9/25/2020

Mamlaka za Urusi zakamata jengo, akaunti za NavalnyImeelezwa kuwa mamlaka za Urusi zilikamata jengo la Alexei Navalny lililoko mjini Moscow pamoja na kuzishikilia akaunti zake wakati akiwa bado hajitambui na akiendelea na matibabu baada ya kudaiwa kulishwa sumu.


Taarifa hii ni kulingana na msemaji wake Kira Yarmysh aliyelihusisha tukio hilo na tajiri mmoja mwenye mahusiano na ikulu ya Kremlin. 


Navalny ambaye ni mkosoaji mkubwa wa rais wa Urusi Vladimir Putin aliruhusiwa kutoka katika hospitali alikokuwa amelazwa mjini Berlin mapema wiki hii, ambako alikuwa anatibiwa kile ambacho mamlaka za Ujerumani zinasema kilikuwa ni sumu inayoua mishipa.


Kiongozi huyo wa upinzani nchini Urusi alianguka na kupoteza fahamu akiwa kwenye ndege inayofanya safari za ndani nchini Urusi Agosti 20 na kukaa karibu wiki tatu akiwa kwenye mashine za kumsaidia kupumua.


Maafisa wa mahakama nchini humo walitangaza kuzikamata hisa za jengo lake la mjini Moscow wiki moja baada ya kuugua, amesema Yarmysh kwenye taarifa aliyoitoa kwa njia ya video jana Alhamisi. Amesema, hiyo inamaanisha kwamba jengo hilo haliwezi kuuzwa, kutolewa kama zawadi ama kuwekwa rehani. Kulingana na msemaji huyo, hatua hiyo ilichukuliwa Agosti 27, ambapo pia akaunti za Navalny zilizuiwa.


Msemaji wa Navalny, Kira Yarmysh asema tukio hilo linahusiana na tajiri huyo mwenye mahusiano na rais Putin.


Amesema, kushikiliwa kwa akaunti hizo kulihusishwa na agizo la mahakama lililoipendelea kampuni ya kusambaza chakula shuleni inayoripotiwa kuwa na mahusiano na Yevgeny Prigozhin, anayetajwa kuwa na mahusiano na rais wa Urusi, Vladimr Putin yaliyosababisha hata kupewa jina la utani "mpishi wa Putin".


Prigozhin alikuwa ni mmoja ya Warusi walioshitakiwa rasmi na jopo la majaji wa Marekani katika uchunguzi uliofanywa na mshauri maalumu Robert Muller, akidaiwa kufadhili jumbe za intaneti zilizohusishwa na kuingilia uchaguzi wa urais wa mwaka 2016 nchini Marekani.


Mwaka jana mahakama mjini Moscow iliagiza Navalvy na washirika wake kulipa dola milini 1.1 kama fidia kwa kampuni hiyo inayodaiwa kuwa na mahusiano na Prigozhin baada ya kuishutumu kusambaza chakula kilichoharibika kwenye shule moja ya watoto wadogo mjini humo na kusababisha mlipuko wa maradhi ya kuharisha miongoni mwa watoto hao.


Tajiri Yevgeny Prigozhin akimtembeza rais Vladimir Putin kwenye kiwanda chake kilichoko nje ya mji wa St. Petesburg mwaka 2010.


Msemaji wa Prigozhin hata hivyo amekana kuwepo na mahusiano yoyote na kampuni hiyo na si mahakama wala shule ambao waliweza kutolea ufafanuzi wa haraka taarifa hizo.


Navalny ameendelea kusalia mjini Berlin akiendelea na matibabu baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini, lakini washirika wake wamesema anapanga kurudi Urusi. Timu ya Navalny inailaumu Kremlin kwa tukio hilo la sumu, madai ambayo maafisa wanayapuuzilia mbali.


Mamlaka, zilishinikiza kuanzisha uchunguzi wa kihalifu huku zikiilaumu Ujerumani kwa kushindwa kuzishirikisha idara za kisheria za Urusi matokeo ya uchunguzi na taarifa za kitabibu. Ujerumani imesisitiza kwamba madaktari wa Urusi wana sampuli zao kutoka kwa Navalny tangu alipokuwa chini ya uangalizi wao kwa masaa 48 kabla ya kusafirishwa na kupelekwa Berlin kwa ajili ya matibabu.


Navalny pamoja na washirika wake kwa muda mrefu wamekuwa mwiba kwa upande wa rais Putin, kwa kuratibu maandamano makubwa mjini Moscow mwaka 2019 na kuchapisha video mara kwa mara wakiwatuhumu wanasiasa maarufu nchini humo kwa ufisadi.


Wafuasi wake wanasema mashitaka na ukamataji unaofanywa na polisi wakimlenga Navalny mwenyewe na wakfu wake ni sehemu tu ya kampeni iliyopangwa ya kudhoofisha shughuli zao.HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Share:
Loading...

0 Blogger:

Post a comment

Loading...

Popular Posts

Copyright © UDAKU SPECIAL BLOG | Powered by Blogger