Waziri wa Ulinzi wa Afrika Kusini akatwa mshahara kwa matumizi ya ndege ya jeshiRais wa Afrika Kusini amemkata mshahara waziri wa ulinzi kwa miezi mitatu baada ya kuruhusu maafisa wa chama tawala kusafari kwa kutumia ndege ya jeshi hadi nchini Zimbambwe pamoja naye Septemba 9.
Nosiviwe Mapisa-Nqakula alishtumiwa kwa kuruhusu matumizi ya rasilimali ya taifa kwa sababu za siasa za chama.


Jeshi la nchi hiyo lilikuwa limeeleza kwamba waziri huyo alikuwa katika ziara rasmi ya kitaifa na kwamba aliwafanyia abiria wengine hisani kwa kuwabeba.


Lakini Rais Cyril Ramaphosa aliitaja hatua hiyo kama makosa.


Bi. Mapisa-Nqakula alienda mji mkuu wa Zimbambwe, Harare kuhudhuria mkutano uliokuwa umepangwa kujadili masuala ya kanda.


Ujumbe kutoka chama tawala cha Afrika Kusini – African National Congress (ANC) – ulikuwa unahudhuria mkutano huo kwa mazungumzo ya dharura na chama tawala cha Zimbambwe Zanu-PF lengo lao likiwa ni kutatua mgogoro wa kisiasa na kiuchumi nchini humo.


 


Lakini wanasiasa wa upinzani walimkosoa vikali waziri huyo kwa sababu hakuendana na ujumbe wa chama cha ANC.


Bwana Ramaphosa, ambaye kipindi anaingia madarakani aliahidi kumaliza sifa mbaya ya chama cha ANC baada ya mwongo mmoja wa kashfa za ufisadi, alisema kwamba “kwa kuungana na wajumbe wa ANC kwenya ndege aliyaokuwa anatumia, hakufanya uamuzi stahiki unaozingatia uongozi mzuri”.


Matokeo yake, alisema ameamua kumkata mshahara Bi. Mapisa-Nqakula na pesa hizo zitaelekezwa katika mfuko wa kusaidia kukabiliana na janga la corona.


Wakati huo huo, chama cha upinzani cha Democratic Alliance kilisema hatua iliyochukuliwa na Bwana Ramaphosa haitoshi.


Suala hilo huenda likajadiliwa zaidi bungeni huku kukiwa na wito wa waziri huyo kufutwa kazi.

 


HABARI HIZI ZINAPATIKANA  KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO BURE