8/06/2020

Majanga Yaendelea Kumwandama Mtoto Aliyeokolewa Chooni


MISUKOSUKO imeendelea kumwandama mtoto (jina linafichwa) ambaye aliopolewa kwenye shimo la choo cha Shule ya msingi Murganza iliyoko wilayani Ngara mkoani Kagera baada ya kutupwa na mama yake mzazi ambapo sasa wasamaria wema waliokuwa wamejitokeza wakihitaji kumlea, wameingia mitini.


 


Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Ngara, Musa Baragondoza amesema wasamaria wema hao wameingia mitini baada ya kugundua kuwa mtoto huyo ana tatizo kwenye ubongo ambalo limesababisha ashindwe kukaa, kutembea wala kusimama.


 


“Sababu ya wasamaria wema hao kukimbia ni baada ya ripoti ya madaktari kuthibitisha kuwa mtoto ana matatizo kwenye ubongo ambayo yamesababisha ulemavu huo kwa kuwa waliona ni mzigo ambao hauvumiliki.


 


“Mtoto huyo kwa sasa yuko kwa Belesi Mitengo, ambaye alikuwa anamuuguza wakati akiwa hospitali ya Nyamihaga akitibiwa mguu uliovunjika baada ya kutupwa kwenye tundu la choo,” alisema afisa huyo.


 


Aliongeza kuwa, licha ya Belesi kuonyesha moyo wa kumlea mtoto huyo, kwa sasa mlezi huyo amekuwa na wakati mgumu baada ya yeye pia kujifungua mtoto mwingine.


“Ifahamike kuwa, Belesi ni mke wa mtu na bado hajapata ridhaa ya familia kama mke ili aendelee kubeba jukumu hilo.


 


“Ninachokiona kwake, bado anaamini kuwa wakipatikana watu wa kusapoti matibabu ya mtoto, akapelekwa kwa madaktari bingwa, anaweza kupona.


“Hivyo, nimekaa na Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Wilaya na Mkoa, ili tuangalie uwezekano wa kumsaidia mama huyo ambaye kiukweli bado anaonyesha moyo wa kumsaidia huyo mtoto.


 


“Binafsi, natamani kupata taasisi kubwa za kutunza watoto hasa za dini, maana hiyo ndiyo ingekuwa sehemu sahihi ya mtoto huyo kuendelea kuishi.


“Lakini kutokana na Wilaya ya Ngara kuwa pembezoni mwa Mkoa wa Kagera na Tanzania, kwa ujumla naona kama itakuwa ngumu kupata taasisi imara.


 


“Hivyo, nimetoa taarifa kwa Afisa Ustawi Mkoa wa Kagera, ili anisaidie kutafuta mtandao wa kuniwezesha kupata kituo hicho,” alisema afisa huyo.


Kwa mujibu wa madaktari, tatizo alilonalo mtoto huyo, halijatokana na kitendo alichotendewa cha kutupwa kwenye shimo la choo, bali tatizo hilo huenda ndilo lililosababisha atupwe kwenye hilo shimo.


 


Baragondoza alisema, yawezekana mzazi au mlezi wake, alishindwa kumvumilia kwa kuona mtoto amekuwa mzigo, ndipo akaamua kumtupa kwenye hilo shimo kwa lengo la kumuua.


Alisema kwa mujibu wa madaktari, tatizo linalomsumbua mtoto huyo, atakuwa alizaliwa nalo au kuna makosa yalifanyika wakati anazaliwa.


 


Kwa upande wa mazoezi ya viungo, Baragondoza alisema kwa sasa anafanyishwa mazoezi pasipo na mwongozo wa mtaalam wa mazoezi tiba.


“Hapa ni kijijini, hakuna hospitali karibu, hivyo mazoezi anafanyia nyumbani chini ya usimamizi wa mlezi wake, ndiyo maana tunatafuta mtu wa kutusaidia kwa kuwa hakuna anachofanyiwa cha kitaalam,” alisema afisa huyo.


 


Kwa upande wake Belesi ambaye anamlea mtoto huyo, alisema msaada wa hali na mali unahitajika ili kumfanya mtoto huyo aendelee kuishi kwa furaha kama walivyo wengine.


“Changamoto


aliyonayo huyo mtoto ni kwamba, hawezi kukaa wala kusimama.


 


“Nikimkalisha kichwa kinainama au kurudi nyuma, ukiachana na hiyo, ni mtoto mtulivu hata wakati nikiwa ninamnyonyesha, mdogo wake (mtoto niliyejifungua) anatulia.


“Kuhusu chakula, anakula vizuri, anapenda kula wali, ugali, ila hapendi kula ndizi,” alisema Belesi.


 


Awali Belesi alijitolea kumlea mtoto huyo wakati akiwa hospitali kwa matarajio ya kuwa, watapatikana wazazi wake na kumchukua, lakini amejikuta akiendelea kumlea hata baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini alikokuwa anatibiwa mguu uliovunjika baada ya kutupwa kwenye shimo la choo.


 


Siku chache baada ya kuokolewa kijasiri kwenye shimo la choo, familia sita ziliandika barua Ustawi wa Jamii wilayani humo zikihitaji kumlea, lakini cha kushangaza zote zimejiweka kando na mtoto huyo.


 


Kwa upande wake Daktari wa tiba ya watoto kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera, Dr Musa Ndyeshobora, alisema hali ya mtoto huyo inaweza kumkuta mtoto yeyote, kinachotakiwa baada ya kugundulika kwa tatizo hilo, anatakiwa kuhudhuria kliniki ya mazoezi ya viungo vya mwili.


 


“Ni ugonjwa ambao unawapata watoto, unatokana na virusi vya ‘Rota Virus’ hivyo watoto wanapararaizi sana sehemu ya miguu ambayo inalegea na kushindwa kutembea, serikali imeweka njia ya kuweza kuwasaidia kuwapima ambapo wanapelekwa Dar es Salaam kwa ajili ya kuwatambua, lakini kunakuwa hakuna dawa tena ya kumsaidia aweze kutembea, ila anatakiwa aendelee kupata mazoezi madogo ili aweze kukomaa viungo.


 


Mtoto huyo wa kike mwenye umri unaokadiriwa kuwa ni mwaka mmoja na nusu, aliokolewa na askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wilayani Ngara, Denis Minja, Mei 21 mwaka huu kwa kushirikiana na wananchi wa kata ya Murganza baada ya kupata taarifa kuwa ametupwa kwenye shimo lenye urefu wa futi 30 la choo ya shule hiyo.

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Weka Comment Yako Hapa Chini:
Share:
Loading...

0 [disqus]:

Post a comment

Featured post

Tovuti bora zaidi ya utabiri wa Soka Tanzania inakutuza shati ya Alex Iwobi iliyotiwa sahihi.

Jiunge nasi ili uweze kuweka dau kama mtaalamu na kubeti Ligi ya England, La Liga, ikiwemo jackpot. Tunakupa habari za mpira wa miguu na ...

Click Below to Subscribe

Popular Posts

Loading...

Copyright © UDAKU SPECIAL BLOG | Powered by Blogger