Mwanamke Aliyeolewa na ndugu Wawili wa Familia Moja, Aeleza ilivyokuwaKwa kawaida ndoa inapovunjika, uhusiano kati ya mwanamke na mashemeji hukatika pia. Lakini kwa Stella Mutahi, kuvunjika kwa uhusiano wake na mumewe kulizaa uhusiano mwingine usio wa kawaida.Kaka yake mume wake aligeuka na kuwa mume wake wa pili. Ilikuwaje hadi Stella akaolewa katika familia moja mara mbili?

Mwanzo wa yote
Stella anasema alikutana na mume wake wa kwanza wakati akisomea huduma za migahawa na mapishi na hata kabla ya kumaliza masomo alikuwa na ujauzito.

Baada ya kuhitimu kutoka chuoni Kikuyu, si mbali sana na jiji la Nairobi, hakurudi nyumbani kwao ila alichukua sanduku lake la nguo na kuanza maisha na baba wa mtoto wake.

Mwanamke huyu anasema kuwa maisha hayakuwa matamu katika ndoa ile ya kwanza kwa kuwa yule mpenzi wake alikuwa na hasira za mkizi. Stella alijihisi kana kwamba maisha yake yalikuwa hatarini .

Kifungua mimba wao akiwa na umri wa miezi minane, mambo yalizidi kuwa mabaya mno kwenye ndoa.

“Nakumbuka usiku wa mwisho wa ndoa yangu ya kwanza baba wa mtoto wangu wa kwanza alianza kunigombeza tukiwa chumbani. Mara ghafla akachomoza upanga uliyokuwa unawekwa pembeni pale chumbani,” anasema.“Nilidhani kuwa alikuwa na nia ya kunimaliza ila alinyanyuka ghafla na kuelekea nje pale ambapo gari langu lilikuwa limeegeshwa. Alianza kulikatakata, huku akivunja vioo vyote kwa upanga ule.”

Ni hapo ambapo wasiwasi ulijaa moyoni mwake na akaamua kujinusuru akiwa bado ana uwezo wa kufanya hivyo.

“Palepale nilihisi maisha yangu yakiwa hatarini, na nilichoweza kutoroka nacho ni mtoto wangu. Nilipewa pa kulala na jirani hadi asubuhi,” Stella anakumbuka.

Kesho yake mwanamke huyo alichukua uamuzi wa kutoka kwenye ndoa yake na kuanza maisha upya akiwa na mwanawe wa kike.

Mwanzo wa penzi la zamani
Haikuchukua muda kwa Stella kukutana na mpenzi mwingine japo mwanadada huyu anasema kuwa yule mwanaume alikuwa anamfahamu kabla ya kuingia chuoni.

Kwa hivyo ilikuwa tu kwamba urafiki wao ulipanda ngazi na kuwa wa kimapenzi.

Baada ya mwaka mmoja, mwaka wa 1999, waliamua kuanza kuishi pamoja kama mke na mume.

Maisha ya ndoa hii kulingana na Stella yalikuwa na changamoto zake ila yeye kama mwanamke alijizatiti kuvumilia kuifanikisha.

Walifanikiwa mabinti watatu.

Stella Mutahi
Stella anasema kuwa changamoto kubwa katika ndoa yake ilikuwa kichapo cha karibu kila siku alichokuwa akikipata bila sababu.

Anasema kuwa mara nyingi mume wake alikuwa anarudi nyumbani na fujo ambazo hazikuwa zinaeleweka.

“Sikuwa ninaelewa hisia za mume wangu kwa kuwa asubuhi tukiamka alikuwa yuko sawa na mcheshi ila ifikapo jioni alikuwa anaanza kunitumia arafa za matusi na vitisho katika simu yangu ya mkononi.

“Nikizisoma hivyo tu, nilikuwa najua ningepokea kichapo cha mwaka usiku,” Stella anasema.

Na kwa kweli, mumewe aliporudi nyumbani jioni alianza kumzaba makofi na mateke bila sababu yoyote ila tu kutoa madai ya jinsi wanawake ni wabaya na kwamba wanawake ndio chanzo cha maisha yake kuharibika, anaeleza Stella.

Hakusema ni wanawake wangapi na wa wapi, ila ni swali ambalo Stella alikuwa anajiuliza kila wakati.

Kutokana na udhalilishaji huo, Stella alianza kuathirika kiakili. Watoto wake pia walimuogopa baba yao kama simba.

Akibisha jioni afunguliwe mlango, wote walikuwa wanatawanyika kama panya waliomsikia paka akiingia.

Stella anasema kuwa ni hali hiyo, pamoja na kutowajibika kwa mwanamume huyo kwa mahitaji ya nyumbani, iliyomlazimu kuanza kupanga njia ya kuondoka kwenye ndoa hiyo.

Safari ya kwenda kwa kaka wa mumewe

Stella anasema mwaka wa kumi wa ndoa hiyo ndio uliokuwa mbaya zaidi. Ilikuwa kila siku ni vita na matusi.

“Nakumbuka nikitamani nigongwe na gari. Kwa hivyo nikiwa mjini nilikuwa natembea hata katikati mwa barabara ili tu gari linigonge, angalau hata mguuni ili nilazwe hospitalini nisirejee nyumbani,” anasema.

Alikuwa akiwahurumia watoto wake, kwani alifahamu kuwa mazingira yale ya uoga na wasiwasi hayakuwafaa.

Stella Mutahi

Siku mmoja aliwachukua watoto wake na kumtembelea binamu yake. Hakuwa amepanga kwamba ile siku ingekuwa mwisho wa ndoa yake, ila aliopofika huko alihisi kabisa hana upendo wala nguvu za kurejea tena kwake.

Alihisi kana kwamba mapenzi yote na uvumilivu wote kwa mume wake ulikuwa umekwisha na kwa hivyo usiku ule hakurejea kwake .

“Usiku ule mume wangu alinitusi kila aina ya matusi. Nilimweleza kuwa nisingerudi tena kwenye ndoa na nilichokuwa nahitaji ni nguo za watoto pamoja na vitu kadhaa vya nyumba ili nianze maisha yangu upya. Hayo yote tulikuwa tunaongea kwenye simu ya mkononi,” anasema Stella.

Baada ya mwezi mmoja alimpigia mwanaume huyo simu, akiwa bado anaishi na binamu yake. Watoto walihitaji sare zao za shule kwani siku ya kufunguliwa kwa shule ilikuwa inakaribia.

“Nilipofika kule nyumbani kwangu nilikuta baba wa watoto wangu ametoa kila kitu cha nyumbani. Alikuwa ameacha nguo zangu na za watoto wangu pekee ndani ya nyumba. Hata vitanda alivihamisha,” anasema.

Katika pilika pilika za kupanga nguo zao pale nyumbani aligundua kuwa yule mumewe alikuwa amemuoa mke mwingine kutokana na kadi ya ubatizo wake iliyokuwa na maelezo hayo.

Ndoa yake iliishia hapo mwaka wa 2009 na mawasiliano kati yake na mumewe huyo yakakatika kabisa.

Kupata penzi ‘jangwani’
Ndugu yake mume wake wa pili alikuwa anawajulia hali kila wakati na akawa anamsaidia Stella na watoto wake kujikimu.

“Alikuwa rafiki wa karibu na watoto wangu walimtambua kama mjomba ambaye aliwapenda sana. Wakati huo alikuwa anatusaidia kama mjomba na shemeji yangu. Hatukuwa na uhusiano wowote wa kimapenzi,” Stella anakumbuka.

Siku moja, Stella na wanawe walifungiwa nyumba na mwenyenyumba kwa kutolipa kodi. Alipomjulisha shemeji yule yaliyotokea, aliwaalika Stella na watoto wake waishi kwake wakati anajipanga kulipa kodi.

Mke wa shemeji yake pamoja na watoto wake walikuwa wameondoka nyumbani kutokana na shida za kindoa kama ambazo zilikuwa zimemkabili Stella katika ndoa yake na baba ya watoto wake.

Stella anasema kuwa yeye akiwa anaishi huko kwa shemeji yake kulikuwa na utulivu wa kipekee na alipata amani kwa mara ya kwanza katika kipindi kirefu.

Watoto wake walikuwa wanafurahi tu na walionekana kuwa wametulia kiakili pia. Mwanamume huyo alikuwa ametulia na hakuwa mtu wa zogo.

“Mazoea yana taabu. Tulianza urafiki wa kimapenzi kule nyumbani na ikawa siri kubwa kati yangu na kaka yake mume wangu wa zamani. Nilijua kuwa nimechukua uamuzi ambao haukufaa ila nilishindwa kujizuia kumpenda kutokana na roho ya utu na utulivu wake,” Stella anasema

Lakini watu walianza kumsema na kumkejeli kwa kuamua kuolewa na kaka yake mumewe.

