Shigongo: Nitakuwa Mbunge wa TaifaMGOMBEA ubunge wa Jimbo la Buchosa mkoani Mwanza, Eric Shigongo amesema akishinda hatakuwa mbunge wa jimbo hilo pekee bali atakuwa mwakilishi wa taifa zima.


Shigongo ameyasema hayo leo (Jumanne) alipofanya mazungumzo na mwandishi wetu kwa njia ya simu na kuomba wananchi wamuamini kumpa nafasi hiyo.


“Nagombea Buchosa, lakini kwangu hii ni nafasi ya kuwa mwakilishi wa wananchi wote nchi nzima hasa vijana, akina mama na watu masikini.


“Najua makali ya umasikini kwa sababu nimetoka familia masikini, ndiyo maana natamani kuwa msaada kwa watu wa hali ya chini.

“Shabaha yangu ni kuhakikisha harakati za kuwakomboa vijana wa nchi hii kifikra na kimapato zinaendelea hasa baada ya kushinda ubunge.


“Nimekuwa nafanya kazi ya kubadilisha mitazamo ya vijana nikiwa sina cheo chochote, leo nikiwa mbunge naona nitakuwa na sauti kubwa zaidi ya nilivyokuwa zamani,” alisema Shigongo.

Aliongeza kuwa katika maisha yake ameteswa na umasikini kwa miaka mingi lakini baadaye alifanikiwa, hivyo anataka kuona vijana wengine hapa nchini nao wanafanikiwa kupitia vipawa walivyopewa na Mungu.


“Nilipoanza safari ya kusaka mafanikio sikuwa msomi, sikuwa na fedha nyingi lakini nilikuwa na kipawa nilichopewa na Mungu, nilikitumia hicho nikafanikiwa.

“Kama mimi nimefanikiwa kwa nini vijana wasomi wanaolalamika hawana ajira nao wasifanikiwe kupitia vipaji vyao?


“Kwa nini wanawake masikini wasifanikiwe katika taifa hili, nawasihi wana Buchosa waniamini, Watanzania waniombee ili nia yangu ya kuhakikisha uchumi wa nchi unamilikiwa na vijana wazalendo inafanikiwa,” alisema Shigongo.

Shigongo kupitia makampuni ya Global Group amekuwa akisaidia watu masikini, kupandikiza ari kwa vijana wajiajiri kupitia fursa zilizopo nchini sambamba na kutoa mikopo kupitia taasisi ya fedha iliyo chini yake ya Wezesha Mzawa.

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO

Post a comment

0 Comments