8/07/2020

Kisarawe yajipanga kwa watakaofanya vurugu kwenye uchaguzi mkuuWAKATI Watanzania wakielekea katika Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 28,2020,Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani imesema haitovumilia wala haiko tayari kujaribiwa. 

Hivyo imewataka wananchi wote kwa ujumla kuwa sehemu ya kuhakikisha Wilaya hiyo inakuwa salama wakati wote kwani bila ya amani hakuna maendeleo, hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kuifanya Kisarawe inakuwa salama wakati wote. 

Hayo yamesemwa leo Agosti 6,2020 na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo wakati akifungua mafunzo ya jeshi la akiba(mgambo) kwa vijana 150 wa wilaya hiyo ambayo yatafanyika kwa kipindi cha miezi minne. 

Jokate Mwegelo amesema wananchi wote wanafahamu nchi inaelekea kwenye uchaguzi mkuu , hivyo ni kipindi ambacho Wilaya hiyo kupitia Kamati ya ulinzi na usalama imejipanga vema kwa ajili ya kufanikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu. 

"Nimekuja kufungua mafunzo haya ya jeshi la akiba , nikiamini tunakwenda kuanda vijana wazalendo kwa nchi yetu, vijana watakaokuwa tayari kuhakikisha hawashiriki kwenye matukio ya uvunjifu wa amani.Kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu huwa kuna vitendo vingi vinavyoashiria kuvura amani. 

"Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kisarawe yote iko hapa, na kwa niaba yao naomba nieleze wazi, tumejipanga, hatutakuwa tayari kujaribiwa na mtu yoyote.Hivyo ni ombi langu kwenu ninyi vijana pamoja na vijana wengine wote wa Kisarawe na wananchi kwa ujumla tuwe wamoja kwa kuifanya Kisarawe yetu kuendelelea kubaki salama,"amesema Jokate. 

Amesisitiza kuwa hawatacheka na mtu yoyote atakayefanya vurugu amani."Kipindi hiki cha uchaguzi, ni kipindi muhimu na sisi tuko vizuri na yoyote atakayejihusisha na vurugu au uvunjifu wa amani hatamvumiliwa." 

Ameomba vijana hao wanaopatiwa mafunzo hayo kuwa sehemu ya raia wema ambao wataisaidia wilaya hiyo kuwa salama na kubwa zaidi wawe sehemu ya watoa taarifa ambazo zitasaidia kudhibiti matukio ya uvunjifu wa amani na uhalifu. 

Pia amesema watakapokuwa wakirejea majumbani wakawe sehemu ya kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na kujiepusha na vitendo visivyovumulika. 

Mkuu wa Wilaya hiyo pia ametumia nafasi hiyo kueleza ni vema vijana wakahakikisha wanashiriki kikamilifu kuchagua viongozi wao kuanzia ngazi ya diwani, mbunge na Rais na hivyo kila mmoja atunze kitambulisho chake cha kupigia kura."Ni haki ya kila mwananchi kushiriki kwenye kuchagua viongozi wao kwani hiyo ni haki yao kwa mujibu wa Katiba." 

Kuhusu mafunzo hayo Mkuu wa wilaya Jokate amesema wanapaswa kuwa watiifu na na raia wema kwa kuhakikisha wanalinda rasilimali za Taifa na kwamba Taifa linawategemea huku akisisitiza ni imani yake baada ya mafunzo hayo watakuwa mfano wa kuigwa kwa jamii. 

Kuhusu utimamu wa mwili Jokate amewataka vijana hao kujiepusha na mambo ambayo yatawafanya kuzorotesha miiili yao na ni vema wakazigatia afya zao kwa kujiepusha na ngono zembe, uvutaji wa dawa za kulevya na uzembe. 

Kwa upande wake Mshauri la Akiba Wilaya ya Kisarawe Meja Mohamed Wawa amesema mafunzo hayo yalianza Julai 13 na yatarajiwa kumalizika Novemba 2 mwaka huu."Jumla ya vijana 150 wanaendelea na mafunzo haya , kati ya hao wasichana ni 62 na waliobakia ni wavulana".

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Weka Comment Yako Hapa Chini:
Share:
Loading...

0 [disqus]:

Post a comment

Click Below to Subscribe

Popular Posts

Loading...

Copyright © UDAKU SPECIAL BLOG | Powered by Blogger