Kijana Mwenye Jinsia Mbili Apata Wakati Mgumu


KILA  anapofikiria kutangamana na watu wanaoifahamu hali yake, Sidney Etemesi huwa anaanza kuishiwa na nguvu na ujasiri hata wa kutembea au kutoka nje.

Sidney Etemesi ni Mkenya aliyezaliwa akiwa na viungo vya uzazi aina mbili, uume na uke.Maumbile yake yamekuwa changamoto kubwa katika uhusiano wake na watu wengine katika jamii. Kila siku, ameishi kukejeliwa kushoto kulia na wanaofahamu hali yake, japo si ya kujitakia.

Mwili wake Sidney umebeba viungo vya uzazi aina mbili, vya kike na vya kiume.

Lakini kwa kumwangalia tu, bila kujua hali yake ya kuzaliwa nayo, basi utamfananaisha na mtu wa kawaida tu.

Yeye huishi kama mwanamume ingawa kwa kiasi muonekano wake wa sura unaegemea upande wa wanawake.

Ni hali ambayo humchanganya Sidney kila kuchao, anapopambana na nafsi yake na kujaribu kujitambulisha kwa wengine.

“Kila siku ya maisha yangu, ninapoingia kwenye bafu nikijitazama maumbile yangu ya kuwa na uke na uume katika mwili mmoja huwa najihisi mnyonge na mwenye hofu kuu. Ila sina lakufanya,” anasema Sydney.Maisha ya utotoni

Sidney alizaliwa akitambulika kama binti au msichana, na wazazi wake wakampa jina Beatrice .

Malezi ya Sydney yalikuwa kama ya watoto wengine, kwa kuwa hali yake ya maumbile ilikuwa ni siri iliyokuwa imefichwa sana na wazazi wake.

Binafsi hakuwa na ufahamu kuwa alikuwa tofauti na watoto wengine na wala hakuwa na ufahamu kuwa maumbile ya kawaida huwa binadamu anabeba aina moja tu ya viungo vya uzazi.Lakini siku zilivyozidi kusonga mbele, alianza kujihisi ndani yake kwamba anavutiwa na kukumbatia tabia za kiume. Alianza kujitambulisha kama mtoto wa kiume na kutaka kucheza na wavulana. Lakini hapo ndipo matatizo kati yake na wazazi wake yalipoanza.

Wazazi wake hawakumuunga mkono, wala hawakutaka kusikia chochote kuhusu hisia zake. Walichofahamu ni kuwa mtoto wao alikuwa binti na hakukuwa na cha ziada.Kuvunja ungo

Matatizo zaidi yalianza pale alipoanza kubalehe akiwa na umri wa miaka 13. Mwili wake ulianza kubadilika kama wanarika wengine, japo mabadiliko yake yalianza kufanana na yale ya kiume.

“Nilichukua uamuzi wa kujitambulisha kama mwanamume kwa kuwa mwili ndiyo uliokuwa unanielekeza. Homoni za mwili wangu zilinielekeza hivyo,” Sidney alisema.Alipochukua uamuzi huo mambo yakaenda mrama zaidi. Alitengwa na hatimaye kufukuzwa nyumbani. Sydney anasema kuwa akiwa na umri wa mika 14 alianza kuishi kama kijana wa kurandaranda mitaani.

Kukimbilia mitaani

Sidney anasema haikuwa rahisi kwani hakuwa na wa kutegemea. Alianza kupitia unyanyapaa na dhuluma kutoka kwa watoto wengine mtaani.

Alibaguliwa na kuchekwa kwa kujitambulisha kama mwanamume ilhali muonekano wake wa sura ulikuwa wa kike .“Muonekano wangu bila shaka umekuwa ukiwakanganya watu sana. Sura yangu na maumbile yangu ya nje ya mwili yana muonekano wa kike zaidi. Lakini undani wangu hisia zangu na nguvu zangu nazihisi kama za kiume tangu zamani,” anasema Sydney.Kipindi cha Sydney kuishi mitaani hakikuwa kirefu kwani kwa bahati alikutana na msamaria mwema aliyemuelekeza kwa muungano wa huntha nchini Kenya.

Hapo ndipo Sidney alipopata nafasi ya kujielewa. Aidha, alikutana na watu ambao wametekwa na maumbile ambayo ni tofauti na jinsi wanavyojitambulisha.Changamoto za kuwa huntha

Sidney amekumbana na changamoto nyingi kila siku. Kwanza kabisa ni kuwa alichukua ujasiri wa kuoa kwani anasema kuwa yeye amekuwa na hisia za kupenda jinsia ya kike.

Anasema jinsia ya uume wake ndio yenye nguvu zaidi ya kike na kwa hivyo amefanikiwa kupata watoto wawili. Lakini ndoa yake imekumbwa na misukosuko.

Anasema mke wake ameikubali hali yake ya maumbile lakini upo wakati ambao mkewe hujawa na wasiwasi kumhusu mumewe.

“Hofu kuu kwangu ni kuwa mimi hupata hedhi, na huwa inaandamana na uchungu na damu nzito kuliko kawaida. ”

Kero la kutokwa na hedhi ndio mojawapo ya mahangaiko mengi katika maisha ya Sydney kwamba amejitambulisha kuwa mwanamume lakini hupata hedhi.

La pili ni kusemwa na watu na kunyanyapaliwa kutokana na muonekano wake.

“Utamsikia mtu akinieleza na kusema ‘yule mume-jike’ ”

Cha tatu ni kuwa ameshawahi kulazimishwa na watu ambao hakukubali kuwataja waliosisitiza kuwa lazima wavione viungo vyake vya uzazi.Alikataa lakini wakatumia nguvu.

“Wakati mwingi mimi huwa na huzuni sana, na huwa ninapendelea kukaa peke yangu ndani ya nyumba,” Sidney alisema.

Hatua ya kujitokeza kwa vyombo vya habari kuelezea hali yake ya kuwa huntha ilisukumwa sana na haja ya kuhamasisha jamii kuhusu uwepo wa watu kama yeye.Anasema kuwa amepitia unyanyapaa mwingi na kwa hivyo anajiona kama mtu mwenye jukumu la kutetea huntha wengine.

Kadhalika, angependa wengine wafahamu jinsi ya kuishi wakiwa huntha kwenye jamii.Hatua ya kubadilisha jina lake imekuwaje?

Sidney ameelezea kuwa katika stakabadhi zake alifaulu kubadilisha kitambulisho chake pekee ambacho kinamtambua kwa jina hilo la Sidney na wala sio Beatrice tena kama jina alilopewa na wazazi wako, lakini kwenye kitengo cha jinsia angali anatambulika kwa jinsia ya kike kutokana na cheti chake cha kuzaliwa.Ombi lake Sidney kama mmoja wa washiriki wa muungano wa Huntha nchini Kenya ni kuwa, huntha watatambulika kama jinsia aina ya kipekee na wala sio kama ya kiume au kike.

 


HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO

Post a comment

0 Comments