Dkt. Abbasi Awatembelea THT, Aahidi Kuenzi Ndoto za Ruge
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi, jana Desemba 4, 2020,   amekutana na wadau wa sanaa za ufundi na kuahidi kusimamia kivitendo hoja yao ya kutaka Watanzania wengi zaidi watumie kwa wingi sanaa za uchongaji, uchoraji na sanaa nyingine za ubunifu za hapa nchini.

 

Amejibu kero ya wadau wa sanaa hizo ya kutaka masoko zaidi kwa kuwaahidi kuwapatia wasanii hao eneo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ili kila kunapotokea michezo waonyeshe na kuuza kazi zinazoakisi utamaduni wa Mtanzania.

 

Pia ametembelea Tanzania House of Talents (THT), kituo cha ubunifu katika sanaa za muziki kilichoasisiwa na hayati Ruge Mutahaba, na kuiahidi familia ya Ruge iliyoohudhuria hapo, akiwemo mama yake mzazi, dada, kaka zake na wasanii wa THT, kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao kuhakikisha ndoto ya Ruge kusaidia kuinua vipaji vya vijana inaendelezwa.“Sisi wanadamu ndiyo tunafika mwisho lakini siku zote ndoto kuu hazifi, niko hapa leo kuwaahidi kuwa mimi na wenzangu wengine wengi nitakaowakusanya wakiwemo wasanii waliopita hapa THT tutashirikiana nanyi kuiendeleza THT,” alisema na kuagiza wizara yake kukiunganisha kituo hicho na Chuo cha Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TASUBA) ili kuwa na ushirikiano katika mafunzo kwa vijana wenye vipaji.

Aidha, ameahidi kutoa mchango wake katika vifaa vinavyohitajika katika kituo hicho.

 


HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO

Post a comment

0 Comments