Matumizi vipodozi vyenye viambata vya sumu tishio kwa afya ya wanawake nchini Tanzania

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA



Matumizi vipodozi vyenye viambata vya sumu tishio kwa afya ya wanawake nchini Tanzania

ASILIMIA kubwa ya wanawake ambao wanaotumia vipodozi nchini wamekuwa wakipata madhara kiafya kutokana na kutumia vipodozi vyenye viambato sumu.


Wapo waliojikuta wakilazimika kutumia gharama kubwa kujitibia baada ya kupata madhara yatokanayo na vipodozi hivyo.


Kwa baadhi ya watumiaji wa vipodozi hivyo haiitajiki vipimo vya maabara kuwafahamu walioathirika wa vipodozi hivyo vyenye viambato sumu kwani wanatambulika hata kwa kuwaangalia.


Wengi waliopata madhara ya kiafya kutokana na vipodozi vyenye viambata sumu (mkorogo) wamekuwa na mvuto wanaokusudia kwa muda mfupi, lakini madhara yanayojitokeza baadaye ni makubwa ikiwepo kupoteza maisha au kutumia fedha nyingi kujitibu.


Kwa kutambua madhara hayo ya vipodozi Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ambalo limepewa jukumu la kusimamia vipodozi hivyo kupitia Mabadiliko ya Sheria ya Fedha ya Mwaka 2019 limekuja na mkakati mkali wa kuelimisha wananchi aina ya vipodozi vyenye viambato sumu vilivyopigwa marufuku kwenye soko la Tanzania ikiwa ni pamoja na kuendesha ukaguzi wa kushtukiza kwenye soko kwa lengo la kuviondoa , kutoa elimu kwa umma na kusajili vipodozi.


Kabla ya shirika hilo kukabidhiwa jukumu hilo mwaka 2019 usimamizi wa vipodozi ulikuwa chini ya iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA).


Ili kuhakikisha vipodozi vyenye viambato sumu haviendelei kutumiwa na Watanzania, TBS inawataka watumiaji wa vipodozi vilivyopigwa marufuku na wananchi kwa ujumla kuepuka matumizi ya vipodozi hivyo, kwani vina madhara ya afya kwa watumiaji.


Pia shirika hilo linawataka wafanyabiashara wa vipodozi kupeleka taarifa za vipodozi wanavyouza ikiwa ni pamoja na kuvisajili vipodozi hivyo kwa lengo la kuhakiki ubora na usalama wake., hatua itakayowasaidia kujua ni vipodozi vipi vimepigwa marufuku na vile vinavyoruhusiwa kwene soko la Tanzania.


Mratibu wa Usajili wa Majengo na Bidhaa za Chakula na Vipodozi wa TBS, Moses Mbambe, anasema vipodozi vilivyopigwa marufuku kwenye soko la Tanzania vina athari kubwa kwa watumiaji.


Kwa mujibu Mbambe miongoni mwa vipodozi vilivyopigwa marufuku nchini ni Krimu na Losheni zenye kiambato cha Hydroquinone , losheni na sabuni zenye  kiambato cha Hydroquinone Vingine ni sabuni zenye kiambato cha Zebaki (Mercury), Krimu zenye kiambato cha Zebaki na michanganyiko yake pamoja na kipodozi cha kupunguza unene chenye kiambato cha mmea (Phytolacea Spp).


 Mtaalam huyo anasema vipodozi hivyo vinavyotokana na mmea 'Arctostaphylos Uva URSI (bearberry extract) venye viambato vya "Hydroquinone na Abutin ambavyo ni sampuli zipatazo tano na vipodozi vyenye kiambato cha Tin Oxide kinachosababisha muwasho kikitumiwa karibu na eneo la macho ambavyo jumla ni sampuli sita.


Anataja vipodozi vingine ni vile vyenye  kiambato cha Malic acid, ambacho  kinachobabua cell za ngozi na kusababisha weupe, mfano Aha Whitening  Cream.


Mbambe anataja vingine kuwa ni vipodozi vya nywele vyenye kiambato cha "Apocynum Cannbium root extract, mfano African Gold Glo na vipodozi vinavyotokana na Tussilago Farfara, mfano Softn Free Hair Food.


"Vingine ni vipodozi vya kuzuia harufu (Antiperspirant) vilivyo na Aluminum Zirconium Compound mfano Triplc Dry Antiperspirant," anasema Mbambe na kuongeza;


"Vingine ni krimu zenye misuguano (Homones in Steroids), jeli zenye "Steroids" na vipodozi vingine vyenye kiambato sumu cha Hydroquinone & steroid na vingine."


Mbambe anasema mtu yeyote anaweza kujua vipodozi ambavyo havitakiwi kwenye soko la Tanzania afike kwenye ofisi za TBS makao makuu na ofisi za kanda na muda si mrefu orodha hiyo itawekwa kwenye website ya shirika.


Akizungumzia madhara ya vipodozi hivyo, Mbambe anasema vipodozi

vyenye Hexachloraphene mtumiaji akijipaka hupenya kwenye ngozi na kuingia kwenye mishipa ya fahamu hasa kichwani.


Pia anasema husababisha ugonjwa wa ngozi na kuathiri ngozi pindi mtumiaji anapokuwa kwenye mwanga na vile vile inakuwa laini na kusababisha kupata ugonjwa kama fungas au maambukizi ya vimelea vya maradhi.


