Kisukari Tishio Kuliko Ukimwi
WAKATI Ukimwi ukiwa ni moja ya magonjwa yanayoogopwa na watu wengi duniani, imebainika kuwa ugonjwa wa kisukari ndio unaoua watu wengi zaidi duniani ikiwemo Tanzania. Ongezeko la ugonjwa huo ni mara 150 kila mwaka. UWAZI linakuchambulia.

 

Ukweli huo unathibitishwa na ripoti ya Shirika la Kimataifa la Kisukari Duniani (IDF) iliyotolewa Septemba mwaka jana, pamoja na ripoti Shirika la Umoja wa Mataifa linalopambana na Ukimwi (UNAIDS) iliyotolewa Juni mwaka huu ambazo zimedhihirisha namna ugonjwa wa kisukari ulivyo tishio hususani katika nchi zenye kipato cha chini na kipato cha kati cha chini.

 

HALI YA UGONJWA WA KISUKARI, UKIMWI DUNIANI

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Shirika la Kisukari Duniani (IDF), ugonjwa wa kisukari ulisababisha vifo vya watu milioni nne mwaka 2017, hata hivyo kwa wastani kila mwaka watu milioni 1.7 duniani hufariki dunia kutokana na ugonjwa huo.

 

Wakati hali ikiwa hivyo, Ripoti ya Shirika hilo la UNAIDS, inaonesha kuwa watu 690,000 pekee hupoteza maisha duniani kutokana na Ukimwi ambao unasababishwa na Virusi Vya Ukimwi (VVU).

 

Aidha, ongezeko la tatizo la kisukari linaendelea kukua kila mwaka ambapo mwaka 2015 ilikadiriwa kuwa na wagonjwa milioni 415, mwaka 2017 wagonjwa milioni 425 na mwaka 2019 wagonjwa milioni 463.

 

Wakati hali ya kisukari ikiwa hivyo, upande wa VVU inaonesha kuwa maambukizi yake yanazidi kupungua kutokana na jitihada mbalimbali zinazofanyika kwani ripoti hiyo ya UNAIDS inaonesha ni watu milioni 38 pekee wenye virusi hivyo duniani.

 

HALI ILIVYO TANZANIA

Kwa upande wa Tanzania, ugonjwa huo wa kisukari ambao unatajwa kuathiri asilimia 50.1 ya watu duniani bila wao kujitambua kama wana tatizo hilo, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Homoni katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dk. Wolfagang Bernard alisema Watanzania milioni 1.5 wanakadiriwa kuwa na kisukari.

 

“Sasa utaona ongezeko la watu duniani ni mara mbili, lakini ongezeko la ugonjwa wa kisukari ni zaidi ya mara 150, huu ugonjwa wa kisukari unaongezeka kwa kasi sana na kasi hii ikiendelea makadirio yajayo ni kwamba mwaka 2030 yaani miaka 10 ijayo idadi ya watu wenye kisukari duniani itakuwa ni milioni 600 na miaka 25 ijayo mwaka 2045 idadi ya wagonjwa itakuwa watu milioni 700.

 

Aidha, alisema asilimia kubwa ya wagonjwa hao ni wale wanaoishi mijini kwa sababu hupunguza kuushughulisha mwili kwa mazoezi na hata kutembea umbali mrefu.

 

“Kwa Afrika kuna wagonjwa milioni 19, Tanzania ina wagojwa milioni 1.5, lakini sasa hawa ni wale waonajulikana kwa sababu wagonjwa wa kisukari hawaoneshi dalili sana,” alibainisha Dk Bernard.

 

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Kituo cha Kisukari – St. Laurent ambaye pia ni Mtafiti Mkuu Mwandamizi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dk. Mary Maige alisema mwaka 2012 walifanya utafiti nchi nzima na kubaini tatizo la kisukari linazidi kukua kwa kasi.

 

“Katika utafiti huo tulibaini kati ya watu 10, mtu mmoja ana kisukari na kati ya watu watano, mtu mmoja ana tatizo la kuchakata sukari mwilini hivyo tukabaini kuwa asilimia 20 ya watanzania wana matatizo ya kuchakata kisukari.”

 

Wakati hali ya kisukari ikiwa hivyo hapa nchini, kwa upande wa maambukizi ya VVU, jitihada zimezidi kuonesha matunda kwani kwa ujumla maambukizi ya Ukimwi yameshuka.

 

Kwa mujibu wa takwimu za Tume ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), maambukizi ya VVU mwaka 2003 /04 yalikuwa asilimia saba wakati mwaka 2016/17 yalikuwa asilimia 4.7.

 

Aidha, hivi karibuni Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Dk. Leonard Maboko alibainisha kuwa takwimu za mwaka 2016 zinaonesha kuwa watu milioni 1.4 ndio wenye VVU nchini.

