Njia Waliyopita Tanzania U17 Hadi Kutwaa Ubingwa CosafaWIKIENDI iliyopita ilikuwa ni ya kitaifa zaidi kwenye anga la kimichezo, baada ya nyimbo za taifa kupigwa mara tatu katika maeneo tofauti. Dar es Salaam ulipigwa pale Next Door Arena, Hassan Mwakinyo akimkalisha Muargentina na kutetea taji la WBF.


Lakini kule Tunisia, uliimbwa tena wakati Taifa Stars walipokuwa wakisaka alama tatu katika harakati za kusaka tiketi ya kucheza Afcon mwakani kule Cameroon. Lakini pia juzi Jumamosi kule Afrika Kusini wimbo huo uliimbwa tena.


 


Uliimbwa ikiwa ni alama ya kuwa timu ya Taifa ya Wasichana wa U17, watakuwa wanashuka dimbani kucheza mchezo wa fainali dhidi ya Zambia kuwania taji la michuano ya Baraza la Vyama vya Soka vya Kusini mwa Afrika (Cosafa). Hatimaye wasichana hao walioshiriki kama wageni waalikwa, wakawapa furaha Watanzania kwa kutwaa taji hilo.


 


Tanzania waliwachapa Zambia kwa penalti 4-3 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1. Haikuwa rahisi kwa Tanzania kuyafikia mafanikio hayo ambayo mwaka jana yalifikiwa na dada zao wa U20, ambao walitwaa taji hilo kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya Zambia.


Sasa makala hii inakupitisha maeneo machache ambayo Tanzania walipitia hadi kutwaa ubingwa kwenye mchezo huo ambao ulikuwa wa kisasi. Mashindano hayo yalianza Novemba 3 hadi 14.


 


ZAIDI YA SIKU 30 KAMBINI


Moja ya kitu ambacho kilisaidia kuwaimarisha wasichana wa U17 ambao pia wanatumia jina la Tanzanite Queens, ni kambi ya muda mrefu ambayo walikaa wakati wakiwa wanajiandaa na mashindano ya kufuzu Afcon dhidi ya Senegal.


Kikosi hicho kinachonolewa na kocha Bakari Shime, kiliingia kambini Septemba 22 na kilikaa hadi Novemba 3, kisha kikaanza safari ya kuelekea Afrika Kusini kwenye mashindano ya Cosafa. Hiyo imeifanya timu hiyo kuwa ngumu na wachezaji kuweza kustahimili kukaa uwanjani kwa dakika nyingi wakicheza kwa kasi ileile kwa dakika zote 90.


 


WAANZA KWA KISHINDO COSAFA


Mchezo wao wa ufunguzi walicheza Novemba 4 dhidi ya Comoros na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 5-1. Mabao ya Aisha Masaka aliyefunga mawili dakika ya 20 na 59, Joyce Fred akifunga moja dakika ya 71, Mwamvua Seif dakika ya 82 na Protasia akifunga dakika ya 88.


Hii ikiwafanya vijana waamini kuwa kila kitu kitakuwa sawa na mambo yatakuwa lami hadi siku ya mwisho na hakuna timu ambayo itaweza kuwatingisha kwenye michuano hiyo.


 


WADUWAZWA NA ZAMBIA


Baada ya kupata ushindi mkubwa katika mchezo wa kwanza, Tanzania wakaduwazwa baada ya kujikuta wakipoteza kwa mabao 2-1 na Zambia kwenye mchezo wa pili uliopigwa Novemba 6. Baada ya kichapo hicho hesabu zikabadilika ghafla na sasa wakawa wanatakiwa kushinda katika michezo inayofuata ili waweze kucheza fainali.


 


KICHAPO CHA KIHISTORIA


Baada ya kupoteza katika mchezo dhidi ya Zambia, vijana wa Kitanzania hawakutaka kurudia makosa tena, wakagawa dozi ya mabao 6-1 kwa wenyeji Afrika Kusini. Aisha Masaka akaweka kambani mabao matano kwa mguu wake, akifunga dakika ya 21, 23, 39, 44 na 86, huku Mwamvua Seif akifunga dakika ya 18.


Hapo sasa hesabu zikawa angalau zimekaa sawa, ingawa wakawa wanahitajika kushinda mchezo unaofuata, tena ushindi wa mabao mengi. Sasa hawakufanya makosa, waliwachapa Zimbabwe michomo 10-1.


 


Protasia Mbunda alifungua dakika ya kwanza ya mchezo, Koku Kipanga akafunga la pili dakika ya 11, nahodha Irene Kisisa akaweka lingine dakika ya 13.


Shehat Mohamed (Manucho), dakika ya 18, 89 Ester Mabanza dakika 32, Zawad Athuman dakika ya 55 naye Aisha Masaka akafunga mabao mawili dakika ya 70 na 83 na yeye akawa amefikisha mabao 10 katika michuano hiyo, Joyce Lema akafunga bao la 10 dakika ya 88.


 


Watwaa kibabe Cosafa


Mpaka kufikia dakika ya 90+2, ilionekana kabisa Tanzania wameshapishana na ubingwa, ingawa kwa wakati wote huo lango la Zimbabwe lilikuwa katika hali mbaya, likiwa linashambuliwa kila mara.


Wale wachezaji wa akiba wa Zimbabwe wakaanza kushangilia baada ya kuona ubao unasoma dakika ya 93, kwa maana ziliongezwa dakika tano hivyo wakaona tayari shughuli imeisha.


 


Ghafla furaha yao ikaja kuzimwa kama kibatali dakika ya 94, baada ya Asha Masaka kuangushwa kwenye boksi na mwamuzi kuamua penalti. Koku Kipanga akauweka mpira kambani na kuipeleka mechi kwenye matuta.


Hatimaye hadithi ya Cosafa U17, ikahitimishwa kwa Tanzania kutangazwa kuwa mabingwa, baada ya kupata penalti 4-3.

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO

Post a comment

0 Comments