9/04/2020

Simulizi Mwalimu Kuuawa Kikatili InasikitishaSIMULIZI ya Mwalimu wa Shule ya Msingi Chalantai, Kata ya Chala, wilayani Nkasi mkoani Rukwa, Tabitha Mwanyanje (29) aliyeuawa kwa kuchomwa kisu shingoni na maeneo mengine mwilini, inasikitisha.


 


Mtuhumiwa mkuu wa mauaji hayo kwa taarifa za kipolisi, ni mume wa mwanamke huyo aliyejulikana kwa jina la Frank Garimoshi (30), huku kisa cha mauaji kikitajwa kuwa ni wivu wa mapenzi. Inaelezwa na vyanzo mbalimbali kuwa, wawili hao walianza visa vya kutoelewana muda mrefu, baada ya mume kumtuhumu mkewe kuwa anachepuka na wanaume wengine.


 


JIRANI ASIMULIA


Akifanya mahojiano na mwandishi wetu, mmoja wa majirani wa wanandoa hao; Safina Kambeu, alidai kuwa katika siku za hivi karibuni, wanandoa hao walikuwa na mgogoro wa mara kwa mara uliohusishwa na wivu wa kimapenzi.


 


Alisema, ‘mchepuko’ aliyedaiwa kumpa wakati mgumu marehemu kwa mumewe hafahamiki, lakini Garimoshi anadaiwa mara kadhaa kuandaa mtego wa kumnasa mkewe akiwa kwenye mchepuko, bila mafanikio.


 


Jirani huyo aliongeza kuwa, baada ya patashika ya muda mrefu kwa wanandoa hao, alishangaa juzikati kusikia mwanamke ameuawa kwa kuchomwa na kisu shingoni na maeneo mbalimbali ya mwilini, jambo ambalo limewasikitisha wengi.


 


HUYU HAPA KIONGOZI WA KIJIJI


Mmoja wa viongozi wa vijiji katika kata hiyo ambaye ni mstaafu, anayejishughulisha na usimamizi wa kanisa la Kipentekosti ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema alipata taarifa ya mauaji ya mwanamke huyo na kufika eneo la tukio haraka.


“Tulifika wengi eneo la tukio na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa, ambaye naye alikuwa kwenye harakati za kujitoa uhai, kwani alikuwa amejijeruhi kwa kisu mwilini.


“Vijana wengi sasa hivi wamemsahau Mungu, unawezaje kumtuhumu mkeo kuchepuka bila ushahidi, kibaya zaidi unaamua kumuua,” alisikitika kiongozi huyo na kuwasihi watu wawe na hofu ya Mungu, kwani kuua ni dhambi na ukatili kwa binadamu.


 


KAMANDA AELEZA CHANZO


Akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari, Kamanda wa Polisi Mkoa Rukwa, Justin Masejo alisema kuwa, tukio hilo limetokea Agosti 25, mwaka huu majira ya saa 10 alfajiri baada ya kuzuka mgogoro katika familia hiyo.


Kamanda alisema, wanandoa hao walianza ugomvi baada ya mwanamke kupokea meseji kwenye simu yake ya mkononi ikionesha kuwa, amepokea fedha kupitia mtandao mmoja wa simu.


“Baada ya mwanamke huyo ambaye kwa sasa ni marehemu kupokea meseji hiyo ya muamala wa fedha, mwanaume alianza kumtuhumu mkewe kuwa, fedha hizo ametumiwa na hawara yake.


“Majibizano yalipozidi, ndipo mtuhumiwa anadaiwa kuchukua kisu na kuanza kumshambulia mkewe, hadi kumtoa uhai.


“Baada ya mwanaume huyo kubaini kuwa amemuua mkewe, naye alianza kujijeruhi kwa lengo la kujiua, lakini hakufanikiwa na sasa amekamatwa na amepelekwa hospitalini kwa matibabu na akipona, atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma za mauaji zinazomkabili,” alisema Kamanda.


 


Aliongeza kwa kuiasa jamii kupenda kusuluhisha migogoro inayotokea kwenye familia kwa kufuata sheria na hata ikibidi, kuwatumia viongozi wa dini na madawati ya jinsia ili kuepukana na madhara.


 


MJADALA MITANDAONI


Aidha, baada ya tukio hilo la mwalimu kuuawa kinyama kuenea kwenye mitandao ya kijamii, kumeibua gumzo na simanzi nzito, hasa miongoni mwa wanawake ambao wengi wamelalama matukio kama hayo kukithiri katika siku za hivi karibuni.


“Jamani wanaume mtatumaliza, mtu kutumiwa fedha ndiyo unamkatakata visu mwili mzima hadi kumuua?”


“Mi naona ipo haja ya jamii kuelimishwa kuhusu migogoro ya ndoa, kusema kweli amani hakuna. Tusidanganyane, ndoa nyingi zimekuwa ndoano.”


“Juzi kuna mwanaume Kimara (jijini Dar es Salaam), alikamatwa kwa kudaiwa kumuua mkewe, machozi hayajakauka mwingine tena anauawa, serikali inatakiwa kulichukulia serious suala la mauaji ya wanandoa, kuna tatizo linachipuka taratibu.”


Baadhi ya komenti zilisomeka kwenye mitandao ya kijamii ambazo zilionesha kuwa, walioshiriki mjadala huo, wengi ni wanawake.


HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Share:
Loading...

0 Blogger:

Post a comment

Loading...

Popular Posts

Copyright © UDAKU SPECIAL BLOG | Powered by Blogger