8/14/2020

Kamati Imefunika Kombe Tu Kesi ya Morrison
NIANZE kusema kuwa Kampuni ya Global Publishers kupitia vyombo vyake vya magazeti ya Championi, Spoti Xtra na Global TV Online tunajivunia hiki ambacho kimetokea wiki mbili hizi.


Mahojiano ya winga Bernard Morrison aliyoyafanya na Saleh Ally kisha kurushwa na vyombo hivyo kwa mara ya kwanza kabisa, kisha vyombo vingine vya habari kufanya mwendelezo wake na kufikia hapo lilipofikia sasa ni jambo la kujipongeza.

Sipongezi maamuzi ya kesi husika bali uwezo wa timu ya Global kunusa harufu ya habari, mwisho kuifanya na kuanzisha mjadala ambao bila shaka umetoa somo kubwa kwa viongozi wa soka, klabu na wachezaji wengine kuhusu suala la mikataba.


FUNZO KUHUSU MIKATABA


Nikiri kuwa moja ya sehemu ambayo viongozi wengi wa soka la Tanzania wamekuwa wakifanya ubabaishaji ni katika suala la mikataba, ndiyo maana inapotokea kuna mchezaji anakuwa na uelewa mzuri au ana watu wazuri nyuma yake kwenye masuala ya kisheria huwa ni rahisi kushinda mgogoro wowote wa kimkataba.


Kwa miaka kadhaa ya hapo nyuma tumewahi kuona jinsi Emmanuel Okwi ambavyo alikuwa akizisumbua klabu zetu za Simba na Yanga katika suala la mikataba.


Mganda huyo amekuwa na watu wazuri nyuma yake wanaomuongoza kwenye masuala ya kisheria ndiyo maana aliwahi kuondoka Yanga kirahisi tu na sababu kubwa ilikuwa ni kukiukwa vipengele vya kimkataba.

KESI NI MORRISON ALISAINI AU HAKUSAINI?


Awali kabisa wakati sakata la Mghana huyo likianza Morrison alisema kuwa yeye hana mkataba wa miaka miwili na Yanga kama ambavyo klabu hiyo ilikuwa ikitangaza.


Alisema mkataba wake wa awali ulikuwa ni wa miezi sita tu, kuhusu kilichotokea baadaye ni makubaliano kuwa atasaini mkataba wa miaka miwili, lakini akasisitiza hakusaini, bali walikubaliana mambo kadhaa.


Hivyo, alipoona hakuna cha maana kinachoendelea, akaamua kubadili maamuzi ya kuhusu kusaini mkataba wa pili na Yanga, hata kesi yake aliyoenda kushitaki kwa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) ni kuwa alikuwa HANA MKATABA WA MIAKA MIWILI NA YANGA.

Kesi ya msingi ni kuwa hajasaini mkataba wa miaka mwili na Yanga, siyo kwamba alishitaki kuwa amesaini kisha Yanga wakakiuka makubaliano.


TFF kupitia Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ikatangaza kuwa Agosti 10, 2020 ndiyo itakuwa siku ya kutoa hukumu, ajabu siku hiyo ndiyo ikawa kama wameanza kusikiliza kesi husika.


Kesi kuchukua siku tatu ikaonekana kama kuna mambo makubwa ambayo yanaweza kuwa yametokea, wakati kiuhalisia ilikuwa ni suala la uhakiki wa mkataba tu upo au haupo, na kama upo kwa nini mchezaji aukane.


USIMBA VS UYANGA NDANI YA KAMATI


Hata kabla ya hukumu hiyo kutolewa, juzi katika Gazeti la Championi Jumatano niliandika kuwa mazingira ya kesi hiyo yanavyoenda kuna Usimba na Uyanga ndani ya kamati husika na kuna dalili za kutengeneza kubalansi mambo.


Hilo halina ubishi, Simba na Yanga ndizo klabu zetu kubwa na zina ushawishi mkubwa kuanzia ngazi ya chini hadi juu, hivyo maamuzi mazito ya kiweledi mara nyingi yamewahi kupindishwa kisa tu nguvu ya klabu hizo.


Katika hukumu ya juzi kupitia kwa mwenyekiti wa kamati husika, Elias Mwanjala alitoa majibu ambayo wazi yanapingana au kutoonyesha uhalisia wa kesi ya msingi ambayo Morrison aliipeleka kwao.

