Mkwasa Apigwa Stop Yanga, Kisa Kipo HapaMAMBO ni moto kufuatia sakata linaloendelea ndani ya benchi la ufundi la Yanga la makocha wa timu hiyo Luc Eymael, Boniface Mkwasa na kocha wa makipa, Manyika Peter kuvurugana.

Eymael, Mkwasa na Manyika walivurugana katika mazoezi ya timu hiyo ikiwa ni siku chache kabla ya safari ya Morogoro kwenda kucheza dhidi ya Mtibwa Sugar kutokana na matokeo mabaya wanayoyapata katika mechi zao zilizopita.


Aidha Kocha Eymael aliweka wazi kuwa iwapo hatabadilishiwa viongozi waliokuwa katika benchi la ufundi alionao akiwemo Mkwasa, Manyika na wengineo wote basi ataachana na klabu hiyo kuifundisha msimu ujao.


Yanga ambayo inapambania kubaki nafasi ya pili ya msimamo wa ligi ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 68 katika mechi 36 ilizocheza ikiwa imebakisha mechi mbili ambapo watani wao Simba wakiwa tayari wameshafanikiwa kutwaa ubingwa kwa kuwa na pointi 81.


Taarifa ambazo Championi Jumatano imezipata kutoka ndani ya benchi la ufundi la Yanga zinasema kuwa, uongozi umewataka Mkwasa na Manyika kubaki Dar kutoambatana na kocha ili kuepusha mvurugano zaidi katika mechi hizi mbili zilizobakia.


“Kocha Luc Eymael walipishana kauli na wasaidizi wake Mkwasa na Manyika kutokana na matokeo yanayojitokeza katika mechi hizo za mwisho kwa kudai kuwa hapati sapoti kama anavyohitaji yeye hivyo hawakuwa na mazungumzo mazuri.


“Uongozi umetumia busara kwa kuwataka Mkwasa na Manyika wasiambatane naye katika safari ya Morogoro kwenye mechi dhidi ya Mtibwa Sugar, hivyo hadi sasa haijajulikana kama watarejea timu ikirudi ama la,” alisema mtoa taarifa huyo.


Championi Jumatano, lilimtafuta Mkwasa aweze kuzungumzia suala hilo simu yake ilikuwa bize wakati wote, lakini Makamu Mwenyekiti wa timu hiyo, Frederick Mwakalebela alisema: “Sifahamu lolote kwa sasa ndugu yangu, nipo mkoani nina matatizo ya kifamilia.”

 


HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO

Post a comment

0 Comments