8/17/2020

Mr. Kuku Kufikishwa Kortini, A-Z Sakata Zima Kumbe Liko Hivi!


NI vilio tupu, ndivyo vimetawala miongoni mwa Watanzania waliowekeza katika Kampuni ya Mr Kuku Farmers Ltd ambayo inamiliki mradi wa ufugaji kuku wa kisasa Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Vilio hivyo vimetokana na hatua ambayo serikali imeichukua baada ya kumfi kisha mahakamani, mkurugenzi wa kampuni hiyo ambaye pia ni mfanyabiashara na mkazi wa Oysterbay jijini Dar es Salaam, Tariq Machibya mwenye miaka (29) kwa tuhuma za uhujumu uchumi.

Machibya maarufu kama ‘Mr Kuku’, alifi kishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mapema wiki hii akikabiliwa na mashtaka saba. Mshtakiwa huyo alisomewa mashtaka yake Agosti 10 mwaka huu na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Godfrey Isaya.


Akisoma hati ya mashtaka, Wakili Wankyo alidai mshtakiwa anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 60/2020 ambapo katika mashtaka hayo saba yanayomkabili mshtakiwa huyo, yapo ya kusimamia na kuendesha biashara haramu ya upatu; kupokea maingizo ya fedha kutoka kwa umma bila kuwa na leseni na mashtaka matano ni kutakatisha fedha.

Miongoni mwa mashtaka hayo ni kati ya Januari 2018 na Mei 2020, katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, mshtakiwa anadaiwa kusimamia biashara ya upatu.

Pia alidaiwa kujihusisha na biashara ya upatu kwa kukubali na kukusanya fedha kutoka kwa umma, akijifanya kwamba watafanya ujasiriamali wa ufugaji wa kuku na wangepata faida ya asilimia 70 ya mtaji wa awali waliowekeza kwa miezi minne na asilimia 90 ya mtaji wa awali waliowekeza kwa kipindi cha miezi sita, kiasi ambacho ni kikubwa katika biashara kuliko mtaji, uliokusanywa.

Wankyo alidai kati ya April 26, 2019 na Januari 26, 2020 maeneo ya Jiji la Dar es Salaam, alijihusisha na miamala ya Sh 6.4 bilioni kwa kutoa fedha hizo kutoka katika akaunti inayosomeka kwa jina la Mr Kuku Farmers Ltd iliyopo katika benki ya CRDB, wakati akijua kuwa fedha hizo ni zao tangulizi la biashara haramu ya upatu.

Upande wa mashtaka umedai kuwa, kesi ni ya uhujumu uchumi na upelelezi katika shauri hilo haujakamilika na Hakimu Isaya ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 24, mwaka huu.

PICHA LILILOANZA

 Wakati Mr. Kuku akiendelea kuvuna fedha kutoka kwa wananchi waliowekeza kwenye kampuni hiyo, ilibainika kuwa Serikali ilianza kufanya uchunguzi kuanzia Aprili mwaka huu na kusababisha taarifa mbalimbali kuanza kuvuja. Kutokana na hali hiyo, Mr. Kuku alijitokeza hadharani kupitia kwenye chanel yake ya YouTube ambayo huwekwa shuhuda mbalimbali za wawekezaji hao, na kueleza hali kampuni inayopitia. Pamoja na mambo mengine, alieleza kuwa akaunti za kampuni hiyo zimefungwa, hivyo kusababisha wawekezaji waliowekeza fedha zao kwenye kampuni hiyo kutopata magawio yao kwa muda muafaka.

“Tupo katika kipindi cha uchunguzi, kwamba tunafanyiwa upelelezi kuhusu shughuli tunazofanya kwa sababu mtaji unaowezesha kuku kuishi na biashara kuendeshwa, haitoki kwenye akaunti ya Mr. Kuku, bali unatoka kwa mtu mmoja mmoja. Serikali ipo katika kujihakikisha kwamba pesa zipo mahali salama,” alisema Aprili mwaka huu.