Kwa vipodozi vyenye Zebaki, Mbambe anasema husababisha madhara ya

ngozi, ubongo, figo na kwenye viungo mbalimbali vya mwili.


"Zebaki inapopakwa kwenye ngozi huweza kupenya taratibu ndani ya mwili na kusababisha sumu yake kuingia kwenye damu, hivyo kuleta

madhara mengi mwilini," anasema Mbambe na kuongeza;


"Mjamzito akitumia vipodozi vyenye Zebaki mtoto huathirika akiwa bado tumboni na uzaliwa akiwa na mtindio wa ubongo."


Lakini pia anasema vipodozi hivyo husababisha ngozi kuwa laini na

yenye mabaka meusi na meupe na kwamba husababisha mzio wa ngozi na

muwasho.


Kuhusu kiambata chenye Steroids, Mbambe anasema hilo ni kundi la

homoni. "Homoni hizi hutengenezwa kwenye miili ya binadamu na wanyama, pia zinaweza kutengenezwa nje ya mwili wa binadamu

(artificial hormones) katika kundi hili. Corticosteroids ndizo hutumika sana kama viambato kwenye vipodozi," anasema Mbambe.

 

Anazidi kufafanua kwamba Steroids zikitumika kwa muda mrefu husababisha madhara mbalimbali kama ugonjwa wa ngozi na kutokwa kwa chunusi kubwa.


"Pia ngozi huwa nyembamba sana na laini na endapo itapata jereha au kufanyiwa upasuaji, kidonda hakitapona na husababisha magonjwa ya moyo,"anasema Mbambe.


Kwa upande wa vipodozi vyenye Chroloform,mtaalam huyo anasema

husababisha kansa ya utumbo mpana na kibofu cha mkojo, kusababisha

ugonjwa wa akili na ule wa mishipa ya fahamu.


Kwa mujibu wa Mbambe Chroloform husababisha ngozi kuungua, maumivu

makali, ngozi kuwa nyekundu sana na kutokwa na vipele. Akizungumzia vipodozi vyenye viambata vya Chlorofluorocarbon (Halogenated Chlorofiuoroaikanes) anasema hivyo husababisha madhara kwenye mishipa ya katikati ya fahamu na hivyo kusababisha mtu kutopumua vizuri.


"Pia husababisha kichefuchefu, kutapika, kuumwa kichwa, kusikia usingizi  na kusikia kuzunguzungu," anasema Mbambe.

Kuhusu Methylene Chloride anasema husababisha saratani, madhara kwenye mishipa ya kati ya fahamu, kwenye maini na kwenye mishipa ya moyo.


Kwa upande wa matumizi ya vipodozi vyenye kiambato cha Bithionol, Mbambe anafafanua kuwa athari zake ni kupata mzio wa

ngozi na athari kwenye ngozi ikiwa itapata mwanga kwenye jua. "Iwapo sumu itaingia kwenye mishipa ya fahamu husababisha ugonjwa wa mishipa ya fahamu na kwamba sumu ya zebaki ikiingia mwilini kwa kiwango kikubwa husababisha madhara kama upofu, uziwi na upotevu wa fahamu mara kwa mara," anasema Mbambe.


Kwa upande wa kiambata chenye Vinyl Chloride, anataja madhara yake

kuwa ni kusababisha kansa ya maini, ubongo, mapafu na mfumo wa damu.


"Sumu hii pia husababisha kuumwa kichwa, kusikia kuzunguzungu na

kupoteza fahamu,"anasema Mbambe.

 

Kuhusu Zirconium, anasema husababisha kansa ya ngozi, huku vipodozi nyenye Halogenated Salicylanilide madhara yake yakiwa ni kusababisha mzio wa ngozi mara inapopata mwanga wa jua pamoja na ugonjwa wa ngozi.


Kwa upande madhara yanayosababishwa na kiambata sumu cha Chloroquinone, Mbambe anasema; "Kundi zima la viambato Chloroquinone hutumika kutengeneza vipodozi, lakini kiambato kinatumika zaidi ni kiambato cha Hydroquinone.


Hydroquinone husababisha madhara ya muwasho wa ngozi, mzio wa ngozi, saratani, kuchubuka kwa ngozi na kusababisha mabaka meupe na meusi."


Pamoja na madhara hayo ya kiafya, Mbambe anasema kuna madhara ya

kiuchumi ambayo yanaweza kuambatana na matumizi ya vipodozi visivyo na ubora na usalama kwa watumiaji.


Anataja gharama hizo kuwa ni Wizara ya Afya kulazimika kutenga fedha nyingi kwa ajili ya ununuzi wa dawa kuwahudumia watu waliopata madhara ya vipodozi fedha ambazo zingeweza kwenda kugharimia shughuli za maendeleo ya nchi. Kupungua kwa kipato cha familia kwa sababu pesa nyingi hutumika kununua vipodozi na mikorogo, badala ya fedha hizo kutumika kwa ajili ya ustawi wa familia .


Kwa msingi huo, Mbambe anasema TBS inawashauri watumiaji wa

vipodozi na wananchi kujiepusha na matumizi ya vipodozi vilivyopigwa marufuku kwani huleta madhara kwa afya ya mtumiaji.


"Kwa hiyo ni muhimu kwa wafanyabiashara wa vipodozi kuleta taarifa za vipodozi wanavyouza TBS kwa njia ya mtandao ili kuwasaidia kujua ni aina zipi za vipodozi vilipigwa marufuku nchini na vilivyoruhusiwa," anasema.


-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad