5/29/2020

Serikali yatoa mwongozo wa kudhibiti corona Vyuoni, Shule za Msingi na SekondariMwongozo huo unaelekeza shule za msingi, sekondari, vyuo na taasisi za elimu juu ya maandalizi ya mazingira kabla ya kufunguliwa, uchunguzi wa afya, usafiri wa kwenda shuleni/vyuoni na mazingira kujifunzia. 

Unaelekeza tahadhari za kujikinga na maambukizi, huku ukiagiza wataalamu wa afya wa mikoa na halmashauri zote nchini, kufanya ukaguzi mara kwa mara wa taasisi zilizo kwenye maeneo yao, kuhakikisha tahadhari zinazingatiwa na kutoa taarifa kwenye mamlaka husika. 

Mwongozo huo ambao utaboreshwa mara kwa mara kukidhi mahitaji, umekuja wakati ambao wanafunzi wa Kidato cha Sita, vyuo na taasisi za elimu wako kwenye maandalizi ya kurejea kwenye taasisi zao kuendelea na masomo Jumatatu, baada ya Mei 20, mwaka huu, Rais Dk John Magufuli kutangaza kurejesha ratiba za masomo. 

Maandalizi ya kufungua Kulingana na mwongozo uliosainiwa na Waziri Ummy Mwalimu (pichani), shule, vyuo au taasisi zimetakiwa kutakasa mazingira yote angalau saa 72 kabla ya wanafunzi kuingia. 

Hii inahusisha taasisi ambazo zilitumika kutunza washukiwa wa Covid-19. Imeelekezwa siku ya kwanza ya kufunguliwa shule na vyuo, elimu itolewe kwa wanafunzi na wafanyakazi kuhusu ugonjwa, dalili na hatua za kujikinga na maambukizi. 

Maelekezo mengine ni kuhakikisha kwenye taasisi husika, kunakuwapo sabuni na maji titirika kwa ajili ya usafi wa mikono katika kila eneo au maeneo ya madarasa, ofisi, lango kuu, mabweni, maktaba, bwalo la chakula, vyoo na maeneo mengine muhimu. 

Wizara inasisitiza matumizi ya sabuni na maji tiririka ndiyo iwe njia kuu ya usafi wa mikono. Vile vile vifaa vya kunawa mikono vizingatie mahitaji ya wanafunzi wenye ulemavu,” alisema Ummy kupitia taarifa hiyo. 

Vitakasa mikono vinaweza kutumika kama mbadala wa maji na sabuni, ingawa wizara imesisitiza kwamba matumizi yake kwa wanafunzi ni suala la hiari. Aidha, shule/vyuo vitakavyotumia vitakasa mikono, vinatakiwa kuhakikisha vina ubora, kwa maana ya kuwa na ethenol yenye asilimia zaidi ya 70. 

Mwongozo umekataza matumizi ya spirit kama mbadala wa vitakasa mkono katika maeneo ya shule, chuo na taasisi na kutaka wanafunzi wasiagizwe na wasiruhusiwe kuingia nayo. 

Shule na vyuo vyenye wanafunzi wa bweni, vinatakiwa kuhakikisha kunakuwapo nafasi ya kutosha kati ya kitanda na kitanda, wanafunzi wasichangie vifaa kama vile taulo, mashuka, vyombo vya kuogea na vifaa vya usafi wa mwili. Imeagizwa pia wanafunzi, walimu na wafanyakazi, wahamasishwe kuvaa barakoa za vitambaa na wazazi wahimizwe kuwapatia watoto wao vifaa hivyo kabla ya kwenda. Uongozi umetakiwa kuweka utaratibu mzuri wa upatikanaji wa barakoa zilizotengeenzwa nchini, zinazoweza kufuliwa na kupigwa pasi. 

Taasisi zimetakiwa pia kuhakikisha kunakuwapo vifaa vya kuhifadhia taka, zitokanazo na barakoa zilizotumika na kuziteketeza. Uchunguzi wa afya Mwongozo umesema wanafunzi watakaohisiwa kuwa na dalili za Covid-19, watatakiwa kufanyiwa vipimo, kabla ya kurudi shuleni/ vyuoni na waliobainika kuwa na ugonjwa, watapaswa kubaki nyumbani hadi afya itakapoimarika. 

Wanafunzi watakaobainika kuwa na dalili za ugonjwa wakiwa shuleni, uongozi utatakiwa kutoa taarifa kwenye kituo cha huduma za afya kilicho karibu, kwa ajili ya uchunguzi na matibabu zaidi. Usafiri kurejea shuleni, vyuoni Wamiliki wa magari ya shule wametakiwa kuweka vitakasa mikono kwa ajili ya wanafunzi wakati wa kupanda. 

Pia wanatakiwa kuwapo wahudumu waliovaa barakoa na kutumia vitakasa mikono kabla ya kupanda gari. Mazingira ya kujifunzia Uongozi wa shule na vyuo umeagizwa kuhimiza wanafunzi, walimu na watumishi, kuzingatia kanuni za usafi binafsi ikiwamo kunawa mara kwa mara na kukaa umbali utakaokuwa salama wakati wa mafunzo. 


HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Weka Comment Yako Hapa Chini:
Share:
Loading...

0 [disqus]:

Post a comment

Click Below to Subscribe

Loading...

Copyright © UDAKU SPECIAL BLOG | Powered by Blogger