Waziri Mkuu Aweka Jiwe La Msingi Kiwanda Cha Samani Ruangwa

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA



WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa rai kwa wawekezaji wachangamkie fursa zilizopo nchini kwa kuangalia maeneo mazuri ya kufanya uwekezaji mpya au kupanua uwekezaji wao.


Ametoa rai hiyo leo (Jumapili, Agosti 16, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa Namichiga, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi, waliohudhuria uwekaji wa jiwe la msingi kwenye kiwanda cha samani cha Saw Mill and Furniture Processing Industry na kisha kukagua eneo la ujenzi wa kiwanda cha kubangua korosho wilayani humo.


Waziri Mkuu amesema hicho ni kiwanda cha kwanza kujengwa Ruangwa hivyo amewataka wakazi wa Namkonjera na vijiji vya jirani wapime ardhi yao ili watu wanunue viwanja na kuanza kujenga.


“Kujengwa kwa kiwanda cha kutengeneza samani na baadaye kiwanda cha kubangua korosho, kutahamasisha uzalishaji wa mazao ya kilimo na misitu pamoja na kuimarisha mnyororo wake wa thamani. Endapo mtajipanga vizuri kwa kujenga viwanda vya kuongeza thamani kwenye zao la korosho, wilaya hii itakuwa kinara kwenye uzalishaji wa zao hilo,” amesema.


“Kwa upande wa viwanda, tusiishie tu kwenye korosho, tuone pia namna ya kuwa na viwanda vya kuchakata ufuta, mbaazi na mazao mengine yanalimwa kwa wingi kwenye maeneo yetu ili kijihakikishia soko na upatikanaji wa ajira.”


Amesema uwekezaji huo unaofanyika sasa, unakwenda sambamba na azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuanzisha na kuendeleza viwanda ili kukuza uchumi, kuleta maendeleo endelevu, kuongeza ajira na kupunguza umaskini kwa Watanzania wote.


Akifafanua kuhusu ujenzi wa viwanda nchini kote, Waziri Mkuu amesema kuimarika kwa uzalishaji hususan kupitia ujenzi wa viwanda, kumekuwa chachu ya upatikanaji wa huduma hususan kufuatia kuimarika kwa mapato ya Serikali na kutengeneza ajira kwa Watanzania.


Amesema katika kipindi cha miaka mitano, Serikali imefanikiwa kuimarisha sekta za kiuchumi na uzalishaji ikiwemo viwanda na biashara. “Katika kipindi hicho jumla ya viwanda vipya 8,477 vimejengwa na kuchangia kuzalisha ajira mpya 482,601,” amesema.


Akizungumzia mchango wa sekta ya viwanda katika pato la Taifa, Waziri Mkuu amesema sekta hiyo imeendelea kukua mwaka hadi mwaka ambapo kwa mwaka 2019 ilikua kwa asilimia 8.5 ikilinganishwa na asilimia 8.05 mwaka 2018, sawa na ongezeko la asilimia 0.45.


“Mchango huo unakwenda sambamba na kuimarika kwa uzalishaji wa bidhaa za viwandani. Kwa mfano, mwaka 2019 bidhaa za viwanda zilikuwa na thamani ya shilingi trilioni 10.2 ikilinganishwa na shilingi trilioni 9.6 mwaka 2018 sawa na ukuaji wa asilimia 5.8,” amesema.


“Maendeleo ya uwekezaji katika sekta ya viwanda tunayoyashuhudia hivi sasa hapa nchini, yameongeza uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zikiwemo za chuma, saruji, vigae, nguo na mavazi, ngozi na bidhaa za ngozi, kusindika nyama, chakula, mbogamboga na matunda, maziwa, mafuta ya kula, sukari, vifungashio, mbolea, dawa za binadamu, sabuni na sigara pamoja na ubanguaji wa korosho.  


Mapema, Naibu Waziri wa Kilimo, Bw. Omar Mgumba alisema uwekaji wa jiwe la msingi Katika kiwanda hicho cha kutengeneza samani, ni matokeo ya msisitizo wa Rais Dkt. John Magufuli na usimamizi wa karibu wa Waziri Mkuu mwenyewe kama sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM.


Alisema Serikali imepania kuongeza uzalishaji wa zao la korosho ifikapo mwaka 2025. “Wenye viwanda vyote vya korosho, nawahakikishieni kwamba tutakuwa na malighafi za kutosha, tumepanga kuongeza uzalishaji kutokatani 300,000 hadi tani milioni moja ifikapo mwaka 2025,” alisema.


Naye Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Bw. Hashim Mgandilwa alisema anawashukuru na kuwapongeza Orascom kwa uamuzi wao wa kujenga kiwanda cha samani na cha kubangua korosho kwani utakuwa na manufaa ya kiuchumi na kielimu.


“Ninawakumbusha wawekezaji hawa waweke kipaumbele katika kurudisha sehemu ya mapato yao kwa jamii,” alisisitza.


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho, Bw. Magira M. Masegesa alisema kiwanda hicho kinamilikiwa na kampuni ya wazawa ya Orascom Construction and Engineering Company (T) Ltd ikishirikiana na kampuni tanzu ya Yukos Entreprises yenye makao makuu jijini Dar es Salaam na kimeajiri wafanyakazi 150 ambao wanatengeneza samani zenye ubora kwa bei nafuu.


“Jumla ya shilingi bilioni 5 zimewekezwa katika kiwanda hiki kwenye awamu ya kwanza na zinahusisha ununuzi wa malighafi, mitambo ya kisasa ya kuvuna, kupakia na kupakua malighafi porini, kuchakata magogo na kutengeneza samani kiwandani. Kiwanda hiki kina uwezo wa kuchakata magogo yenye ujazo wa mita 10,000 kwa mwaka,” alisema.


Amesema kiwanda cha ubanguaji wa korosho kinachotarajiwa kujengwa, nacho pia kitawekezwa sh. bilioni 5 zikiwa ni mtaji katika awamu ya kwanza.


(mwisho)

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,


-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad