11/04/2020

Giza Nene Latanda Upinzani

 


WAKATI Watanzania wakikaa chini na kutafakari mustakabali wa siasa nchini katika kipindi cha miaka mitano ijayo, giza nene limetanda kwa upande wa vyama vya upinzani baada ya kutokea anguko la kihistoria katika uchaguzi mkuu uliofanyika wiki iliyopita.

 

IJUMAA wikienda linachambua. Katika uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 28 nchi nzima, huku upande wa Zanzibar ukifanyika kwa muda wa siku mbili (Oktoba 27-28), umeshuhudia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikikwapua viti 256 vya ubunge, huku vyama vya upinzani vikiambulia viti nane pekee kati ya viti 264.

 

Aidha, kwa upande wa urais, vivyo hivyo CCM imechukua nafasi za pande zote ambapo kwa upande wa Tanzania, Dk. John Magufuli alishinda kwa kupata kura milioni 12.5 kati ya kura milioni 15.9 zilizopigwa.

  

Mgombea wa Chadema, Tundu Lissu alipata kura milioni 1.9 na kufuatiwa na mgombea wa ACT Wazalendo, Bernard Membe aliyepata kura 81,129. Kwa upande wa Zanzibar, CCM kupitia Dk. Hussein Mwinyi iliibuka na ushindi kwa kuvuna kura 380,042 sawa na asilimia 76.27 na kufuatiwa na aliyekuwa mgombea wa ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad aliyepata kura 99,103 sawa na asilimia 19.87.

MAANDAMANO

Mojawapo ya kete ambayo vyama hivyo vinaitegemea ni kufanyika kwa maandamano nchi nzima ili kushinikiza kurudiwa kwa uchaguzi mkuu jambo ambalo wachambuzi wa siasa wanaona ni gumu kufanyika.

Viongozi wakuu wa vyama vya upinzani Chadema na ACT Wazalendo, walitoa tamko kuhusu uchaguzi huo ambapo pamoja na mambo mengine walitaka kuvunjwa kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi -NEC na ile ya Zanzibar- ZEC. ‘’Kuanzia Jumatatu (jana), wanachama wa vyama vyetu na wote wasiokubaliana na uchaguzi huu, kushiriki katika maandamano ya amani kuanzia Novemba 2 hadi hapo madai yetu yakapotekelezwa’’ walisema.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Deus Kibamba alisema maandamano sio suluhu ya changamoto zilizojitokeza katika uchaguzi huo.

“Viongozi hawa wanatakiwa kukaa chini na kutafakari nini cha kufanya kwa sababu uchaguzi umekwishafanyika. Wajipange kukusanya ushahidi ili kwenda kuwatetea wagombea wao waliopoteza majimbo na kata. Kwa sababu sheria inawaruhusu na kesi hizo ndani ya mwaka mmoja mahakama inakuwa imeshatolea uamuzi.

“Kwa upande wa urais wao wenyewe walikuwa bungeni lakini walishindwa kutetea hoja ili matokeo ya urais pia yaweze kupingwa mahakamani, lakini sasa kuyapinga kwa kufanya maandamano hawatafanikiwa zaidi wananchi watavunjwa miguu na wengine kupoteza maisha bure bila sababu za msingi,” alisema.

MABADILIKO

Licha ya kwamba hili ndio jambo la msingi linalotarajiwa na wengi kutekelezwa na viongozi wa vyama hivyo vya upinzani, bado kwao ni giza nene katika kuhakikisha wanafanya mabadiliko yatakayowawezesha kupiga hatua kisiasa.

Katika hili Kibamba alisema viongozi wa vyama vyote vya upinzani nchini wanatakiwa kukutana na kuamua kusimamisha mgombea mmoja katika kila nafasi kwa sababu chaguzi ndogo nyingi zitafuata hivi karibuni.

“Haiwezekani upinzani usimamishe wagombea urais 15, na Zanzibar wasimame 16… alafu utegemee wataishinda CCM, hilo ni jambo ambalo haliwezekani,” alisema.

Aidha, mabadiliko hayo yanaendelea kuwa giza nene kwa upande wa upinzani hasa ikizingatiwa kuwa wanahitaji kuibua upya na kutetea hoja kuhusu mabadiliko ya Katiba ambayo yatawawezesha kutimiza lengo la kutengeneza tume huru za uchaguzi kwa upande wa Zanzibar na Tanzania.


“Lakini sasa hawana wabunge bungeni ambao wanaweza kuibua hoja na kupigia kelele suala hilo, wanabaki kuwa wanasiasa nje ya bunge ilihali katazo la kufanya siasa linaweza kuendelea na kuwanyima fursa kabisa ya kusikika,” aliongeza Kibamba.


Hoja hiyo iliungwa mkono pia na Mchambuzi mwingine wa masuala ya siasa, Mpoki Buyah ambaye alisema ili mabadiliko hayo yafanikiwe, vyama hivyo viwekeze kwa vijana.


Alisema inakadiriwa kati ya watanzania milioni 25 hawakupiga kura mwaka huu kwa sababu ya kuwa na umri chini ya miaka 18, lakini wanaweza kushawishiwa kupiga kura katika uchaguzi ujao na kufanya mabadiliko.

“Nasema hivyo kwa sababu tafi ti zinaonesha kundi la vijana hupenda mabadiliko wakati kundi la wazee hupendelea kuendelea na kile kilichozoeleka.


“Kwa hiyo iwapo wapinzani wataweza kubuni sera na mipango ambayo itafanya kundi hili kubwa la wapiga kura kuvutiwa nao, bado kutakuwa na uwezekano wa kuibuka na kufanya vizuri kwenye miaka ijayo,” alisema.

RUZUKU

Ukata ndani ya vyama hivi vya upinzani kihunzi kingine ambacho kinaibua giza nene katika kuelekea kwenye mabadiliko ya kisiasa.

Hatua hiyo inatokana na ukweli kwamba katika uchaguzi wa mwaka huu ukata ulisababisha wagombea wa upinzani kutokuwa na mabango kokote huku wengine wakishindwa kufanya kampeni katika baadhi ya mikoa.

Hata hivyo, kutokana na uchache wa wabunge wanaokwenda bungeni, mathalani wa upande wa Chadema, wanaweza kuwa wabunge wawili pekee hali ambayo itazidisha ukata ndani ya chama hicho.

Awali chama hicho ambacho katika uchaguzi wa mwaka 2015 kilikuwa na wabunge zaidi ya 70, kinadaiwa kuwa kilikuwa kinapokea ruzuku zaidi ya Sh milioni 300 kwa mwezi pamoja na michango ya wabunge hao zaidi ya Sh 500,00 kila mwezi

Hata hivyo, fedha hizo hazikutosha kuendesha chama na hata kukiwezesha kutunishiana misuli na CCM chenye vitega uchumi kila kona ya nchi.

Kutokana na hali hiyo, kupungua kwa ruzuku kunaweza kusababisha chama hicho kikuu cha upinzani nchini kuzidi kupata wakati mgumu wa kusimama hasa ikizingatiwa siasa za nyakati hizi zinalazimu wagombea kutumia gharama kubwa katika chaguzi.


STORI: GABRIEL MUSHI, DAR

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Share:

0 [disqus]:

Post a Comment

Popular Posts

Copyright © UDAKU SPECIAL BLOG | Powered by Blogger