Watano Familia Moja Waliokufa Dar Wazikwa BuchosaWATU watano wa familia moja akiwemo mama, watoto wake watatu na wifi yake, waliopoteza maisha baada ya nyumba yao kuwaka moto majira ya saa nne usiku wa kuamkia Oktoba 14, mwaka huu katika eneo la Pugu CCM Kirumba jijini Dar es Salaam wameagwa leo na kuzikwa nyumbani kwao katika Kijiji cha Sukuma, Kata ya Bukokwa, Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema mkoani Mwanza.


 


Simanzi na majonzi vimetawala wakati wa kuaga miili ya ndugu hao walioacha huzuni kubwa huku mamia ya watu wakishiriki maziko hayo.
Aidha, mgombea ubunge wa Jimbo la Buchosa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Eric Shigongo, amesitisha kampeni zake kwa leo na kuamua kuungana na familia hiyo  na waombolezaji kuwafariji wafiwa na kuwapa pole.


 


Baba wa familia hiyo, Edward Katemi, amesema moto huo ulianza majira ya saa nne usiku huku chanzo kikitajwa kuwa ni hitilafu ya umeme. Waliofariki katika familia hiyo ni mke wake, Jackline Frank, mdogo wake Ester Katemi na watoto wake Edwin Katemi, Edson Katemi  na Evon Katemi.
Katemi mesema kwa kushirikiana na majirani zake walipambana kuiokoa familia yake bila mafanikio kutokana na ukosefu wa vifaa vya kuwezesha uokoaji katika tukio hilo na waliwasiliana na watu wa kikosi cha uokoaji lakini walichelewa kufika kutokana na changamoto ya usafiri iliyokuwepo pamoja na mvua kubwa
“Chanzo ni shoti ya umeme iliyopelekea nyumba yangu kuungua, madhara yaliyotokea ni mke wangu kipenzi, mdogo wangu pamoja na wanangu watatu wameniacha, chanzo ni umeme ulikatika tangu asubuhi, uliporudi ukakatika tena, nahisi uliporudi tena ulikuja kwa kasi zaidi,” ameeleza Katemi.


 


“Tulijaribu kila njia ya kuwaokoa lakini ilishindikana kwa sababu tulikuwa sisi tu na wananchi kadhaa, tuliwasiliana na ‘Fire’ lakini wakashindwa kufika, baadaye tuliweza kubomoa ukuta na tukaanza kuwatoa lakini bahati mbaya walikuwa wamezidiwa na tulipowapeleka hospitali wakawa wamefariki,” amesimulia Katemi.

 


HABARI HIZI ZINAPATIKANA  KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO BURE