiafrika zilizokuwa zingali zinakoloniwa.

Jina la jumuiya hiyo lilibadilishwa kutoka Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) na kuwa Umoja wa Afrika (AU) mnamo Julai mwaka 2002.

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO

Post a comment

0 Comments