Diamond Kwa Sasa Hana Baba, Ukweli Mchungu

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA



Kwa Mkono wa, Robert Heriel.


Tahadhari: Makala hii inaweza isimfae kila mtu, kwani lugha iliyotumika humu inaweza kuwa kali na yenye kuumiza kwa baadhi ya watu. Hivyo ikiwa wewe unajijua sio mvumilivu wa lugha ngumu, maneno makali basi nakusihi ishia hapa hapa kusoma. Na kama utaendelea basi ni wazi umejiona kuwa utahimili, hivyo sitahusika na maumivu au athari yoyote itakayokupata kisaikolojia.


Wiki hii kumekuwa na watu wengi mtandaoni hasa Youtube ambao wamemuandama Msanii mkubwa wa taifa hili aitwaye Diamond PLatnum kuhusu sakata lake na Baba yake, Mzee Abdul. Wengi wamekuwa wakimponda Diamond kwa kutomsaidia Baba yake, Mara sijui hamjali, sijui hampendi, sijui hamhudumii basi kila mmoja na maoni yake na jinsi uelewa wake ulivyo. Wanahaki ya kutoa maoni kwa kadiri akili yao inavyowatuma, lakini lazima jambo hili tulijadili kwa mapana yake.


Nimeandika makala hii kwa sababu, sio Diamond pekee ambaye hamtunzi Baba yake, yapo maelfu na maelfu ya vijana wasiotunza wazazi wao kwa sababu zao mbalimbali. Na ndio maana hata Mbunge wa Kahama Mjini, Mhe. Kishimba Mwaka jana kama sikosei alishawahi kupeleka hoja Bungeni kuhusu kuundwa kwa sheria ya lazima kwa watoto kusaidia wazazi wawapo wazee. Lakini leo tujajikita zaidi kujadili wale wasiohudumia baba zao au wazazi kwa sababu ya KUTELEKEZWA NA MMOJA WAZAZI AU WAZAZI WOTE.


Diamond ni kielelezo cha vijana wengi waliomo ndani ya taifa hili waliotelekezwa na Baba kama inavyofahamika na ilivyoelezwa. Hakuna jambo baya kama kutelekezwa iwe kwa sababu au bila sababu maalumu. Kumtelekeza mtoto inamuathiri kimakuzi yake, mtoto anakuwa anaishi bila kujiamini hata kama akiishi maisha ya kuaminishwa kuwa ajiamini. Mtoto anayetelekezwa na Mama au Baba huathitika kisaikolojia na mara nyingi baadaye huwa na roho ngumu mno licha ya kuwa anaweza kuwa na utu lakini kwa sehemu kubwa anaweza kuwa mkatili. Ni watoto wachache ambao wametelekezwa ambao wakiwa watu wazima hawana roho ngumu.


Baba anapomtelekeza mtoto kwa sababu yoyote ile bila kujali ni nzuri au mbaya. Mtoto huanza ku-assume kwamba hana Baba, na Baba yake alishakufa miaka mingi. Na hapa ndipo hatari inapoanza. Baba anaweza kufikiri anamtoto licha ya kumtelekeza lakini kwa upande wa mtoto yeye anajua hana baba, tena anaassume kama alishakufaga miaka mingi mno licha ya kuwa anakutanaga naye iwe barabarani au kwa kuongea na simu mara moja moja. Ukishatelekeza mtoto ni kujitengenezea mazingira ya mtoto kukuona MZIMU unayeishi duniani. Yaani mtoto akikuona anakuchukulia kama mzimu uliyekwisha miaka mingi mno. Kikawaida mtu akishakufa hana sehemu kwa waliohai, hivyo mtoto anakuchukulia kuwa huna msaada wowote, wewe ni mzimu tuu, ulishakufa na kuoza miaka mingi moyoni mwake.


Ninaongea jambo hili kwa uzoefu, sio kwa kuhadithiwa, naongea kitu ninachokielewa kwani nami ni sehemu mambo haya. Mzazi akishakutelekeza na kukuacha ukiwa tangu mdogo na hapa nazungumzia chini ya miaka saba kama sio kumi.

