Miaka 41 bila chanjo, dawa ya Ukimwi

 

Dar es Salaam. Wakati suluhisho la ugonjwa wa virusi vya corona, Covid-19, likielekea kupatikana, dunia bado inaendelea na vita ya kutafuta dawa na chanjo ya Ugonjwa Unaodhoofisha Kinga ya Mwili (Ukimwi) ambayo leo inatimiza miaka 41.


Ingawa Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema dunia imepiga hatua kubwa katika mapambano hayo, bado ugonjwa huo ni tatizo kubwa duniani, na linazidishwa na kuibuka kwa Covid-19 iliyosababisha rasilimali nyingi kugeuziwa kwake, huku uchumi ukidorora na hivyo kupunguza kasi ya uchangiaji vita hiyo.


“Covid-19 inatishia maendeleo ambayo dunia imepata katika masuala ya afya na yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, yakiwemo mafanikio dhidi ya Virusi vya Uvimwi,” anasema mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na VVU (Unaids), Winnie Byanyima katika ujumbe wake wa mwaka huu.


“Kama yalivyo magonjwa yanayosambaa duniani. hali ya kutokuwa na usawa inaongezeka; kutokuwepo na usawa wa kijinsia, rangi, kijamii na kiuchumi. Tunakuwa na dunia ambayo haina usawa zaidi.


“Najivunia kwamba kwa mwaka uliopita, wanaharakati wa VVU walihamasisha kutetea maendeleo yetu, kulinda watu wanaoishi na VVU na makundi mengine yaliyo katika hali hatarishi na kuzuia virusi vya corona”.


Byanyima anatoa ujumbe huo wakati watu wanaosihi na VVU walikuwa milioni 38 mwaka jana, huku watu milioni 1.7 wakiwa na maambukizi mapya mwaka huo, wakati vifo vilifikia watu 690,000 katika kipindi hicho, kwa mujibu wa takwimu za UNaids.


ADVERTISEMENT

Covid-19, ambao ni ugonjwa wa homa ya mapafu, iliibuka mwishoni mwa mwaka jana jijini Wuhan, lakini hadi sasa kampuni kubwa za dawa duniani za Pfizer na BioNTech zinasubiri idhini ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ili ainze kusambaza chanjo yake na kurejesha matumaini kwa nchi mbalimbali kuzindua uchumi.


Lakini wanachotegemea wagonjwa wa VVU ni dawa za kurefusha maisha za ARV, huku wasioambukizwa wakihimizwa kutumia mipira katika ngono, kutofanya ngono, kujiepusha na matumizi ya sindano moja kwa matibabu na kuepuka damu ya mtu mwingine kugusa michubuko.


Hapa nchini takwimu zinaonyesha kuwa takribani watu 72,000 hupata maambukizi mapya kwa mwaka.


“Hata hivyo alisema Tanzania imefanikiwa kupunguza vifo vitokanavyo na VVU na maambukizi mapya,” alisema mkurugenzi mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), Dk Leonard Maboko.


“Mwaka 2001 tulikuwa na takribani watu 130,000 walioambukizwa, hivi sasa maambukizi mapya yanafikia 72,000 kwa mwaka. Bado tunaichakata na tunaendelea. Mwaka jana 2019 imekuwa 68,400 bado maambukizi yanatokea. Lakini walioambukizwa wakipata dawa wanaishi muda mrefu.”


Mikoa inayoongoza kwa maambukizi ya VVU ni Njombe kwa asilimia 11.4, Iringa (11.3) na Mbeya asilimia 9.3.


Lakini hali si nzuri kwa vijana vijana balehe ambao yakwimu zinaonyesha 171,257 wanaishi na virusi vya Ukimwi. Hili ni kundi la vijana walio na umri kati ya miaka 15 hadi 24.


Takwimu za Tacaids zinaonyesha kuwa kwa siku zaidi ya watu 200 hupata maambukizi mapya ya vvu, huku kati yao 80 ni vijana.


Katika takwimu hizo inaonyesha wasichana wawili mpaka watatu wa rika hilo huambukizwa virusi hivyo kila baada ya saa moja.


Balozi wa vijana kutoka Tanzania Youth Alliance (Tayoa), Dk Lilian Mwakyosi alisema tatizo ni kubwa nchini hivyo imefika wakati wazazi waongee na mabinti zao ili kupunguza maambukizi mapya.


“Asilimia 32 ya maambukizi mapya yanatoka katika kundi la wasichana wa miaka 15 hadi 24. Kila baada ya saa moja mabinti wawili mpaka watatu wa umri huo wanapata maambukizi ya virusi vya Ukimwi,” alisema.


