8/27/2020

MAMBO Muhimu ya Kuzingatia Katika Malezi Na Makuzi Ya Mtoto..!!!


Malezi ni matendo yote yanayofanywa na wazazi, walezi na jamii kwa lengo la kumlea, kumkuza, kumlinda, kumuendeleza mtoto kimwili, kiakili, kijamii, kihisia na kimaadili ili aweze kuishi, kukua vizuri na kukubalika na jamii.

Ili mtoto aweze kukua katika misingi hiyo muhimu yapo mambo muhimu ambayo wazazi wanapaswa kuyazingatia wakati wote wa malezi na makuzi. Mambo hayo ni pamoja na:

Afya

Ili mtoto awe na afya bora, anahitaji kupatiwa kinga zote dhidi ya maradhi ya kuambukiza kwa njia ya chanjo na kupatiwa tiba mara anapougua. Magonjwa sugu kama Kisukari, Pumu au Saratani  yanaweza kuathiri makuzi na maendeleo ya mtoto.

Mazingira yanayomzunguka mtoto hayana budi kuwa katika hali ya usafi na usalama wakati wote. Mazingira hayo ni pamoja na mahali anapolala, sehemu anazochezea, mavazi na vyombo anavyotumia. Inashauriwa kuwa wazazi, walezi na jamii wahakikishe watoto wadogo ikiwa ni pamoja na wale walio katika mazingira magumu zaidi wanapata chanjo kwa wakati na wanawasaidia kuweka mazingira yao katika hali ya usafi.

Ikiwa mtoto wako ana ugonjwa sugu ni busara kuzungumza na mtaalamu wa afya ili kuweza kufahamu ni jinsi gani ugonjwa huo utaathiri afya ya mtoto wako na namna bora ya kumrinda.

Lishe

Ili mtoto aweze kukua vizuri kimwili na kiakili anahitaji chakula bora au mlo kamili. Chakula bora au mlo kamili unajumuisha vyakula vyenye virutubisho kama protini, wanga, mafuta, vitamini na madini.

Chakula bora hakina budi kianze kwa mama mjamzito, mara baada ya mtoto kuzaliwa apatiwe maziwa ya mama pekee kwa miezi 6 ya kwanza, baada ya miezi hiyo mtoto apatiwe vyakula vya kulizika. Mtoto aendelee kunyonyeshwa maziwa ya mama hadi miezi 24 na kumpatia vyakula vya nyongeza.

Ni muhimu mtoto aliye na umri chini ya miaka mitano apate milo isiyopungua mitano kwa siku na yenye virutubisho vya kutosha. Inashauriwa virutubisho hivyo vitokane na vyakula vinavyozalishwa katika maeneo anayoishi mtoto.

Maandalizi ya vyakula vya mtoto yafanyike kwa makini ili visipoteze viini lishe kwa mfano, ukoboaji wa nafaka mfano mahindi, kuloweka nafaka na upikaji wa mboga za majani kupita kiasi ni sababu zinazochangia uharibifu wa viini lishe na ubora halisi wa chakula. Hali hii husababisha utoaji wa lishe duni kwa mtoto na hivyo kuathiri ukuaji na uchangamshi kwa mtoto.

Wakati wa kutayarisha chakula, kila kundi la chakula liwepo katika mlo kamili. Kimsingi, kuna makundi makuu manne ya vyakula. Kundi la kwanza ni chakula Kikuu mfano nafaka mahindi, 
mtama, mizizi (mihogo). Kundi la pili ni vyakula vyenye Utomwili mfano nyama, samaki, maharage, kunde, mbaazi, Kundi la tatu ni vyakula vyenye vitamini na madini kwa wingi mfano matunda na mboga za majani na kundi la nne ni vyakula vyenye nishati kwa wingi mfano mafuta ya kupikia na sukari.

Uchangamshi

Uchangamshi ni matendo au mwelekeo anaoonyesha mzazi au mlezi kwa mtoto kwa lengo la kuchochea ukuaji na maendeleo ya mtoto kimwili, kiakili, kimaono, kihisia na kimaadili ambapo uchangamshi wa mtoto huanza tangu akiwa tumboni kwa mama na kuendelezwa baada ya kuzaliwa.
Uchangamshi katika kipindi hiki huchangiwa kwa kiwango kikubwa na hali ya afya ya mama. Hivyo malezi na uchangamshi wa awali kwa mtoto unatakiwa uanze mara mimba inapotunga.

Mama mjamzito anahitaji matunzo kimwili, kijamii na kisaikolojia ili mtoto aliyeko tumboni aweze kukua katika mazingira salama. Ili kuhakikisha kuwa mtoto anapata malezi changamshi akiwa tumboni wazazi au walezi hawana budi kuzingatia mambo kama mjamzito kupata mahitaji ya lazima, asifanye kazi nzito na ngumu, apewe upendo, apate muda wa kupumzika, mahali pazuri pa kulala, 
ahudhurie kliniki pamoja na kupata matibabu na ushauri wa kitaalamu.

Inashauriwa mama mjamzito kutojihusisha na ulevi wa pombe, madawa ya kulevya, uvutaji wa sigara na vile vile kujiepusha na magonjwa ya kuambukiza.

Uangalizi

Uangalizi unajumuisha vitendo vitakavyowezesha kuhakikisha kuwa mtoto yuko katika hali ya usalama ili kulinda uhai na maendeleo ya mtoto. Vitendo hivyo vinajumuisha kumpatia mtoto mahitaji muhimu kama vile chakula chenye virutubisho vyote, chanjo dhidi ya magonjwa na tiba mara anapougua, ulinzi na usalama, kumpakata, kuzungumza naye na kucheza nae.

Hivyo inashauriwa kuwa ni vyema mtoto apewe uangalizi wa kutosha ili kumwepusha na ajali na mazingira hatarishi yatakayopelekea kuathiri afya yake, kupata ajali au kufanyiwa vitendo viovu kwa mfano kubakwa.

Ujirani na Jamii inayozunguka

Majirani na jamii inayokuzunguka vina mchango katika malezi na makuzi ya mtoto wako. Ukuaji na maendeleo mazuri ya mtoto yanachagizwa na mahusiano mazuri na watoto wenzake, walimu wake na watu wengine wanaomzunguka.

Lakini vitu kama ufinyu wa makazi, matunzo mabaya ya mtoto au sehemu isiyo salama kwa mtoto kuchezea au kukaa vinazorotesha ukuaji na maendeleo ya mtoto.
HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Weka Comment Yako Hapa Chini:
Share:
Loading...

0 [disqus]:

Post a comment

Featured post

Tovuti bora zaidi ya utabiri wa Soka Tanzania inakutuza shati ya Alex Iwobi iliyotiwa sahihi.

Jiunge nasi ili uweze kuweka dau kama mtaalamu na kubeti Ligi ya England, La Liga, ikiwemo jackpot. Tunakupa habari za mpira wa miguu na ...

Click Below to Subscribe

Popular Posts

Loading...

Copyright © UDAKU SPECIAL BLOG | Powered by Blogger