Baba hajui unasoma au husomi

Baba hajui unakula nini na unavaa nini

Baba hajui lini uliumwa na ulitumia madawa gani

Baba hajui hata bei ya pensel au daftari mapaka unamaliza shule

Baba hajui hata unamiaka mingapi

Baba hana anachojua kuhusu wewe zaidi ya kujua wewe ni mtoto wake


Baba hajali wala kuthamini kuwa wewe ni mwanaye, hajitoi kama Baba ili uone jitihada zake hata kama hana pesa au hana mali, hata kukutafuta na kukusalimia kila mara hiyo tuu hataki. Alafu kuna Mababa wengine mafala sana(Ninaweza kuwa hata mimi pia), unayakuta yanajadili kabisa ati mtoto akikua atakuja mwenyewe, mimi ni Baba yake tuu, Yaani kama punguani au mwehu. Nani aje, labda watoto wehu wasiojitambua, ukizingua unazinguliwa, ukijifanya kidume kutia mimba alafu hujui kulea alafu unasubiri toto likue ndio ulete kaptura yako hutaamini macho yako nakuambia, ukijifanya unatema laana zako uchwara tunakutimua na upuuzi wako, watishe wajinga huko, na huyo mungu mpumbavu aliyekufundisha kufanya upuuzi, mwambie hatumuogopi kwani tunajua hana atakaloweza kutufanya.


Sisi tunamuamini Mungu aliyeumba mbingu na nchi, Baba anayejua majukumu yake, ambaye anakutaka utunze familia yako ikiwemo na watoto. Kama ulimuasi huyo mungu sasa subiri matunda yake, huwezi vuna usipopanda.


Watu wanamtishia Diamond Ujinga ujinga, ati atapata Radhi sijui laana, yaani upuuzi upuuzi tuu. Diamond chochote atakachokifanya kwa Baba yake yupo sahihi, asipomhudumia yupo sahihi kwani naye hakuhudumiwa na wala hatapata radhi wala laana popote pale labda mukamloge ndio muiite Laana, maana waafrika ndio tabia zetu hizi, mnajifanya mnamlaani alafu kwa nyuma mnaenda kumloga ili akidhurika ionekane ni laana. Hakuna cha laana hapo wala ndugu yake Radhi. Huwezi vuna usipopanda, kama alimzaa ndio kisingizio basi naye kamzalia wajukuu, hiyo pia inatosha. Kama kuzaa ndio kigezo hata mbuzi anazaa na ng'ombe.


Wanaume tuache upumbavu wa kuzaa na kutelekeza watoto. Tunawapa shida hawa wanawake na watoto. Unazalisha mwanamke wa watu unamuacha, anahangaika na lawama,majina ya hovyo, kutukanwa huku na huko sijui single mother ni kiwanja chenye mgogoro, sijui mtoto haramu, na upuuzi upuuzi mwingine. Alafu toto limekua limefanikiwa unaleta putura yako bila haya.

Umesahau mwanamke wa watu alivyotukanwa ni single mother kama kiwanja chenye mgogoro.

Umesahau kuwa ulivyomzalisha mwanamke wa watu ukamtelekeza alivyopata tabu kupata mwanaume mwingine wa kumuoa na kujenga uaminifu kwake

Umesahau jinsi ulivyokuwa unapigiwa simu za matatizo ya mtoto utume hata mia ya nguo hupokei simu unajifanya huoni.

Umesahau hayo, alafu unatakwa ukumbukwe kwa mambo yapi?


Umesahau jinsi mtoto wako alivyoitwa mtoto haramu wakati ungemuoa mama yake au kuishi naye wala asingedhalilishwa hivyo

Umesahau jinsi mtoto wako alivyohangaika kujieleza kuwa wewe(Babaake) yupo wapi na anafanya kazi gani pindi alivyokuwa akiuliwa shule za msingi na sekondari, wewe umejificha huko hata hutaki mtoto wako akujue.

Umesahau yote hayo au unajifanya huyajui, sivyo?


Watoto karibia wote waliotelekezwa wanajua nazungumzia nini, wengi mioyo yao ilishasahau habari za wazazi waliowatelekeza, walisha-assume wamekufa na wale wanaowaona ni mizimu.

Hivi Baba mzima unakaa miaka mitano hupigi hata simu kwa mtoto au kwa mama yake unategemea mtoto akikua atakupigia mara kwa mara. Watu hawajui kuwa input is equal to output. Au hawajui kuwa maisha hutumia kanuni ya KIOO. Ukisimama mbele ya kioo, ukicheka na taswira yako itacheka, ukinuna tawira yako itanuna.

Huwezi mtelekeza mtoto miaka nenda rudi alafu kwa upumbavu wako utegemee mtoto akiwa mkubwa atakutafuta mara kwa mara, hiyo haipo na haijawahi kuonekana.


Hata walioko kwenye ndoa wenyewe ni mashahidi, mzazi mwenye mazoea na watoto(wengi huwa kina mama), mtoto akikua humtafuta mama zaidi kuliko Baba, na wapo watoto ambao huwatafuta baba zao kuliko mama zao na hii ni kutokana na mazoea tangu utotoni.


Kuna watu wanasema Diamond amsamehe Baba yake, wako sahihi kabisa.