“Nilikuwa najua watu wananisema, nilijua pia kuwa watoto wangu hawakuwa wanafurahia uhusiano wangu na mjomba wao, ila mimi nilichukua uamuzi huo nasikutaka mtu kunikosoa wala kunipa ushauri wa yule mtu nitakayempenda,” anasema.

“Nilikuwa nimeumizwa mno kwenye ndoa za awali. Yule mwanamume alinipa utulivu na mapenzi ya kweli, nilishindwa kujizuia,” Stella anasema.

Mwanadada huyu anasema kuwa mama mkwe wake alitumani mara kadhaa aalikwe nyumbani ili wazungumzie juu ya hali ile, lakini yeye hakuwahi kufika kule nyumbani kwa mume wake kabisa.

Baba wa watoto wake , aliyekuwa mume wake kwa muda wa miaka kumi alipopokea habari kuwa ni ndugu yake ambaye amemrithi mke wake aliendelea na matusi ya kila siku kwenye simu.

Mwishowe Stella aliamua kwenda kituo cha polisi kushtaki kwa kuwa alikuwa anamtishia mno.

Stella Mutahi

Maisha ya ndoa yake hiyo yalinawiri kwa kiasi kuwa aligundua talanta yake ya kuendesha magari ya kasi na kushiriki mbio za magari za Safari Rally.

Aliwahi kuwa mmoja wa manahodha wa magari hayo kwa muda wa miaka mitatu.

Stella anasema kuwa haya yote yaliwezekana kutokana na utulivu aliokuwa anaupata ndani ya ndoa ile.

Hata hivyo, alikuwa anajihisi kana kwamba ndani ya moyo wake, yeye hakuwa kielelezo chema kuhusiana na mahusiano ya kimapenzi na ndoa kwa watoto wake ambao ni wasichana.

Stella anakiri kuwa alihisi kana kwamba hakuwa na sauti ya kutoa muongozo wa maisha kwa wasichana wake kutokana na chaguo lake.

Ni jambo ambalo lilimsumbua sana kwa miaka mingi ila kama anavyosema alikuwa anajitia hamnazo huku siku zikisonga.

Mwisho wa kosa na raha
talanta yake ya kuendesha magari ya kasi na kushiriki mbio za magari za Safari Rally
Alikuwa na talanta ya kuendesha magari ya kasi na kushiriki mbio za magari za Safari Rally
“Tukielekea mwaka wa kumi nilianza kumwambia huyu mume wangu kuwa, tulikosea kwa kuingia kwenye ndoa.

“Nilimweleza kuwa ningetaka kuondoka kwake kwa kuwa nimeharibu mno mahusiano ya kinyumbani na kutoa taswira mbaya kwa watoto wangu na wake.

“Kumbuka kuwa hatukuwa tumekosana, ila nilimpa mawazo yangu. Alikubali shingo upande. Alisema uamuzi nitakaouchukua hatakuwa na budi ila kuukubali,” Stella anasema.

Kuhusiana na hali ya watoto, Stella anaeleza kuwa licha ya kuwa hawakuwa wanamueleza aliona kuwa hisia zao zilikuwa hazipendi hali ya maisha yao.

Walikuwa pia hawana ujasiri wa kuzungumza kuhusu jamii yao kwa wenzao

“Watoto wangu hawakuwahi kumtambua huyu kaka yake baba yao kama mume au baba yao. Walikuwa hawana uhusiano naye tena ila walikuwa wanamheshimu. Waliendelea kumuita mjomba licha ya sisi kuanza kuishi naye na akiwa anawafanyia majukumu ya baba.”

Stella aliondoka kwenye ndoa ile baada ya miaka tisa na ni hatua ambayo aliichukua kwa uchungu mwingi ila alisema kuwa dhamiri yake ilimkataza kuendelea kuishi na shemeji yake kama mume.

Sasa ni mwaka wa tatu tangu kumalizika kwa ndoa hiyo.

Stella anasema amejitokeza kwenye vyombo vya habari kuomba msamaha kwa mke wa yule shemeji yake, watoto wake na pia kwa wote aliowakosea kwa kuchukua hatua ya kuolewa na ndugu wa mumewe.

Stella pia anaona mabadiliko makubwa kwa watoto wake baada ya kuondoka kwenye ndoa na mjomba wao.

Huwa anawashauri sana na anasema kuwa amepata ujasiri wa kunena mbele ya watu kwani hajihisi kama ana hatia tena.

Stella yuko katika mstari wa mbele kuwashauri wanandoa jinsi ya kuishi kwa kuvumiliana na kuzidisha upendo katika ndoa.

 


HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO

Post a comment

0 Comments