 “Tulianza na kuku chini ya 300, lakini sasa tuna kuku zaidi ya 200,000, na mradi huu upo katika eneo la hekari 34 ilhali ni mradi ambao una thamani ya zaidi ya Sh bilioni 1.5,” alisema Mr. Kuku kupitia chaneli hiyo ya Mr Kuku Farms Limited.
Licha ya kuwaondolea hofu wawekezaji hao kutokana na akaunti hizo kufungwa, sasa hali imezidi kuwa tete baada ya kufi kishwa mahamakamani wiki hii. NI VILIO Aidha, wakati hali ikiendelea hivyo mahakamani, upande wa pili wananchi waliowekeza katika mradi huo, sasa wameanza kukumbwa na wasiwasi na kubainisha hofu yao kuhusu usalama wa fedha zao.

Baadhi ya wananchi waliowekeza kwenye mradi huo ambao pia wamejitambulisha kupitia chaneli hiyo ya YouTube, ni Baraka Kipasura ambaye alisema alianza na mtaji wa Sh milioni saba kwa kuwekeza kuku 1000 ambazo baada ya miezi minne alipata fedha mara mbili yaani milioni 14.

Baraka ambaye Aprili alidai kuwa amefi kisha mtaji wa Sh milioni 26.6 anadaiwa kuwa na mtaji wa Sh milioni 52 kwa mujibu wa taaifa zake.

 “Mara ya kwanza sikuamini aliponipa mchanganuo wa mradi huo, lakini alipendelea kunisumbua, ndipo nikafanya uamuzi baada ya kutembelea mradi na kupata viashiria vya kumuamini,” alisema.
Aidha, mwingine ni Nunu Ally Fakame ambaye naye alidai kuanza mwaka 2019 kwa kuwekeza kiasi cha Sh 70,000 lakini mpaka kufi kia Aprili, tayari alikuwa na mtaji wa Sh milioni 1.1.


 “Mwanangu aliona hilo wazo, akanipa namba nikapiga simu na nikaenda kuangalia eneo la mradi na kujiridhisha, ilibidi nitafakari kwa sababu suala la uwekezaji ni gumu kwa sababu ya uaminifu. Nikaona na kuridhika, ndipo nikaamua kuwekeza,” alisema.
Mwingine ni Palvin Magnus ambaye alidai kuwa alianza kuwekeza tangu mwaka 2018 kwa kuweka mtaji wa Sh 350,000 na hadi Aprili mwaka huu, alikuwa na mtaji wa Sh milioni 16. Wawekezaji hao wameeleza hofu yao dhidi ya fedha hizo hasa ikizingatiwa tangu uchunguzi uanze Aprili mwaka huu, akaunti za kampuni hiyo zilifungwa.

Wakizungumza na AMANI kwa sharti la kutotajwa majini, baadhi ya wawekezaji hao, waliiomba Serikali kuwaangalia kwa jicho la huruma hususani fedha walizowekeza kwa sababu wao walidhani biashara hiyo ya upatu ni halali.

 Aidha, mchambuzi wa masuala ya ujasiriamali na uchumi, Kessy Juma kupitia andiko lake, alifafanua kuwa kwanza Watanzania wanapaswa kutambua kuwa upatu sio shughuli halali kisheria. ‘Ni shuhuli ya kutajirika kwa haraka’ inayoweza kukuingiza hasara kubwa sana,” alisema.

Alionya kuwa ndugu na mara kadhaa marafi ki wamegombana, ndugu kukwaruzana, mahusiano kuvunjika kutokana na upotevu wa pesa zilizosababishwa na upatu, hivyo Watanzania wanatakiwa kuwa makini na uwekezaji wa fedha zao kabla ya kufanya uamuzi.

Stori: Mwandishi Wetu, Amani
HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Weka Comment Yako Hapa Chini:
Share:
Loading...

0 [disqus]:

Post a comment

Click Below to Subscribe

Popular Posts

Loading...

Copyright © UDAKU SPECIAL BLOG | Powered by Blogger