Lakini nataka kuwaambia, na waliotelekezwa wote na wazazi wao ni mashahidi hapa; hata umsamehe mzazi aliyekutelekeza bado hamtakuwa na mazoea kama ilivyokawaida, kama mlikuwa hamuongei hamtaongea kabisa. Kwanza mtaongea nini na mtu ambaye hamna mazoea naye tangu ukiwa mdogo kabisa, mtaongea nini hasa. Unajua watu wanamlaumu Diamond lakini hawajui tuu mambo haya.


Kuhusu Kumtunza;

Diamond na watu wa aina yake wanayohiyari ya kuwatunza wazazi wao waliowatelekeza. Diamond anaweza akamtunza au asimtunze Baba yake. Kama Baba yake hakuchukua kuwa ni wajibu kumtunza mwanaye, Diamond yeye akiwa kama Baba, akafanya ni hiyari yake. Basi hata Diamond anaweza kuona sio wajibu wake kumtunza Baba yake bali ni hiyari yake.


Kuna watu wanadhani Diamond ataumia kama baya lolote litampata Baba yake, kama wewe ni mmoja wao basi unakosea sana. Watu kama Diamond waliotelekezwa na wazazi wao hakunaga upendo tena kwa Baba zao, yaani tayari wanaona kama hawana Baba, Baba zao walishakufa miaka mingi sana. Hawapati maumivu yoyote kwa lolote litakalo wapata Baba zao ikiwa tuu waliwatelekeza. Hivyo mtu anayedhani Diamond ataumia siku Baba yake akipata madhara ni kwamba haelewi mambo haya.

Moyo uliokufa hauwezi kuumia.


Diamond anamchukulia Baba yake kama watu wengine, wala hana kinachomuuma, hata akimsaidia, Baba Diamond asidhani anasaidiwa na mtoto wake bali ajue anasaidiwa na mtu baki.


Ukiona mtu alitelekezwa na mzazi wake iwe ni Baba au Mama na anajifanya anaupendo na Baba au Mama aliyemtelekeza wengi huwa ni wanafiki, wengi wanafanya hivyo kuogopwa kusemwa na jamii.


Wewe kama unauchungu na Baba, mhudumie Baba yako na Mama yako, usijifanye una uchungu wa mzazi kwa wazazi wasiokuhusu.


Tena Diamond alitakiwa asiwasiliane kabisa na Baba yake ili iwe fundisho kwa sisi wanaume wengine kuwa tutunze watoto wetu. Tena angetakiwa aende kumshtaki mahakamani kwa kumtelekeza ili atie adabu.

Lakini kusema amsamehe ni kufundisha vijana wadogo kutelekeza watoto alafu wanajua mwisho wa siku wataomba msamaha na watasamehewe..

Hatuwezi ishi hivyo, niliwahi sikia habari za Mwana FA ambaye sasa ni Mbunge wa Muheza naye alimzingua Baba aliyejitia ni Baba yake.


Wewe kama unauchungu na Baba wa mtu badala ya Baba yako, kamsaidie wewe.


Kuhusu laana ya Mungu, tutakutana kwa Mungu huko, mbele kwa mbele.

Waafrika wengi bado tuna mambo ya kipuuzi na kutishana kusiko na sababu, ati mzazi hakosei, hakosei yeye ni Mungu?

Mimi ni mzazi ninakosea mara kwa mara, kama ninyi wazazi msiokosea shauri yenu waambieni watoto wenu wajinga hivyo. Maana kuna viwazazi mshenzi vinajifanya miungu watu havikosei. Upumbavu mtupu. Mungu ndio hakosei sisi wengine Garagaja. Watoto wangu mimi Baba yenu ni mzazi lakini pia nakosea.

Nikizingua mnayohaki kunizingua mkinisamehe hiyo ni neema mmenipa. Nimemaliza.


ZINGATIA, Makala hii haimuhusu Baba Diamond na Diamond pekee bali jamii nzima, inahusu sisi wababa wote tuache kutelekeza watoto. Pia Makala hii imemchukulia Baba Diamond kama mtu aliyemtelekeza Diamond kutokana na kile kinachoendelea mitandaoni hivyo inaweza kuwa kweli au sio kweli. Kuhusu Wamama nitaandika siku nyingine.


WITO: Wababa tuache kutelekeza watoto kwa matokeo yake huweza kuja na athari mbaya. Pia watoto tuliotelekezwa tunaweza kusamehe kama inawezekana lakini tujiepushe na unafiki, kama huwezi kusamehe ni bora usisamehe kuliko kujifanya umesamehe alafu ukabaki na kinyongo ndani kwa ndani.


Ulikuwa nami;


Robert Heriel

Taikon wa Fasihi

0693322300

Kwa sasa, Dar es salaam

-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. UMESEMA KWELI KABISA HONGERA!!! UJUMBEE UWAFIKIE WANAUME WOTE!!

    ReplyDelete

Top Post Ad