Haijawahi Kutokea! Zuchu Aweka Rekodi ya Ajabu WCB

 


ANAWAKERA eeeh? Mchawi wa Zuhura Othman Soud almaarufu ‘Zuchu’ si mwingine, bali ni namba ambazo zinamfanya aweke rekodi ya ajabu kwenye Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) Bongo.

 

Uchunguzi wa Gazeti la IJUMAA WIKIENDA kwenye mitandao ya kusikiliza, kutazama, kuuza na kununua muziki, umeonesha kwamba, haijapata kutokea kwa lebo hiyo, kwa msanii wake kutamba kwa namba 8,2,1,0 kama ilivyotokea kwa Zuchu.

 

Mbali na Zuchu kutamba kwa namba hizo Kibongobongo, nje ya nchi nako ameonekana kuwa moto wa kuotea mbali, ambapo amevuna namba 1×4, 10, 17, 20 na 46. Hata hivyo, namba 1×3 aliyopata msanii huyo wa kike mwenye umri mdogo nchini, ndiyo iliyoshangaza wengi, ambapo kwa historia ya muziki wa Bongo Fleva, haijapata kutokea msanii yeyote kufika kiwango hicho cha mafanikio.

 

8,2,1,0 NI NINI?


Kwa mujibu wa takwimu sahihi kutoka Mtandao wa Boomplay ambao unajihusisha na kazi za wasanii duniani, hasa muziki, kwa mwezi Septemba, mwaka huu, wasanii wa WCB ndiyo waliofanikiwa kushika kumi bora kwa nyimbo zao kusikilizwa na wengi.

 

Hata hivyo, rekodi ya siku 18 tu za mwezi huo, zimeonesha kati ya wasanii wote wa WCB waliotamba, Zuchu ameingiza nyimbo 8 kati ya 10. Nyimbo hizo ni; Litawachoma (1), Cheche (2), Nisamehe (4), Wana (5), Raha (6), Kwaru (8), Hakuna Kulala (9) na Ashua (10) huku mbili zilizobaki akiwaachia wenzake.

 

Namba 2 ambayo inapatikana kwenye takwimu hapo juu, ni ya ‘bosi kubwa’ wa WCB, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, ambaye jina lake limeonekana mara mbili kwenye nyimbo za Litawachoma na Cheche, ambazo alishirikishwa na Zuchu.

 

Namba 2, ni nyimbo mbili za msnii Mbwana Yusuf Kilungi ‘Mbosso’ uitwao Sina Nyota ulioshika namba 3 kwenye orodha ya Boomplay kisha Ashua akiwa na Zuchu ukiwa kwenye namba 10. Moja nyingine inakwenda kwa wasanii wengine wa WCB, RJ The Dj na mwenzake Abdul Iddi ‘Lava Lava’, ambao walifanikiwa kupenyeza wimbo wao wa Sexy Mama kwenye listi hiyo.

 

Wasanii wengine wawili wa WCB, Raymond Mwakyusa ‘Rayvanny’ na Mwanahawa Abdul ‘Queen Darleen’ waliambulia sifuri kwenye chati hiyo tamu ya Boomplay na hivyo kuhitimisha namba 0, kwenye rekodi hizo.

 

UCHAMBUZI WA NAMBA 1×4, 10, 17, 20 na 46


Ukweli kuwa namba huwa haziongopi, upo palepale kwamba, mbali na Zuchu kuitikisa rekodi ya Boomplay Bongo, kwenye mtandao mwingine wa kijamii wa YouTube ambao ‘hudili’ na video mbalimbali duniani, nako ameweka rekodi ya kipekee kupitia video ya wimbo wake wa Cheche.

 

Mbali na video hiyo kuwa namba moja Bongo, imeweza kushika namba hiyo kwenye nchi nyingine ambazo ni Uganda na Kenya, hivyo kumpa Zuchu alama 1×4 kwa wakati mmoja. Aidha, video hiyo imeweza kushika namba 10 katika nchi za Falme za Kiarabu, namba 17 nchini Afrika Kusini, namba 20 Saudi Arabia na kubamba nafasi ya 46 nchini Uingereza.

 

UFAFANUZI WA 1×3 KWA KINA


Rekodi nyingine ya ajabu ambayo imewashangaza wengi aliyoweka Zuchu kwenye Mtandao wa YouTube, ni kuweza kushika namba 3 za juu kwenye listi ya nyimbo zinazo-trendi kwa wakati mmoja. Msanii huyo ameweza kupenyeza nyimbo zake za Litawachoma (audio) kuwa namba moja, Cheche (video) kushika namba mbili na Cheche (audio) kukamata namba tatu.

 

Uchunguzi wa Gazeti la IJUMAA WIKIENDA unaonesha kwamba, hakuna msanii yeyote Bongo aliyewahi kuachia ngoma tatu kwa wakati mmoja na kukamata ‘TOP 3’ ya Mtandao wa YouTube tangu mtandao huo uruhusu jambo hilo kufanyika.

 

ZUCHU AKATA NGEBE ZA MBOSSO, RAYVANNY


Uchunguzi unaonesha kuwa, tangu Lebo ya Wasafi ianzishwe, hakuna msanii wa kike aliyewahi kutikisa kwa mafanikio kama Zuchu kiasi cha kuwafanya wasanii wa kiume kwenye lebo hiyo ‘kushika adabu’.

 

Ni wazi kuwa Mbosso, Rayvanny na Lava Lava ambao ni wasanii wa kiume kutoka WCB, kwa sasa hawafurukuti kwenye rekodi za Zuchu, kwani kati yao hakuna hata msanii mmoja aliyewahi kumshirikisha bosi wao ambaye ni Mondi kwenye nyimbo mbili mfululizo na kuziweka kileleni kwenye mitandao ya kijamii.

 

Inaweza kuwa jambo la kukera kidogo ikisemwa kuwa, kwenye lebo ya WCB ukimtoa nguli wa Bongo Fleva, Mondi ambaye ndiye Baba Lao, anayefuatia kuitekenya mioyo ya wapenda muziki wa kizazi kipya kwa sasa ni Zuchu, au uongo?

 

ZUCHU KILA KONA


Kutokana na makali ya muziki ambao msanii huyo ameyaonesha kwa kipindi kifupi tangu asajiliwe WCB, wengi wamemtabiria makubwa Zuchu kiasi cha kumbatiza jina la malkia mpya wa Bongo Fleva. Uchunguzi uliofanywa na IJUMAA WIKIENDA kwenye mitandao ya kijamii umeonesha kuwa, msanii huyo amekuwa gumzo kila kona.

 

“Huyo mtoto anajua.” “Ni malkia anayechukua kiti cha Lady Jaydee.” “Anajua hadi anakera.” Hizi ni baadhi ya komenti ambazo IJUMAA WIKIENDA limezikusanya kutoka kweye Mtandao wa YouTube ambako ngoma za msanii huyo zinawaka kama moto wa petroli.


STORI: RICHARD MANYOTA, DAR  

 


HABARI HIZI ZINAPATIKANA  KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO BURE