 

WATALAAM WA AFYA WANASEMAJE?

Dk Wolfagang Bernard alishauri kuwa njia ya kuzuia ugonjwa wa kisukari ni kuzingatia mtindo bora wa maisha ikiwemo ulaji wa vyakula vinavyofaa na kufanya mazoezi.

 

“Njia ya kuzuia ni rahisi kufanya mabadiliko ya mtindo wa maisha kama kupunguza uzito, kufanya mazoezi, kuepuka kula vyakula vyenye sukari kwa wingi, kuepuka kunywa pombe, uvutaji wa sigara,” alisema Dk. Bernard.

 

Aidha, Dk Marry Maige aliongeza kuwa utumiaji wa sukari kwa wingi kama kuongeza sukari kwenye chai, kunywa juisi yenye sukari na vinywaji vingine vinachosha kongosho.

 

“Tunashauriwa hasa katika wakati huu wa mabadiliko ya maisha ni muhimu kufanya mazoezi walau dakika 30 kwa siku,” Dk Maige.TIBA ASILI KIBOKO HII HAPA

Hata hivyo, licha ya ugonjwa huo wa kisukari kuendelea kuwa tishio, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Dawa za Asili katika Kitivo cha Dawa Asili cha Chuo Kikuu Kishiriki cha Afya Muhimbili (MUHAS), Joseph Otieno, alisema tayari wamepata dawa mbili ambazo ni kiboko katika kudhibiti kisukari.

 

“Kuna dawa ambayo inatokana na lishe au mimea ambayo imeonekana kuwa na uwezo wa kupunguza kiasi cha sukari na kuregulate seli za kwenye bandama.

“Tayari tumezitengeneza na iko katika hatua za utafiti lakini tumeanza kuwapatia watu kama clinical observation, kwa hiyo tumetengeneza katika mfumo wa vidonge (capsules).

 

“Hii inaitwa Amoper, imetokana na vyakula kabisa imeonesha matokeo mazuri, lakini pia kuna ile juice inaitwa Morizela ambayo nayo ni lishe,” alisema.

Aidha, mmoja wa wagonjwa aliyezungumza na UWAZI, alithibitisha kutumia dawa hiyo aina ya Amoper na sasa hali yake imeanza kutengamaa.

 

Mgonjwa huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini, ameliambia UWAZI kuwa awali aligundulika kuwa na kisukari ambayo ilipanda hadi kufikia 21, lakini alipoanza kutumia dawa hiyo ya Amoper ndani ya mwezi mmoja tayari imeshuka hadi kufikia kiwango cha saba.

 

“Nilipewa dawa za kizungu lakini kama unavyojua zile zina sumu nyingi ndio maana nikapendelea hizi za asili na kweli matokeo yake ninaanza kuyaona,” alisema.

 

Wakati Muhimbili hali ikiwa hivyo, kwa upande wake Dk. Claudius Haule Ligendayika ambaye pia hutumia tiba mimea kutibu magonjwa mbalimali aliongeza kuwa kuna tiba ya kisukari aina ya pili na aina ya kwanza.

 

“Kuna tiba aina mbili za ugonjwa wa kisukari wa aina ya pili (diabetes type two) ambayo tiba yake ya aina ya kwanza haiponyeshi bali hushusha tu kiwango cha kisukari mwilini kwa njia ya kunywa dozi za kifamasia kama vile metformin, mega one na mega two.

 

“Lakini dawa hizi ukinywa pamoja na unga wa chai za mimea ya dawa ya mdalasini, mlonge, mstafeli na mchaichai, zitashusha kiwango cha sukari mwilini kwa kuzimeng’enya kikemikali zake na kuzigeuza kutoka kuwa sukari na kwenda kuwa kemikali za aina nyingine ambazo hazidhuru mwili kisha kupelekwa kwenye mkojo.

 

KISUKARI NI NINI

Dk. Marry Maige alifafanua kuwa kisukari ni kundi la magonjwa yanayohusiana na ufanyaji kazi wa mwili ambapo mtu anakuwa na kiwango kikubwa cha sukari aina ya glucose katika mwili kutokana na mwili wake kukosa uwezo wa kutengeneza insulin ya kutosha au seli za mwili wake haziwezi kutumia insulin iliyopo au pengine mwili kuwa na matatizo yote mawili kwa pamoja.

 

Alisema ugonjwa wa kisukari husababisha mgonjwa kupata haja ndogo mara kwa mara (polyuria), kusikia kiu kila wakati (polydipsia) na njaa (polyphagia).

HABARI; GABRIEL MUSHI, UWAZI

 

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO

Post a comment

0 Comments