Takwimu pia zinaonyesha kuwa vijana waliopo vyuoni ndio wanaathirika zaidi kwa kupata maambukizi.


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Aboubakar Kunenge alisema takwimu zinaonyesha kiwango cha mambukizi mapya kwa mkoa huo kimepungua kutoka asilimia 10.9 mwaka 2007/2008 hadi asilimia 4.7 mwaka 2017/2018, akisema zinaongeza matumani kwa watendaji pamoja wadau wanaoangalia afua za ukimwi.


Wakati hali ikiwa hivi Tanzania, Ripoti iliyotolewa Machi 20 na UNAids inaonyesha kuongezeka kwa matibabu ya VVU. Hadi kufikia mwaka 2019 kulikuwa na zaidi ya watu milioni 24 waliokuwa wanaishi na vvu na wakiwa katika matibabu.


Ripoti hiyo pia inaonyesha hata hivyo kuwa ahadi nyingi zilizotolewa kuboresha maisha ya wanawake na wasichana kote duniani, hazijatekelezwa.


Wanawake wa kati ya umri wa miaka 15 na 49 na wanawake wa umri mdogo takribani 6000 wa umri wa miaka 15 hadi 24, wanapata VVU kila wiki.

 

Juhudi za chanjo bado


Wakati magonjwa mengine ya mlipuko yakichukua miezi 18 kupata chanjo, wanasayansi bado wanahangaishwa na kujua vizuri tabia ya virusi vya Ukimwi ili kutengeneza chanjo.


Mafanikio ambayo dunia imefanikiwa katika kupambana na changamoto za afya ni pamoja na kupata chanjo dhidi ya virusi vya ugonjwa wa kupooza, homa ya mapafu ya hepatitis A na B, virusi vya papilloma (HPV), ndui na tetekuanga.


Lakini kwa miaka 41 bado wanasayansi wanahaha kupata sukluhisho la virusi vya Ukimwi.


“Ni vigumu sana kuopata chanjo ya VVU kwa sababu ni tofauti na aina nyingine ya virusi. VVU haiendani na njia halisi za kutafuta chanjo,” inaandika tovuti ya healthline.com.


“Mfumo wa kinga ya mwili wa karibu binadamu wote ni pofu kwa VVU... chanjo huundwa kwa ajili ya kuigiza utendaji wa kinga ya mwili ya mtu aliyepona... chanjo hulinda dhidi ya magonjwa, si maambukizi, lakini VVU ni maambukizi hadi unapofikia hatua ya tatu au Ukimwi.”


Tovuti hiyo pia inaandika kuwa vikwazo vingine vinavyochelewesha kupatikana kwa chanjo ni ukweli kwamba virusi vya VVU vilivyouawa au kudhoofishwa haviwezi kutumika kutengenezea chanjo na kikubwa zaidi ni kwamba chanjo nyingi hukinga mwili dhidi ya virusi vinavyoingia mwilini kupitia mfumo wa hewa au wa kumeng’enya chakula, lakini Ukimwi huingia kupitia damu.


Hata hivyo, mafanikio yaliyopatikana katika kupambana na ugonjwa huo ni dawa zinazotumika kufubaza virusi vya Ukimwi na kumuwezesha mgonjwa kuishi maisha ya kawaida na marefu zaidi, tofauti na ilivyokuwa mwanzoni mwa miaka ya themanini wakati wagonjwa walipokuwa wakichukua miaka michache kufariki baada ya kuambukizwa.


Matibabu ambayo yanahimizwa ni ya dawa inayoitwa antiretroviral therapy (ART) ambayo inatakiwa itumiwe na kila mtu mwenye maambukizi. Dawa hiyo haitibu VVU lakini inaufanya ugonjwa huo udhibitike na pia kupunguza hatari ya kusambaza kwa wengine.


Pia wataalamu wamekuwa wakihimiza watu kupima afya mara wanapohisi kuambukizwa ili kuanza kuchukua tahadhari mapema ikiwa ni pamoja na kuanza kutumia dawa hizo za kufubaza.


Juhudi za kutafuta dawa na chanjo pia zitategemea juhudi za pamoja.

 

Ufadhili


Desemba 2019, mfuko wa dunia (Global Fund) ulitangaza mgao kwa nchi lengwa huku Tanzania ikipata Dola za Marekani 587,270,528 sawa na Sh1.333 trilioni kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa ukimwi, malaria na kifua kikuu kwa kipindi cha 2020/2022.


Katika gawio hilo Tanzania ilipewa kiasi cha Dola za Marekani 587,270,528 (Sh1.333 trilioni), Dola 364,840,423 (Sh828.19 bilioni) ilikuwa ni kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa Ukimwi.

Mwananchi

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO

Post a comment

0 Comments