Kauli ya Tundu Lissu kuhusu lugha ya KiingerezaMgombea wa Kiti cha Urais kupitia CHADEMA Tundu Lissu, amesema kuwa endapo atatakiwa atoe maoni yake kuhusu Watanzania kuzungumza lugha ya Kiingereza yeye atasema, Tanzania siyo nchi ya kuzungumza lugha hiyo kwa kuwa wengi hawakijui na hakuna sera rasmi ya lugha hiyo.


Lissu ametoa kauli hiyo hii leo Septemba 9, 2020, wakati akizungumza na Wahariri pamoja na Waandishi wa Habari nyumbani kwake na kusema kuwa kama nchi inataka watu wake wazungumze lugha hiyo ipasavyo, basi Walimu wajengewe misingi mizuri ya lugha hiyo ili waweze kuwalisha watoto chakula kilicho chema.


“Ni aibu watu hawajui Kiingereza, ukienda kwenye Mikutano ya Kimataifa huko Mtanzania akizungumza utatamani uingie chini ya uvungu wa Meza, siyo kwa sababu sisi hatuna akili ni kwa sababu hatujawahi kuwa na sera rasmi ya lugha ya kufundishia”, amesema Lissu.


“Kama tunataka kila mtu azungumze kiingereza kama inavyotakiwa, fikiria Walimu wakielewa Kiingereza sawasawa siyo hiki cha kuchapia halafu wawaeleweshe watoto wetu, ukiniuliza nitasema sisi hatuwezi kuwa nchi inayozungumza Kiingereza”, ameongeza.


Akizungumzia mwenendo wa mikutano ya kampeni ndani ya chama hicho, Lissu amesema kuwa chama hicho kitaanza rasmi kufanya kampeni ya Jimbo kwa Jimbo kuanzia kesho Septemba 10, 2020.

 


HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO

Post a comment

0 Comments