Hoja ya Morrison ilikuwa HANA MKATABA, lakini kwa mujibu wa kamati ni kuwa mkataba wa Yanga huo wa miaka miwili ulikuwa na mapungufu ndiyo maana Morrison ameshinda na yupo huru kujiunga na timu yoyote anayoitaka.


Hivyo, kinachoonekana hapo kamati haikuwa wazi kujibu msingi wa hoja ya kesi kuwa mkataba ulikuwepo au haukuwepo, maana mchezaji alisema hana na hajasaini, sasa kamati inaposema mkataba una mapungufu tuelewe vipi?

KAMATI IMECHEMKA KATIKA KESI YA MSINGI


Kwa mujibu wa majibu ya Mwanjala ni kuwa Morrison alidanganya kuwa hana mkataba, mwenyekiti huyo wa kamati anamaanisha mkataba uliwepo ila tu ulikuwa na mapungufu aliyoyaita ni madogo, kama hivyo ndivyo kwa nini wasimgeuzie kibao mchezaji kwa kumwambia alidanganya kuwa hana mkataba wakati alisaini.


Kamati inapokuja na hoja kuwa; ‘Mkataba una walakini kidogo, kuna karatasi zimechanwa, kuna sehemu haijasainiwa, tarehe zimekosewa….’ Bila kificho nasema ni hoja za kitoto na kamati inajua inachofanya.

Suala la mkataba kuwa na mapungufu na mkataba kutokuwepo ni vitu viwili tofauti. Kama haukuwepo maana yake kwa nini Yanga ilipeleka mkataba feki TFF na kama ulikuwepo ila ukawa na mapungufu kwa nini Morrison alisema hakuwa na mkataba!

Kwa klabu kubwa kama Yanga haiwezekani mchezaji akasaini kisha akakosa nakala au klabu ikakosa nakala ya kile kilichosainiwa.

Baadaye Mwanjala anasema kuwa Morrison aliidharau kamati kwa kusaini mkataba na klabu nyingine wakati kesi yake ikiwa inaendelea, kisheria anaposema ‘Contempt of Committee’ ni wazi kuna kosa hapo.

Kwa ufupi alichokiuka hapo Morrison ni kudharau kile kilichokuwa kikifanywa na kamati, kweli ni kosa kisheria, japokuwa katika utetezi wake anaweza kueleza kuwa hakuwa na mkataba ndiyo maana alisaini na klabu nyingine.

FILAMU ZILIKUWA NYINGI


Siku ya pili wakati kesi ikiendelea, kamati ilisema imeshindwa kutoa maamuzi kwa kuwa kuna nyaraka zimekosekana, lakini kesho yake asubuhi mwanasheria mkongwe Alex Mgongolwa akihojiwa na kituo kimoja cha redio aliulizwa kuhusu kukosekana kwa nyaraka hiyo akasema hajui chochote, na kama ipo hivyo basi mteja wake ambaye ni Yanga atawasilisha nyaraka hiyo.


 


Mgongolwa ni mmoja wa watu wa Yanga ambao walikuwa wakiifuatilia kesi hiyo kwa ukaribu, majibu yake kuhusu nyaraka yalinifanya nitafakari mara mbili kuhusu kilichokuwa kikiendelea ndani ya kamati na uhalisia wa jambo lenyewe.


 


Yote kwa yote Morrison katuonyesha kuwa kuna tatizo katika kuzingatia weledi wa maamuzi ya kamati hizi za TFF, pia ni vema wachezaji na viongozi wakaongeza umakini wao katika suala la mikataba.


HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Weka Comment Yako Hapa Chini:
Share:
Loading...

0 [disqus]:

Post a comment

Featured post

Tovuti bora zaidi ya utabiri wa Soka Tanzania inakutuza shati ya Alex Iwobi iliyotiwa sahihi.

Jiunge nasi ili uweze kuweka dau kama mtaalamu na kubeti Ligi ya England, La Liga, ikiwemo jackpot. Tunakupa habari za mpira wa miguu na ...

Click Below to Subscribe

Popular Posts

Loading...

Copyright © UDAKU SPECIAL BLOG | Powered by Blogger