8/09/2020

Mwalimu Nyerere Alivyomsotesha BEN Mkapa Shambani...KITABU "My Life, My Purpose" - "Maisha Yangu, Kusudi Langu", cha Rais wa Tatu wa Tanzania, Benjamin Mkapa, kina mengi. Mengi sana.

Mzee wetu Benja wa Lupaso ameshalala usingizi wa dawamu. Hata hivyo, si vibaya kudurusu yale aliyotuachia kupitia kitabu chake.

Ukurasa wa 70, kuna sura ya saba. "My First Steps on My Political Journey" - "Hatua Zangu za Mwanzo kwenye Siasa". Benja anasimulia uteuzi uliofanywa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1974.

Ndio, Mwalimu Nyerere alimteua Benja kuwa Ofisa Habari wa Rais. Kabla ya hapo, Benja alikuwa Mhariri Mtendaji wa Daily News. Magazeti ya Serikali.

Ferdinand Ruhinda, aliyepata kuwa msaidizi wa Benja, ndiye aliteuliwa kuwa Mhariri Mtendaji wa Daily News. Hivyo, Benja akamkabidhi Ruhinda ofisi.

Baada ya makabidhiano ya ofisi ya Daily News, Benja akajikuta hana kazi ya kufanya. Aliteuliwa kuwa Ofisa Habari wa Rais, lakini Rais, Mwalimu Nyerere, hakuwepo Dar. Alikuwa zake Butiama.

Benja akawaza afanyeje? Kukaa na kusubiri sio mtindo wake wa ufanyaji kazi. Akaona bora amfuate Mwalimu Butiama. Alipofika Butiama, alikuta Mwalimu Nyerere yupo shamba.

Mwalimu alipomuona Benja, akamwambia: "Ben, umekuja kuripoti kazini? Karibu!" Baada ya hapo Mwalimu aliendelea kulima kwa jembe la mkono.

Hata ungekuwa wewe, bosi wako akiwa analima, utasimama pembeni kumtazama? Thubutu! Benja akawaza, akaomba jembe ili na yeye ashiriki kilimo.

Kilichofuata, Benja alijikuta analima kwa saa tatu mfululizo. Benja anasema ilikuwa kazi ngumu mno kwake kwa sababu alizoea ofisini. Anasema, haikuishia siku hiyo, bali kila siku asubuhi, kwa siku walizokuwepo Butiama na Mwalimu Nyerere, waliamkia shamba.

Kwa msisitizo; Benja anasema, hivyo ndivyo alivyoanza kazi ya Uofisa Habari wa Rais. Shambani na msoto wa jembe la mkono.

Ni stori ya Baba wa Taifa. Na urais wake, lakini alitenga muda wa kwenda kijijini kulima. Sio kutuma, alilima mwenyewe. Nitajie anayeweza kufanya hivyo.

Hawa wa siku hizi, akishakuwa Rais, anajiona kawa bosi wa taifa. Anaanzaje kushika jembe?

Endelea kupumzika Mjamaa. Mwalimu Nyerere. Baba wa Taifa.

Lala salama Big Ben. Benja wa Lupaso.

Ndimi Luqman MALOTO
HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Weka Comment Yako Hapa Chini:
Share:
Loading...

0 [disqus]:

Post a comment

Click Below to Subscribe

Popular Posts

Loading...

Copyright © UDAKU SPECIAL BLOG | Powered by Blogger